
Maana ya Kuondolewa Dhambi na Upatanisho ni Nini?
19 June 2025
Toba Inaonekanaje?
19 June 2025Mahali pa Maombi
Ni nini lengo la maisha ya Kikristo? Ucha Mungu huzaliwa kutokana na utiifu kwa Kristo. Utiifu hufungua utajiri wa uzoefu wa Kikristo. Maombi ndiyo yanayochochea na kukuza utiifu, yakiuweka moyo katika “hali sahihi ya kiakili” ya kutamani kutii.
Bila shaka, maarifa pia ni muhimu kwa sababu bila maarifa hatuwezi kujua kile ambacho Mungu anakihitaji. Hata hivyo, maarifa na ukweli vitabakia kuwa dhahania isipokuwa tunaposhirikiana na Mungu katika maombi. Ni Roho Mtakatifu anayefundisha, hamasisha, na kuangazia Neno la Mungu kwetu. Hupatanisha Neno la Mungu na kutusaidia kumjibu Baba katika maombi.
Maombi yana sehemu muhimu katika maisha ya Mkristo. Kwanza, ni sharti kamili la wokovu. Baadhi ya watu hawawezi kusikia; lakini ingawa ni viziwi, wanaweza kuokolewa. Wengine huenda wasiweze kuona; hata ingawa ni vipofu, wanaweza kuokolewa. Ujuzi wa Habari Njema–wokovu kupitia kifo cha upatanisho na ufufuo wa Yesu Kristo–utakuja kutoka chanzo kimoja au kingine, lakini katika uchambuzi wa mwisho, mtu lazima amuombe Mungu kwa unyenyekevu ampe wokovu. Sala ya wokovu ni sala moja ya waovu ambayo Mungu amesema ataisikia.
Je, wale walioko mbinguni wana nini lililo sawa kati yao? Mambo kadhaa. Wote wamehesabiwa haki, baada ya kuweka imani yao katika upatanisho wa Kristo. Wote wanamsifu Mungu. Na wote wameomba wokovu. Kutokuwa na maombi ni kutokuwa na Mungu, Kristo, Roho Mtakatifu, na tumaini na uhalisia wa mbinguni.
Pili, mojawapo ya alama za hakika za Mkristo ni maisha yake ya maombi. Mtu anaweza kuomba na asiwe ni Mkristo, lakini haiwezekani kuwa Mkristo na usiombe. Warumi 8:15 inatuambia kwamba kule kufanywa wana wa Mungu kiroho kunatufanya tuseme kwa sauti: “Abba!” “Baba”. Maombi kwa Mkristo ni kama pumzi ilivyo katika uhai, lakini hakuna jukumu la Mkristo linalopuuzwa sana kama hili.
Maombi, angalau maombi ya faragha, ni magumu kufanya kwa nia ya uongo. Mtu anaweza kuhubiri kwa nia ya uongo, kama vile manabii wa uongo wanavyofanya; mtu anaweza kushiriki katika shughuli za Kikristo kwa nia za uongo. Mengi ya mambo ya nje ya dini yanaweza kufanywa kwa nia za uongo, lakini ni jambo lisilowezekana kwamba mtu yeyote angeweza kuwasiliana na Mungu kwa nia isiyo sahihi. Mathayo 7 inatuambia kwamba katika “siku ya mwisho,” wengi watasimama kwenye hukumu na kumwambia Kristo juu ya matendo yao makuu na ya heshima yaliyofanywa kwa jina lake, lakini jibu lake litakuwa kwamba hawajui.
Kwa hivyo, tumealikwa, hata kuamriwa, kuomba. Maombi ni fursa na pia ni wajibu, na wajibu wowote unaweza kuchosha. Maombi, kama njia yoyote ya ukuaji kwa Mkristo, yanahitaji kazi. Kwa namna fulani, maombi si ya kawaida kwetu. Ingawa tuliumbwa kwa ajili ya ushirika na uhusiano na Mungu, athari za Anguko zimewaacha wengi wetu wavivu na wasiojali kuhusu kitu muhimu kama maombi. Kuzaliwa upya kunachochea shauku mpya ya ushirika na Mungu, lakini dhambi inapingana na Roho.
Tunaweza kupata faraja kutokana na ukweli kwamba Mungu anaijua mioyo yetu na anasikia maombi yetu ya kimya zaidi ya maneno yanayotoka midomoni mwetu. Wakati wowote tunaposhindwa kueleza hisia za kina na mihemko ya roho zetu au tunapokuwa hatuelewi kabisa ni nini tunachopaswa kuombea, Roho Mtakatifu hutuombea. Warumi 8:26-27 inasema,
Vivyo hivyo Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa. Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu. Wakati hatujui jinsi ya kuomba au nini cha kuombea katika hali fulani, Roho Mtakatifu hutusaidia. Kuna sababu ya kuamini kutoka kwa maandiko haya kwamba ikiwa tunaomba vibaya, Roho Mtakatifu anarekebisha makosa katika maombi yetu kabla ya kuyapeleka mbele ya Baba, kwa maana Kifungu cha 27 kinatueleza kwamba yeye “huombea watakatifu kulingana na mapenzi ya Mungu.”
Sala ni siri ya utakatifu–ikiwa utakatifu, kwa kweli, una kitu chochote cha siri ndani yake. Ikiwa tutachunguza maisha ya watakatifu wakuu wa kanisa, tunagundua kwamba walikuwa watu wakuu wa maombi. John Wesley aliwahi kusema kwamba hakuwa na maoni mazuri kuwahusu wahubiri ambao hawatumii angalau masaa manne kwa siku katika maombi. Luther alisema kwamba aliomba mara kwa mara kwa saa moja kila siku isipokuwa alipokuwa na siku yenye shughuli nyingi sana. Kisha aliomba kwa masaa mawili.
Kupuuza maombi ni sababu kuu ya kukwama katika maisha ya Kikristo. Zingtia mfano wa Petro katika Luka 22:39-62. Yesu alikwenda kwenye Mlima wa Mizeituni kuomba kama ilivyokuwa desturi yake na akawaambia wanafunzi wake, “Ombeni ili msije mkaingia majaribuni.” Wanafunzi walilala badala yake. Jambo lengine ambalo Petro alifanya lilikuwa kujaribu kupambana na jeshi la Kirumi kwa upanga; kisha akamkana Kristo. Peter hakuomba na matokeo yake yalikuwa kuingia katika majaribu. Lililo kweli kwa Peter ni kweli pia kwa sisi sote: tunaanguka faraghani kabla hatujaanguka hadharani.
Je, kuna wakati sahihi na usio sahihi wa kuomba? Isaya 50:4 Asubuhi ni wakati wa kipekee ambapo Mungu huwapa watu wake shauku ya kusali kila siku. Lakini kuna vifungu vingine vinavyotoa nyakati za maombi kuwa wakati wote wa siku. Hakuna sehemu ya siku iliyowekwa kando kuwa takatifu zaidi kuliko nyingine. Yesu aliomba asubuhi, wakati wa mchana, na wakati mwingine usiku kucha. Kuna ushahidi kwamba alikuwa na wakati uliotengwa kwa ajili ya maombi; hata hivyo, kwa kuzingatia uhusiano ambao Yesu alikuwa nao na Baba, tunajua kwamba ushirika kati yao haukuwahi kukoma.
1 Wathesalonike 5:17 inatuamuru kuomba bila kukoma. Inamaanisha kwamba tunapaswa kuwa katika hali ya ushirika wa kudumu na Baba yetu.
Makala haya yalichapishwa kwanza katika Blogu ya Huduma za Ligonier.


