Faraja ya Mkristo katika mauti ni ipi?

10 September 2026

Faraja ya Mkristo katika mauti ni ipi?

10 September 2026

Kwa nini tabia ni muhimu katika utumishi?

Mungu ni mwenye uweza, mwenye upendo, tena mwenye wivu kwa ajili ya utukufu wa jina lake kuu. Katika Isaya 44:23–24, Bwana anajiita “Mkombozi” na kutangaza kwamba amewaokoa watu wake na kwamba “atatukuzwa katika Israeli.” Hakika, Mungu hutukuzwa kwa namna ya kipekee kupitia kwa wokovu wa wenye dhambi..

Kwa nini, basi, wenye dhambi wengi zaidi hawaokolewi? Kwa nini makanisa mengi yanayohubiri injili kwa uaminifu hapa duniani hayafuriki? Kwa nini mikusanyiko mingi ya waamini haijai wanaume, wanawake, na watoto wenye njaa na kiu ya haki? Kwa ufupi, uamsho wa kiroho ambao Wakristo wanautamani kuuona uko wapi?

Ukosefu wa uamsho miongoni mwa watu wa Kristo, na ukosefu wa utakatifu miongoni mwa viongozi wa Kristo, mara nyingi huenda sambamba.

Hakika, kuna sababu nyingine zinazofanya kazi. Makanisa yanayofifisha injili hayatashuhudia uongofu wa kweli kwa wingi. Wachungaji wanaokumbatia burudani hawatasababisha mikusanyiko ya waumini kububujikwa na machozi. Viongozi wa Kikristo wanaopuuzia toba watapata waongofu wa kweli wachache.

Pamoja na hayo, ni kweli vilevile kwamba wahubiri wanaopuuza tabia zao binafsi wasitarajie kuona uamsho katika makanisa yao. Mungu, katika hekima yake ya enzi kuu, ameonyesha kwamba inapokuja suala la ukuaji wa Kanisa Lake, haki ya kimaadili ya viongozi wake ni muhimu.

“Wokovu ni wa Bwana!”

Je, vipi kumhusu Yona? Ilibidi aliburutwe kwa nguvu akipiga mateke na kelele mpaka Ninawi,  hata hivyo mji mzima ukaamini hata kupata wokovu. Je, vipi kumhusu Yeremia? Mtu huyo wa Mungu alihubiri kwa moyo wake wote, bali alikubana na kukataliwa na taifa zima—taifa lililojua vyema la kufanya zaidi. Je, vipi kumhusu Petro? Huyu Mtume mwenye mapungufu alitoa mahubiri yenye nguvu kwenye Pentekote huko Yerusalemu, na maelfu wakaamini hata kupata wokovu. Na, mwisho, je, vipi kumhusu Mwokozi wetu asiye na dhambi? Aliishi maisha makamilifu lakini akakutana na kukataliwa, sio uamsho.

Mifano kama hii inathibitisha kwamba kile Yona alichotangaza ni kweli: “Wokovu watoka kwa Bwana!” (Yona 2:9). Ukweli rahisi ni kwamba hatuwezi kuanzisha uamsho. Hakuna kiwango chochote cha mafundisho sahihi, mahubiri ya uaminifu, na tabia isiyo na lawama kinachohakikishia uongofu wa hata nafsi moja. Mungu ni mkuu juu ya wokovu, na huo ndio mwanzo na mwisho wa jambo hilo. Majina ya wote watakaookolewa kesho yameandikwa katika Kitabu cha Uzima cha Mwanakondoo. Wateule wa Mungu watakuja kwenye imani ya wokovu kwa wakati wake mkamilifu.

Na Hata hivyo . . .

Na hata hivyo, Mungu wetu mkuu ameamua si tu mwisho wa wokovu, bali pia njia za kuufikia wokovu huo. Katika zaidi ya kifungu kimoja cha Agano Jipya, wazee wanahimizwa kuwa watakatifu kwa ajili ya kanisa. Wachungaji hawapaswi kutarajia huduma yenye matunda ikiwa wao wenyewe si vielelezo vya Uaminifu katika huduma.

Zingatia maagizo ya Petro kwa wazee katika 1Petro 5:2–3:

Lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe; si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika.Msijifanye mabwana juu ya wale walio chini ya uangalizi wenu, bali kuweni vielelezo kwa hilo kundi.

Kwa nini wachungaji hawa lazima wawe mfano kwa kondoo? Je, haitoshi kwa mhubiri kusema yaliyo kweli na sahihi tu? La, haitoshi. Je, kweli yanajalisha anayotenda anapokuwa faraghani nyumbani? Ndiyo, kweli yanajalisha sana.

Si ajabu, basi, kwamba Mtume Paulo alimwambia Timotheo kwamba hata wokovu wa wasikilizaji wake ulitegemea maisha yake na mafundisho yake: “Jilinde sana nafsi yako na mafundisho yako; Dumu katika hayo, kwa maana kwa kufanya hivyo, utajiokoa wewe mwenyewe pamoja na wale wanaokusikia” (Timotheo 4:16). Bila shaka, Paulo alijua kuwa wokovu ni wa Bwana; na hata hivyo, katika utoaji wa ajabu wa Mungu, chombo cha kutangaza Injili kinapaswa kuwa safi.

“Mtumishi mtakatifu ni silaha ya kuogofya.”

Mchungaji wa Kiskoti Robert Murray M’Cheyne alimwamini Kristo baada ya kifo cha ghafla cha kaka yake mkubwa. Alihitimu taaluma ya theolojia mwaka 1835 akiwa na msukumo wa “kumkimbilia Bwana” kwa bidii kadiri ya siku alizopewa. “Maisha yanatoweka upesi,” aliandika muda mfupi kabla ya kuwa mchungaji wa Kanisa la Mtakatifu Petro, Dundee, “fanyeni haraka kwa ajili ya umilele.” Umilele ulimfikia mapema kuliko ilivyotarajiwa: alikufa akiwa na miaka ishirini na tisa, lakini si kabla ya kujifunza umuhimu wa maisha matakatifu ya kibinafsi.

M’Cheyne aliwahimiza wachungaji wenzake wawe mifano kwa makundi yao. Akawasihi waangalie maisha yao na mafundisho yao:

Zaidi ya yote, ustawishe roho yako mwenyewe. Nafsi yako ndiyo jukumu lako la kwanza na kuu kabisa. Tafuteni kuongezeka katika utakatifu wa kibinafsi. Mungu habariki sana vipaji vikubwa bali hubariki mfanano na Yesu. Mtumishi mtakatifu ni silaha ya kutisha katika mkono wa Mungu. Neno moja utakalolinena wakati dhamiri yako iko wazi, na moyo wako umejaa Roho wa Mungu, lina thamani kuliko maneno elfu kumi yanayonenwa katika kutokuamini na dhambi.

Mungu hajali tu yale tunayosema; pia anajali sisi ni watu wa namna gani. Hivyo hatupaswi kushangaa Bwana anapoondoa mkono wake wa baraka juu ya huduma pale dhamiri ya kiongozi wa Kikristo inapokuwa imefifia, na moyo wake kwa upumbavu umezama katika mielekeo ya dhambi.

Hapana, hatuwezi kuleta uamsho kupitia mafundisho sahihi na maisha matakatifu, wala hatupaswi kutarajia uamsho bila hayo.

  1. Iain H. Murray, “Robert Murray M’Cheyne: Minister of St. Peter’s, Dundee, 1836–1843.” Banner of Truth, Novemba 12, 2001. Ilichapishwa awali katika Jarida la Banner of Truth, Na. 4 (Desemba 1955): 4. 14–23, https://banneroftruth.org/us/resources/articles/2001/robert-murray-mcheyne/?srsltid=AfmBOoolrEO61gcLnQA4_I3SOY_fnC_R9ObxJVVdQ16wfUcbrYmhmcJ9. ↩

Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.

Aaron Menikoff

Aaron Menikoff

Dkt. Aaron Menikoff ni mchungaji wa Mount Vernon Baptist Church huko Sandy Springs, Georgia, na profesa mshiriki wa historia ya kanisa katika Reformed Theological Seminary huko Atlanta. Yeye ni mwandishi wa Character Matters, Politics and Piety, na mwandishi mwenza wa Prioritizing Missions in the Local Church.