
Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kuhusu Utakatifu
30 April 2026Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kumhusu Musa
Musa ni mmoja wa watu muhimu zaidi katika Biblia. Hapa kuna mambo matano ambayo pengine huyajui kumhusu:
1. Musa alikuwa mdogo kati ya ndugu watatu.
Dada yake, Miriam, alikuwa mkubwa kutosha kuwa macho ili kuona kitakachomtokea mtoto, na kisha kuingilia kati akiwa na binti wa Farao (Kutuka 2:1–10). Ndugu yake, Haruni, alikuwa mkubwa kwa miaka mitatu zaidi (linganisha Hesabu 33:39 na Kumbukumbu la Torati 34:6).
2. Maisha ya Musa yaligawanywa katika vipindi vitatu vya miaka arobaini kila kimoja.
Ingawa Kutoka 2 haikutaja, Matendo 7:23 inatuambia kwamba Musa alikuwa na umri wa miaka arobaini alipompiga Mmisri. Matendo 7:30 inatuambia kwamba miaka arobaini ilipita huku Musa akichunga kondoo jangwani kabla ya Mungu kumtokea katika kichaka kinachowaka moto. Kisha, Kumbukumbu la Torati 34:6 inatuambia kwamba Musa alikufa akiwa na umri wa miaka 120. Kwa hiyo Musa alikaa miaka arobaini huko Misri, miaka arobaini jangwani akichunga kondoo, na miaka arobaini jangwani akiwachunga Waisraeli.
3. Musa alioa mwanamke Mkushi (Hesabu 12:1).
Tunajua kwamba alimuoa Zipora, binti wa kuhani wa Midiani (Kutoka 2:16, 21). Lakini je, mke Mkushi aliyetajwa katika Hesabu 12 alikuwa Zipora? Wengine, kama vile Augustine na Calvin, wamechukua mtazamo kwamba Zipora na mke Mkushi alikuwa mwanamke yule yule. Wengine wamechukua mtazamo kwamba mwanamke Mkushi alikuwa mke wa pili kwa kuwa Kushi kawaida humaanisha Ethiopia. Kwa kuwa Biblia yenyewe haioni inafaa kutupa mwangaza zaidi juu ya jambo hili, lazima tuliache bila kuliamua.
4. Musa alikuwa “mpole sana, zaidi ya watu wote waliokuwa juu ya uso wa dunia” (Hesabu 12:3).
Kauli hii, ambayo inadhaniwa kutoka kwa Musa mwenyewe, inaonekana kujipinga. Je, mtu mpole au mnyenyekevu anaweza kuandika kuhusu upole wake mwenyewe ipasavyo? Wasomi wakosoaji wamechukulia kauli hii kuwa ishara kwamba haikuandikwa na Musa. Lakini ikieleweka ipasavyo, maoni haya ni muhimu katika muktadha huu. Miriamu na Aroni wamezua shambulio juu ya haki ya Musa ya uongozi. Badala ya kujibu kwa hasira na kinyongo, Musa alimruhusu Mungu kuzungumza kwa niaba yake. Kama tahariri ya Keil na Delitzsch inavyosema, “Kwa sababu alikuwa mpole zaidi ya watu wote, aliweza kwa utulivu kuacha shambulio hili juu yake kwa Hakimu mwenye hekima na haki yote, ambaye alimwita na kumstahilisha kwa ajili ya afisi yake.
5. Musa na Eliya walitokea pamoja na Yesu kwenye Mlima wa Kubadilika Sura (Mathayo 17:1–8; Marko 9:2–8; Luka 9:28–36).
Kwa nini Musa na Eliya walitokea pamoja na Yesu na si watu wengine wa Agano la Kale ni mada ya mjadala. Wengine wanaona kwamba Musa na Eliya wanawakilisha sheria na manabii, mtawalia. Pamoja, katika umbo la kibinafsi, wanawakilisha Agano la Kale lote. Wengine wanaona kwamba wanawakilisha vipindi viwili vikuu vya miujiza katika Agano la Kale. Mtazamo wangu ni kwamba Musa na Eliya walikuwa watu wawili katika Agano la Kale waliokutana na Bwana kwenye Mlima Sinai. Kwa hivyo inafaa kwao kukutana na Bwana katika kubadilika kwake, na hivyo kuthibitisha utambulisho wake wa kimasihi.
Makala haya ni sehemu ya mkusanyiko wa Misingi ya Ufuasi wa Kikristo.


