
Jinsi ya Kusoma Sheria za Kibiblia
3 February 2026
Jinsi ya Kusoma Ushairi wa Kiebrania
10 February 2026Je, Theolojia ya Kimfumo Inasaidia?
Nakumbuka mkutano niliokuwa nao miaka kadhaa iliyopita na ndugu kadhaa katika Kristo. Tulihitaji kumpata mzungumzaji kwa ajili ya mkutano wa wanaume wakujipumzisha. Mwanamume mmoja alisema, “Jambo la mwisho tunalotaka ni theolojia. Tunahitaji vitendo.” Mara nyingi, huo ndio mtazamo: theolojia haisaidii. Lakini mkutano huo ulipomalizika wakupumzika, mzungumzaji alionekana kuwa wa msaada sana hasa kwa sababu aliitumia theolojia. Alifundisha mafundisho ya Neno la Mungu kwa ufasaha, kwa msimamo, na kwa kuwapa changamoto ya kuitikia walioskia.
Theolojia Inayosaidia ni Nini?
Theolojia ni kufikiri kwa makini kuhusu mafundisho ya Kikristo. Mafundisho ya imani yanatoa muhtasari na kueleza mafundisho ya Maandiko Matakatifu. Biblia inahimiza “mafundisho yenye uzima” (Tito 2:1), ambayo yanamaanisha mafundisho yenye afya.
Theolojia ya kimfumo ni uchunguzi wa yale ambayo Biblia nzima inafundisha kuhusu mafundisho fulani na uhusiano wake na mafundisho mengine. Kwa mfano, mwenye dhambi anawezaje kuhesabiwa haki au kuhesabiwa kuwa mwenye haki na Mungu? Kuhesabiwa haki kunatuonyesha nini kumhusu Mungu, Kristo, na sisi wenyewe?
Kusudi la theolojia ya kimfumo, kama mafundisho yote ya Kikristo, si kusababisha mabishano bali kuimarisha imani na utauwa (1 Tim. 1:4–5). Kama wanatheolojia wa Mageuzo walivyosema, “Theolojia ni mafundisho ya kuishi kwa Mungu kupitia Kristo.”
Lakini hiyo haimaanishi kwamba theolojia yote ni ya manufaa. Nilipofungua kitabu cha kwanza cha theolojia ya kimfumo nilichowahi kusoma, nilifikiri, “Hii ni nzuri! Mwandishi anafikiria kwa kina kuhusu imani.” Lakini katika kitabu hicho, mwandishi alisema kwamba ni upuzi kuzungumzia ufufuo wa mwili wa Kristo kutoka kwa wafu. Mwandishi alikuwa si muumini. Si lazima niseme, nilikiweka kitabu hicho chini.
Theolojia ya kimfumo ni ya msaada tu ikiwa ni aminifu kwa Neno la Mungu, hasa injili kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu na akafufuka kutoka kwa wafu (1 Kor. 15:3–4). Kwa hiyo, tunapaswa kutumia utambuzi. Tunaweza kujifunza kitu kutoka kwa karibu yeyote, hata wasioamini. Lakini tunapojifunza mafundisho na theolojia, lazima tuchague walimu wetu kwa busara.
Kwa nini Theolojia ni ya Msaada?
Theolojia ya kimfumo ni ya msaada kwa sababu maarifa ni ufunguo wa kukua katika neema (2 Petro 1:2; 2 Petro 3:18). Kiini cha uzima wa milele ni kumjua Mungu (Yohana 17:3). Mtume Paulo alithamini maarifa ya Kristo zaidi ya vitu vingine vyote (Fil. 3:8). Paulo alijiona mwenye bahati kuhubiri “utajiri usioweza kuchunguzwa wa Kristo” (Efe. 3:8).
Mara nyingi sana, tunapitia tu maisha bila kufikiria kwa nini tunafanya kile tunachofanya. Theolojia ya kimfumo inapata kutoka kwenye Biblia majibu ya maswali makubwa ya maisha. Mungu ni nani? Kusudi lake kwa ulimwengu ni nini? Mimi ni nani? Kwa nini nipo hapa? Kwa nini kuna uovu? Ninawezaje kuushinda? Ni watu gani wanaoweza kunisaidia? Historia inaelekea wapi?
Zaidi ya yote, theolojia ya Kikristo ni njia ya kumjua Mungu wa Utatu: Baba katika upendo wake wa milele, Mwana katika neema yake ya wokovu, na Roho Mtakatifu katika ushirika mzuri anaotupa na Mungu na sisi kwa sisi (2 Kor. 13:14). Maarifa ya Bwana yana thamani zaidi kuliko hekima yote ya kibinadamu, nguvu, na utajiri (Yer. 9:23–24). Mungu hutumia Neno lake kutuweka huru na kututakasa, kama Yeye alivyo mtakatifu (Yohana 8:31–32; Yohana 17:17).
Tunawezaje Kusoma Theolojia kwa Njia Inayosaidia?
Wajibu wa kufanya theolojia iwe ya msaada hauko kwa mwandishi pekee. Msomaji pia ana kazi ya kufanya. Hapa kuna vidokezo vya jinsi ya kutumia theolojia ya kimfumo kwa ufanisi.
1. Soma theolojia ili kulisha upendo wako, si kiburi chako.
Maarifa yanaweza kutufanya tujivune kwa kiburi, lakini ikiwa nia yetu ni upendo tutalenga kujenga watu wengine (1 Kor. 8:1).
2. Soma theolojia na Biblia ikiwa wazi.
Angalia marejeo ya Maandiko. Yasome katika muktadha. Kuwa kama Waberoya, ambao walikuwa “wakichunguza Maandiko kila siku” ili kuthibitisha kile walichosikia (Matendo 17:11).
3. Soma theolojia kwa maombi.
Usisome tu kumhusu Mungu; soma ukiwa katika uwepo wa Mungu. Mtafute Mungu unaposoma. Lisha nafsi yako kwa utukufu na neema yake (Zab. 63:5–8). Mpende Mungu kwa “akili yako yote” (Marko 12:30).
4. Soma theolojia kwa imani katika Kristo. Kristo ni Neno, mfunuaji wa Mungu (Yohana 1:1, 18).
Mtegemee Yeye kufungua akili yako kuelewa Neno (Luka 24:45).
5. Soma theolojia kwa umakini na tafakari (2 Tim. 2:7).
Tunasoma vitabu vingine haraka kwa ajili ya kupata maarifa machache. Lakini theolojia nzuri ya kimfumo inafaa kusomwa kwa makini.
6. Soma theolojia ukijua mipaka yako.
Wewe si Mungu. Kwa hiyo, ni upumbavu kufikiri kwamba unaweza kumwelewa Mungu kikamilifu (Zab. 145:3). Lakini wewe ni mwanadamu uliyoumbwa kwa sura ya Mungu (Mwa. 1:27). Kwa hiyo, kwa neema ya Kristo unaweza kumjua Mungu (1 Yoh. 5:20).
7. Soma theolojia kwa ajili ya kumsifu Mungu.
Mara kwa mara mpe Mungu sifa na shukrani kwa kile anachofunua kuhusu Yeye mwenyewe (Zab. 119:164). Hiyo inafanya theolojia kuwa kionjo cha mbinguni!
Makala hii ni sehemu ya mkusanyiko wa Hemenitiki (taaluma ya ufasiri wa Biblia).


