
Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kumhusu Musa
5 May 2026
Samsoni alikuwa nani?
12 May 2026Ruthu alikuwa nani?
Wakristo wengi wanamfahamu Ruthu, mmoja wa wahusika wakuu katika kitabu cha Agano la Kale chenye jina lake. Ni simulizi inayojulikana na kupendwa na watu wazima na watoto sawia. Lakini hata kama tunaifahamu simulizi hiyo, ni vizuri kwetu kukumbuka Ruthu alikuwa nani, ili kutuchochea kuishi kwa uaminifu na kutuliza macho yetu kwa Mwokozi wetu, Yule ambaye Ruthu anamwashiria.
Mgeni
Jambo la kwanza tunalojifunza kumhusu Ruthu ni kwamba yeye ni mwanamke Mmoabi, aliyeolewa na mmoja wa wana wa Elimeleki na Naomi, ambao walikuwa wametoka Bethlehemu katika Yuda (Ruthu 1:1–4). Hili ni muhimu, hasa kwa kuwa Wamoabi hawakuruhusiwa “kuingia katika kusanyiko la Bwana” kwa sababu walishindwa kuwapa watu wa Mungu mahitaji walipotoka Misri na kwa sababu walimwajiri Balaamu kuwalaani watu wa Mungu (Kumbukumbu. 23:3–5). Israeli ilikatazwa “kutafuta amani yao au ustawi wao” (Kumb. 23:6).
Mjane
Pili, mume wa Ruthu alikufa katika nchi ya Moabu, akimuacha mjane bila watoto (Ruthu 1:5). Sio tu kwamba alihuzunika kwa kumpoteza mume wake, lakini pia baba mkwe wake na shemeji yake walikufa. Baada ya mateso, aliondoka katika nchi yake kuandamana na mama mkwe wake kwenda Bethlehemu, ambako njaa ilikuwa imekwisha na kulikuwa na chakula tena (Ruthu 1:6–7).
Binti Mkwe Mwaminifu
Tatu, wakati mama mkwe wake alipomsihi arudi nyumbani Moabu kabla hawajafika Bethlehemu, Ruthu alikataa. Hatimaye, shemeji yake alirudi, lakini Ruthu “alimshikilia [Naomi]” (Ruthu 1:14). Huu ulikuwa uamuzi wa gharama, hasa kwa kuwa Naomi hakuwa na wana wengine wa kumpa Ruthu kama mume. Ikiwa Ruthu angebaki naye, ilikuwa inawezekana sana kwamba angebaki mjane bila watoto. Hata hivyo, alijibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Kwa maana uendako nitakwenda, na ukaapo nitakaa” (Ruthu 1:16).
Mwanamke wa Imani
Njiani kuelekea Bethlehemu, Ruthu alitoa tamko la imani: “Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu” (Ruthu 1:16). Tamko hili lilithibitishwa na matendo yake ya kumcha Mungu katika siku zilizofuata. Kwa imani alianza kujipatia riziki kwa ajili ya Naomi na yeye mwenyewe: “Niruhusu niende shambani na kuokota masuke ya nafaka nyuma ya yule ambaye nitapata kibali machoni pake” (Ruthu 2:2). Kwa imani alifanya kazi kwa bidii mashambani (Ruthu 2:7). Boazi alimpongeza kwa yote aliyomfanyia mama mkwe wake, akambariki kwa maneno haya: “Bwana na akulipe kwa yote uliyoyafanya, na ujazwe thawabu kamili na Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye chini ya mbawa zake umekuja kutafuta kimbilio!” (Ruthu 2:12). Kwa imani Ruthu alitii mpango wa Naomi wa kumwomba Boazi amkomboe na kwa ujasiri alikwenda kwenye sakafu ya kupuria kumwomba Boazi amuoe (Ruthu 3:1–13). Kwa imani alisubiri kwa busara hadi jambo hilo litakapomalizika ipasavyo (Ruthu 3:18).
Mke na Mama Mwenye Kumcha Mungu
Ingawa Ruthu alikuwa amepitia mateso mengi katika maisha yake, Bwana alimzawadia kwa kumpa yule mtu ambaye alikuwa ameomba Bwana amlipe kwa matendo yake mema na uaminifu wake (Ruthu 2:12). Boazi, baada ya kutatua mambo ipasavyo, alimchukua Ruthu kuwa mke wake (Ruthu 4:10). Wazee na watu wa Bethlehemu walimbariki:
Bwana na amfanye mwanamke huyu, anayekuja katika nyumba yako, kuwa kama Raheli na Lea, ambao pamoja walijenga nyumba ya Israeli… nyumba yako na iwe kama nyumba ya Peresi… kwa sababu ya uzao ambao Bwana atakupa kwa mwanamke huyu kijana. (Ruthu 4:11–12)
Bwana aliwabariki Boazi na Ruthu kwa mtoto wa kiume (Ruthu 4:13). Kwa umuhimu, wanawake wa mji walimwita “mkombozi” na “mrejesha maisha” (Ruthu 4:14–15). Walimwomba Mungu kwamba jina lake “lingejulikana katika Israeli” (Ruthu 4:14). Pia walimwita Obedi, maana yake “mtumishi” (Ruthu 4:17).
Ukoo wa Yesu Kristo
Mwana wa Ruthu, Obedi, akawa “baba wa Yese, baba wa Daudi” (Ruthu 4:17). Kitabu cha Ruthu kinahitimisha na ukoo wa Daudi ili kutuonyesha ukoo wa Yesu Kristo:
Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi… na Salmoni baba wa Boazi kwa Rahabu, na Boazi baba wa Obedi kwa Ruthu, na Obedi baba wa Yese, na Yese baba wa Daudi mfalme. (Mathayo. 1:1, 5–6)
Yesu ni mkombozi na mtumishi mkuu zaidi kuliko Boazi na Obedi. Yeye ni mfalme mkuu zaidi kuliko Daudi. Anajulikana katika ulimwengu mzima:
Bwana aliniambia, “Wewe ni Mwanangu;
leo nimekuzaa.
Niombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako,
na miisho ya dunia kuwa milki yako.” (Zaburi. 2:7–8)
Tunapozingatia ungamo na tabia ya Ruthu, na tuchochewe kuelekea kwa uaminifu tunapomwangalia Yesu, Mkombozi wa watu wa Mungu, Yeye ambaye “hakuja kutumikiwa bali kutumikia, na kutoa maisha yake kuwa fidia kwa wengi” (Mathayo. 20:28).
Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.


