
Yesu Alitoa Ahadi gani Kabla ya Kupaa Kwake?
21 July 2026
Hamasa kwa ajili ya Upendo
21 July 2026Je, Inamaanisha Nini Kuwa “Ndani ya Kristo”?
Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo. Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu ili tuwe watakatifu mbele zake. Kwa upendo alituchagua tuwe wanawe kupitia kwa Yesu Kristo kulingana na makusudi ya mapenzi yake, kwa sifa ya Mungu kwa neema zake kuu alizotubarikia sisi katika Mwanawe Mpendwa. Ndani yake tunao ukombozi kupitia kwa damu yake, yaani msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote akitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo, ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani kuvitia vitu vyote vya mbinguni na duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo.
Katika Kristo sisi nasi tumepata urithi, tukisha kuchaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake ili, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Kristo, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake. Ninyi pia mliingia ndani ya Kristo mliposikia neno la kweli, Injili ya wokovu wenu. Baada ya kuamini, mlitiwa muhuri ndani yake, huyo Roho Mtakatifu mliyeahidiwa, yeye ambaye ni amana yetu ya kutuhakikishia urithi wetu hadi ukombozi wa wale walio milki ya Mungu, kwa sifa ya utukufu wake. (Waefeso 1:3–14)
Watu wanapokuuliza kuhusu imani yako, unajielezaje? Je, unaweza kusema, “Mimi ni Mpresbiteri” au “Mbaptisti”? Au labda, “Mimi ni Mepiskopali”? Au labda unasema tu, “Mimi ni Mkristo”?
Inawezekana haijawahi kuingia akilini mwetu kwamba kama tungeweza kuwauliza waumini wa siku za Agano Jipya wajieleze, huenda wasingejibu, “Sisi ni Wakristo.” Kwa kweli, neno Mkristo linatokea mara tatu tu katika Agano Jipya. Wanafunzi waliitwa “Wakristo” mara ya kwanza huko Antiokia (Matendo 11:26). badaye, Agripa alionekana kana kwamba analitamka kwa dharau neno hilo alipomuuliza Mtume Paulo, “Je, unanishawishi kwa haraka namna hii niwe Mkristo?” (Matendo 26:28). Na baadaye, katika waraka wake wa kwanza, Simoni Petro anazungumzia kuhusu mateso ya mtu kama “Mkristo” (1 Petro 4:16).
Katika miktadha hii mitatu, Mkristo pengine ni neno la dhihaka, hata “hotuba ya chuki” iliyobuniwa na wapinzani wa injili, kama vile neno Puritan lilivyokuwa katika karne ya kumi na saba. Inawezekana kabisa kwamba lilikuwa linatamkwa kwa dharau kama neno fundamentalisti leo. Haya ni “maneno ya chuki.” Ikiwa hivi ndivyo neno Mkristo lilivyoanza kutumika kwa kawaida, haishangazi kwamba katika Matendo ya Mitume, Luka anachagua kutumia neno “mwanafunzi” (kwa mfano, katika Matendo 6:1; kuna mifano zaidi ya dazeni mbili) au mara kwa mara anawataja waumini kama wafuasi wa “Njia” (Matendo 9:2; 22:4; 24:14), kwa kuwa walimfuata Yule aliyesema, “Mimi ndiye njia” (Yohana 14:6).
Lakini kama ungemuuliza Paulo, “Unajifikiriaje wewe mwenyewe?” jibu lake labda lisilingekuwa lolote kati ya hayo hapo juu, bali, “Mimi ni mtu ndani ya Kristo.”
Nakumbuka, nikiwa kijana mdogo, nikisoma 2 Wakorintho 12:1–10—sehemu ambayo Paulo anazungumzia ufunuo wa ajabu aliopokea na mwiba katika mwili uliomzuia kujivuna. Akianzisha kifungu hicho, anasema kwamba aliwahi kumjua “mtu ndani ya Kristo” ambaye alipata ufunuo wa ajabu wa maajabu na neema ya Mungu, ya kushangaza sana kiasi kwamba alihisi itakuwa si halali kuyafafanua kwa wengine. Nakumbuka nikijiuliza, “Ni nani huyu ‘mtu ndani ya Kristo’ asiyejulikana ambaye Paulo anazungumzia?” Labda nilikuwa mzito wa akil, lakini jibu lilinijia taratibu: Paulo anajizungumzia yeye mwenyewe! Hii ndiyo njia ya msingi anavyojieleza kwa sababu ndiyo njia ya msingi anavyojifikiria. Yeye ni “mtu ndani ya Kristo.”
Shika maneno haya “ndani ya Kristo” na maneno yanayofanana nayo (kwa mfano, “ndani yake”) akilini mwako. Kisha pitia haraka kurasa sitini au zaidi katika Biblia yako zinazohusisha nyaraka kumi na tatu za Paulo. Utakuta usemi “ndani ya Kristo” au badala yake zaidi ya mara themanini. Maneno yanayofanana “ndani ya Bwana” (au wakati mwingine “ndani ya Bwana Yesu”) ni karibu mara mbili ya idadi hiyo.
Ikiwa hujawahi kuliona hili hapo awali, huenda ukashangazwa na jinsi ambavyo Paulo hutumia misemo hii mara kwa mara, na ukajiuliza ni kwa nini hujawahi kuyapa umakini wa kutosha. Na bado inawezekana kuwa umekuwa ukisoma nyaraka za Paulo kwa miaka, hata miongo kadhaa, bila kugundua umuhimu wa usemi huu mdogo wa kihusishi ambao ni njia yake ya msingi ya kuelezea maana ya kuwa Mkristo.
Maneno haya mawili, kihusishi “ndani ya” kikifuatiwa na jina “Kristo,” yanaunda mada kuu ya kurasa hizi. Mwishoni mwa kitabu, unaweza kusamehewa kwa kufikiri kwamba haya ni maelezo marefu zaidi ya maneno mawili ambayo umewahi kusoma! Na bado kurasa hizi zitagusa tu juu juu ya fundisho hili tajiri na la ajabu. Lakini natumaini zitakutia moyo kuona, kutoka kwa mitazamo mbalimbali ya kibiblia, maana ya kuwa “ndani ya Kristo.” Ikiwa wewe ni wake, hivi ndiyo wewe ulivyo kweli na kwa hakika, kila siku ya maisha yako—mwanamume au mwanamke ambaye uko “ndani ya Kristo.”
Mwanafunzi mmoja wa Agano Jipya ameonyesha kwamba katika filamu ya The Godfather, neno Mafia halitumiki kamwe, na bado ni dhana ya msingi ya filamu nzima. Kwa njia sawa, hata wakati usemi huu maalum wa “ndani ya Kristo” hautumiki, kile kinachomaanishwa nacho ni msingi wa kila kitu ambacho Mtume Paulo anasema kuhusu kuishi maisha ya Kikristo. Na zaidi ya hayo, pia ni suluhisho la masuala mengi yanayomsumbua muumini binafsi au kusanyiko zima.
Agano Jipya halijawahi kufafanua maana ya kuwa “ndani ya Kristo.” Njia bora ya kuelewa umuhimu wake ni kutafakari vifungu mbalimbali vinavyoelezea kinachohusishwa. Hapa, jukumu letu kuu la msingi ni kujitambulisha na umuhimu wa kuwa “ndani ya Kristo.” Mojawapo ya njia bora za kufanya hivyo ni kwa kutafakari uwepo wake katika sura ya kwanza ya waaraka wa Paulo kwa Waefeso.
Constantine R. Campbell, Paul and Union with Christ: An Exegetical and Theological Study (Zondervan, 2012), 24n4
Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.


