Mahali pa Maombi
19 June 2025
Tunamaanisha Nini Tunapozungumzia “Utakatifu wa Maisha ya mwanadamu”?
20 June 2025
Mahali pa Maombi
19 June 2025
Tunamaanisha Nini Tunapozungumzia “Utakatifu wa Maisha ya mwanadamu”?
20 June 2025

Toba Inaonekanaje?

xr:d:DAFXk0WDSFg:25,j:45162075609,t:23011320

Zaburi moja ya toba, Zaburi 51 iliandikwa na Daudi baada ya kukabiliwa na nabii Nathani. Nathani alitangaza kwamba Daudi alikuwa ametenda dhambi kubwa dhidi ya Mungu kwa kumchukua Bathsheba kuwa mke wake na kwa kumuua mume wake, Uria.

Ni muhimu kuona uchungu na majuto ya moyoni yaliyoonyeshwa na Daudi, lakini pia tunapaswa kuelewa kwamba toba ya moyo ni kazi ya Mungu Roho Mtakatifu. David anatubu kwa sababu ya ushawishi wa Roho Mtakatifu juu yake. Si hivyo tu, lakini anapoandika sala hii, anaiandika katika msukumo wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anaonyesha katika Zaburi 51 jinsi anavyosababisha toba mioyoni mwetu. Kumbuka hili tunapoitazama zaburi hii.

Zaburi 51 inaanza, “Ee Mungu, unihurumie, kwa kadiri ya upendo wako usiokoma, kwa kadiri ya huruma yako kuu, uyafute makosa yangu” (Zab. 51:1). Hapa tunaona kipengele ambacho ni msingi katika toba. Kawaida, mtu anapofahamu dhambi yake na kuiacha, hujiachilia kwenye rehema za Mungu. Tunda la kwanza la toba ya kweli ni kutambua haja yetu kubwa ya rehema. Daudi hamuombi Mungu ili apate haki. Anajua kwamba ikiwa Mungu angemshughulikia kulingana na haki, angeangamizwa mara moja. Kwa hiyo, Daudi anaanza ungamo lake kwa ombi la rehema.

Wakati Daudi anapomsihi Mungu kufuta makosa yake, anamuomba Mungu kuondoa doa kutoka kwenye roho yake, kufunika udhalimu wake, na kumsafisha kutoka kwenye dhambi ambayo sasa ni sehemu ya kudumu ya maisha yake. Kwa hiyo anasema, “Unioshe na uovu wangu wote na unitakase dhambi yangu!” (Zab. 51:2). 

Mawazo ya msamaha na utakaso yanahusiana, lakini si kitu kimoja. Katika Agano Jipya, Mtume Yohana anaandika, “Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote” (1 Yohana 1:9). Katika roho ya toba, tunakwenda mbele za Mungu na kukiri dhambi zetu, tukiomba siyo tu msamaha, bali pia nguvu za kujizuia kutoifanya dhambi hiyo tena. Kama Daudi anavyofanya katika zaburi hii, tunaomba kwamba mwelekeo wetu wa uovu uondolewe.

Daudi anaendelea, “Kwa maana ninajua makosa yangu, na dhambi yangu iko mbele yangu daima” (Zab. 51:3). Huku si tu kukiri hatia kwa kawaida. Yeye ni mtu anayesumbuliwa; anasema, “Najua nina hatia.” Hakuna jaribio la kupunguza hatia yake.  Hakuna jaribio la kujitetea. Hata hivyo, sisi mara nyingi ni mabingwa wa kutoa visingizio na tunaharaka ya kujitetea kwa kutoa kila aina ya sababu kwa tabia zetu za dhambi. Lakini katika maandishi haya, kwa nguvu za Roho Mtakatifu, Daudi anafikishwa mahali ambapo anakuwa mkweli mbele za Mungu. Anakubali hatia yake, akitambua kwamba dhambi yake ipo daima. Hawezi kuiondoa, na hili linamsumbua.

Kisha analia “Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi na kufanya yaliyo mabaya machoni pako” (Zab. 51:4). Kwa namna moja, Daudi anatia chumvi hapa. Ametenda dhambi mbaya sana dhidi ya Uria, familia na marafiki wa Uria, Bathsheba, na taifa zima la watu wa Mungu. Lakini Daudi anaelewa kwamba dhambi hatimaye ni kosa dhidi ya Mungu, kwa sababu Mungu ndiye pekee mkamilifu ulimwenguni. Kwa kuwa Mungu ndiye hakimu wa mbingu na dunia, dhambi zote zinafafanuliwa kwa misingi ya uvunjaji wa sheria ya Mungu na ni kosa dhidi ya utakatifu Wake. Daudi analijua hili na analikubali. Hapunguzi ukweli wa dhambi yake dhidi ya wanadamu, lakini anatambua umuhimu wa dhambi yake dhidi ya Mungu.

Kisha anatoa kauli ambayo mara nyingi hupuuzwa. Inapatikana katika sehemu ya pili ya mstari wa 4 na ni moja ya maelezo yenye nguvu zaidi ya toba ya kweli tunayopata katika Maandiko: “ili uthibitike kuwa wa kweli unenapo,na kuwa na haki utoapo hukumu.” (Zab. 51:4). Kimsingi Daudi anasema, “Ee Mungu, una haki kamili ya kunihukumu, na ni wazi kwamba sistahili chochote zaidi ya hukumu Yako na ghadhabu Yako.” Daudi anakubali kwamba Mungu hana lawama na ana kila haki ya kumhukumu. Hakuna kubishana au kujadiliana na Mungu.

“Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi, mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba kwa mama yangu. Hakika wewe wapendezwa na kweli itokayo moyoni, ndani sana ya moyo wangu wanifundisha hekima” (Zab. 51:5–6). Siyo tu kwamba Mungu anataka ukweli kutoka kwetu, anautaka kutoka ndani yetu kabisa. Daudi anakubali kwamba ameshindwa kufanya kile ambacho Mungu amekiagiza, na kwamba utiifu wake mara nyingi ni sherehe za nje tu badala ya matendo yanayotoka ndani kabisa ya nafsi yake.

Kisha Daudi anapaza sauti tena akiomba utakaso: “Nioshe kwa hisopo, nami nitakuwa safi, unisafishe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji” (Zab. 51:7). Tunaweza kusikia hali ya kutokuwa na msaada kabisa katika sauti ya Daudi. Daudi hasemi, “Mungu, subiri kidogo. Kabla ya kuendelea na mazungumzo haya katika sala, lazima nisafishe mikono yangu. Lazima nioshwe. Daudi anajua kwamba hawezi kujiondolea doa la hatia yake. Hawezi kuifidia. Lazima tuungane na Daudi katika kukubali kwamba hatuwezi kufidia dhambi zetu wenyewe.

Kupitia kwa nabii Isaya, Mungu baadaye alitoa ahadi hii,

Njooni basi tuhojiane,”asema Bwana.“Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu,zitakuwa nyeupe kama theluji;ingawa ni nyekundu sana kama damu,zitakuwa nyeupe kama sufu. (Isa. 1:18) Mungu anafurahia kutusafisha anapotupata na uchafu.

Kisha Daudi anasema, “Unipe kusikia furaha na shangwe” (Zab. 51:8a). Toba ni jambo lenye uchungu. Nani anafurahia kupitia ungamo la dhambi na kukiri hatia? Hatia ndiyo mharibifu mwenye nguvu zaidi wa furaha. Ingawa wakati huu Daudi hana furaha sana, anamuomba Mungu arejeshe nafsi yake na kumfanya ahisi furaha na shangwe tena. Anatoa hoja hii anaposema, “Acha mifupa uliyoivunja ifurahi” (Zab. 51:8b). Je, hicho si kifungu cha kuvutia? Anasema,

Mungu, umenivunja. Mifupa yangu imevunjika; haikuwa Shetani au Nathani aliyevunja mifupa yangu, bali wewe uliivunja mifupa yangu uliponihukumu kwa hatia yangu. Kwa hivyo, ninasimama mbele yako kama mtu aliyevunjika, na njia pekee ninavyoweza kuendelea ni ikiwa Utaniponya na kunirudishia furaha na shangwe.

Kisha anasema, “Ufiche uso wako usizitazame dhambi zangu, na uufute uovu wangu wote. Ee Mungu, uniumbie moyo safi, uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu” (Zab. 51:9–10). Njia pekee ya kuwa na moyo safi ni kwa kazi ya uumbaji mpya wa kiungu. Siwezi kujiumbia hilo ndani yangu. Ni Mungu pekee anayeweza kuumba moyo safi, na Yeye huumba mioyo safi kwa kuzifuta dhambi zetu.

Kisha Daudi analia, “Usinitupe kutoka mbele zako wala kuniondolea Roho wako Mtakatifu” (Zab. 51:11). Daudi anatambua kwamba hili ni jambo baya zaidi ambalo linaweza kumtukia mwenye dhambi yeyote. Anajua kwamba Mungu anaweza kututenga na uso wake ikiwa tutaendelea kuwa na moyo mgumu wa kutotubu. Yesu anaonya kwamba wale wanaomkataa wataondolewa kutoka kwa Mungu milele. Lakini sala ya toba ni kimbilio kwa muumini. Ni jibu la kiungu la mtu anayejua kuwa yuko katika dhambi. Aina hii ya itikio inapaswa kuashiria maisha ya wale wote ambao wameokolewa.

Daudi anaendelea, “Unirudishie tena furaha ya wokovu wako, unipe roho ya utii, ili initegemeze. Ndipo nitakapowafundisha wakosaji njia zako, na wenye dhambi watakugeukia wewe” (Zab. 51:12–13). Mara nyingi tunasikia kwamba watu hawapendi kuwa karibu na Wakristo kwa sababu Wakristo huonyesha mtazamo wa kujiona bora au mtazamo wa kujifanya watakatifu zaidi kuliko wengine. Lakini haipaswi kuwa hivyo. Wakristo hawana chochote cha kujivunia; sisi si watu wenye haki tunaojaribu kurekebisha wasio na haki. Kama mhubiri mmoja alivyosema, “Uinjilisti ni tu maskini mmoja akimwambia maskini mwingine mahali pa kupata mkate.” Tofauti kuu kati ya muumini na asiyeamini ni kusamehewa. Kitu pekee kinachomfanya mtu astahili kuwa mhudumu kwa jina la Kristo ni kwamba mtu huyo amepata msamaha na anataka kuueleza kwa wengine.

Ee Bwana, fungua midomo yangu, na kinywa changu kitatangaza sifa zako. Wewe hupendezwi na dhabihu, au ningaliileta, hufurahii sadaka za kuteketezwa. Bali dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika, moyo uliovunjika wenye toba, Ee Mungu, hutaudharau. (Zab. 51:15–17). Hapa ndipo tunapoupata moyo na roho ya toba ya kinabii kama inavyoonekana katika sura ya mwisho. Asili ya kweli ya toba ya kiungu inapatikana katika kauli hii “moyo uliovunjika wenye toba, Ee Mungu, hutaudharau.” Daudi anasema kwamba kama angeweza kufidia dhambi zake mwenyewe, angefanya hivyo; lakini kwa hali ilivyo, tumaini lake pekee ni kwamba Mungu angemkubali kulingana na rehema Zake.

Biblia inatuambia waziwazi na kutuonyesha kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba Mungu huwapinga wenye kiburi na huwapa wanyenyekevu neema. Daudi analijua hili kuwa kweli. Ingawa amevunjika jinsi alivyo, anamjua Mungu na jinsi Mungu anavyohusiana na watu wenye toba. Anaelewa kwamba kamwe Mungu hachukii au kudharau moyo uliovunjika na wenye toba. Hiki ndicho Mungu anachotaka kutoka kwetu. Hivi ndivyo Yesu alivyokuwa akifikiria katika Heri aliposema, Heri walio na huzuni, kwa maana “watafarijiwa” (Mathayo 5:4). Maandishi haya hayahusu tu kuomboleza kwa kumpoteza mpendwa, bali pia huzuni tunayoipata tunapohukumiwa na dhambi zetu. Yesu anatuhakikishia kwamba tunapohuzunika kwa sababu ya dhambi zetu, Mungu kwa Roho Wake Mtakatifu atatufariji.

Ningependekeza kwamba Wakristo wote waikariri Zaburi 51. Ni mfano kamili wa toba ya kiungu. Mara nyingi katika maisha yangu, nimemjia Bwana na kusema, “Niumbie ndani yangu moyo safi, Ee Mungu,” au, “Futa makosa yangu.” Nisafishe kwa hisopo. Nioshe na unifanye safi. Mara nyingi nimeomba, “Ee Bwana, nirudishie furaha ya wokovu wako,” na kulia, “Dhidi yako, wewe tu nimetenda dhambi.” Wakati tunapohisi kuzidiwa na ukweli wa hatia yetu, maneno yanatupungukia tunapojaribu kujieleza kwa toba mbele za Mungu. Ni baraka kweli kuwa na maneno ya Maandiko yenyewe midomoni mwetu katika nyakati hizo.

Dondoo hili linatoka kwenye kijitabu cha R.C. Sproul cha Maswali Muhimu Je,Toba ni Nini?.


Makala haya yalichapishwa kwanza katika Blogu ya Huduma za Ligonier.

R.C. Sproul
R.C. Sproul
Dkt. R.C. Sproul alikuwa mwanzilishi wa Ligonier Ministries, mchungaji wa kwanza wa mahubiri na mafundisho katika Saint Andrew’s Chapel huko Sanford, Fla., rais wa kwanza wa Reformation Bible College, na mhariri mtendaji wa gazeti la Tabletalk. Kipindi chake cha redio, Renewing Your Mind, bado kinapeperushwa kila siku katika mamia ya stesheni za redio ulimwenguni na kinaweza kusikilizwa mtandaoni pia. Alikuwa mwandishi wa vitabu zaidi ya mia moja, vikiwemo The Holiness of God, na Everyone’s a Theologian. Alijulikana ulimwenguni kote kwa utetezi wake mahiri wa Kutokukosea kwa Maandiko na uhitaji wa watu wa Mungu kusimama na ukweli wa Neno lake.