Ukomavu wa Kikristo ni nini?

24 September 2026

Ukomavu wa Kikristo ni nini?

24 September 2026

Nguvu ibadilishayo ya utakatifu wa Mungu katika maisha ya kila siku

Wiki chache baada ya kumgeukia Kristo, marafiki zangu wengi walikuwa na maswali—hasa kuhusu maana ya jambo hilo katika maisha yangu ya mbeleni: Je, bado ningeendelea kutoka na kwenda kwenye burudani za usiku? Je, niliruhusiwa kunywa? Swali moja lililojitokeza sana katika zile siku za mwanzo liliulizwa na baba wa rafiki yangu. Alinikaribia na kuniuliza, “Inakuwaje kujua kwamba kwa maisha yako yote, watu wote watakuwa nje wakiburudika na kufurahia maisha huku wewe ukikiishia kwenda kanisani tu?” Sasa nikitazama nyuma, nacheka kwa swali la aina hiyo, lakini wakati ule lilinifanya nijiulize kimyakimya: Je, nilikuwa tayari (na naweza) kuyaacha maisha yangu ya anasa? Je, nilikuwa tayari kuitumia siku ya Jumapili kanisani? Je, mimi, nikimnukuu Mtume Paulo kwa muhtasari, nilikuwa tayari kuyasahau mambo yale yaliyopita, na kukaza mwendo kufikia yale yaliyo mbele? (Wafilipi 3:13).

Mazungumzo kama hayo hapo juu yamejitokeza mara nyingi katika zaidi ya miaka thelathini ya kumfuata Kristo, na msisitizo unaorudia kila ninapokabiliwa na maswali hayo umekuwa wa kidunia. Daima yamenihusu mimi na tamaa zangu—mimi ni nani, na ninachotaka. Hayajawahi kumhusu Mungu na matamanio yake—yeye ni nani, na anachotaka. Hili halishangazi; hatupaswi kamwe kutarajia mtu asiyeamini kufikiri zaidi ya ulimwengu wa mambo ya kimwili. Mambo haya yanaweza kueleweka tu na wale walioungana na Kristo. Kama Paulo asemavyo, “Mtu ambaye hana Roho hawezi kupokea mambo yanayotoka kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa upambanuzi wa rohoni” (1Kor. 2:14).

Hii inanileta kwenye mada ya makala haya: nguvu ya utakatifu wa Mungu ibadilishayo. Baada ya miezi michache tangu niwe Mkristo, ilikuwa wazi kwangu kwamba hamu yangu ya kuacha mambo ya ulimwengu huu na badala yake kufuata utakatifu ilitegemea tajiriba ya maarifa yangu kumhusu Mungu katika Kristo.  Kadiri uelewa wangu wa Mungu ulivyozidi kuongezeka, ndivyo jitahida zangu za kufanana naye zilivyoongezeka. Hii ni kweli hasa inapohusu utakatifu wa Mungu.

Utakatifu wa Mungu si sifa tu—ndiyo msingi na kiini cha nafsi yake. Ni usafi wake ulio timilifu, ukamilifu wa maadili, na kujitenga kwake kabisa na chochote cha kawaida au kilicho najisi. Kama mwanatheolojia Louis Berkhof alivyoeleza, Mungu mtakatifu ni “aliye tofauti na viumbe vyote vyake, na aliyeinuliwa juu yao katika ukuu usio na kikomo.”¹ Utakatifu ndiyo sifa pekee ya Mungu iliyosisitizwa kwa kurudiwa mara tatu: “Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu” (Isaya 6:3; Ufunuo 4:8). Tangazo hili la utakatifu mara tatu linasisitiza kwamba Mungu ametengwa kabisa—hakuna aliye kama Yeye. Joel Beeke analifafanua hivi: “Ametengwa kwa utukufu wake, kwa ajili ya utukufu wake. . . . Yeye ni mtakatifu kwa sababu ya alivyo kama Mungu, [na Yeye] ni mtakatifu kwa sababu amejitolea kwaghera kudhihirisha jinsi alivyo katika kila analofanya.”²

Kinyume na utakatifu wetu, wenye dosari na usio thabiti, utakatifu wa Mungu ni wa milele na haubadiliki. Hufafanua kila kitu anachofanya.. Kwa mfano, pendo la Mungu ni takatifu; haki yake ni takatifu; rehema yake ni takatifu; nguvu zake ni takatifu; ukweli wake ni mtakatifu. Kwa hiyo, kuutambua na kuukumbatia utakatifu wa Mungu kutageuza namna tunavyofikiri, kuishi, na kumwabudu.

Tunapokutana kwa kweli na utakatifu wa Mungu, tunabadilishwa. Zingatia Isaya 6. Isaya ameshindwa kabisa na udhihirisho wa utakatifu wa Mungu. Anamalizika nguvu kabisa, akilia, “Ole wangu! (Isaya 6:5)  Kukutana na utakatifu wa Mungu hutunyenyekeza, hufichua dhambi zetu, na hubadilisha akili na mioyo yetu, na kutulazimisha kupatanisha matakwa yetu na mapenzi yetu na matakwa yake na mapenzi Yake. Nayo shauku na mapenzi ya Mungu kwa ajili yetu ni tuwe watakatifu kwa sababu yeye ni Mtakatifu:“Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.” (Mambo ya walawi 11:44; 1Petro 1:16). Tukitambua uhitaji wetu kwake, tunatengwa kwa ajili ya makusudi yake na kubadilishwa ili tufanana naye.

Kufafanua hili kwa kina kunapita upeo wa tafakari hii fupi, lakini somo ni rahisi: Ukitamani kuwa kama Kristo zaidi, fanya bidii zote kumjua Mungu wako Mtakatifu—Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Soma kitabu cha R.C. Sproul, The Holiness of God, au cha J.I. Packer, Knowing God, au cha Stephen Charnock, The Existence and Attributes of God. Zaidi ya yote, soma Maandiko kwa kuomba kwa shabaha ya kukua katika kumjua Kristo. Kama D.A. Carson alivyonena:

Watu hawasogelei utakatifu kwa bahati tu. Pasipo jitihada zinazoendeshwa na neema, kwa kawaida watu hawataelekea kwenye uchamungu, maombi, utiifu wa Maandiko, imani, na furaha katika Bwana. Tunavutwa na maridhiano ; . . .tunavutwa na kutokutii; . . . tunavutwa na ushirikina.

Kukua katika kumjua Mungu wetu mtakatifu ndani na kupitia Kristo kunazuia kuvutwa huko, kunatuweka katika njia ya utakatifu, na kutuahidi maisha ya furaha na shangwe ya kudumu. Kwa hiyo, wakati mwingine mtu atakapokuuliza, “Unakuwaje kujua kwamba kwa maisha yako yote, kila mtu atakuwa nje akiburudika na kufurahia maisha, wakati wewe umekwama na kanisani?” tabasamu na useme: “Laiti ungemjua Mungu wangu mtakatifu, laiti ungemjua Yesu, usingeuliza hivyo. Kwenda kanisani kumwabudu ni furaha yangu, maana Yeye peke yake aweza kuujaza moyo wangu shangwe na furaha tele!” (Zaburi 16:11; Isaya 35:10; Yohana 16:24).

  1. Louis Berkhof, Summary of Christian Doctrine (Banner of Truth, 2011), 28. ↩
  1. Joel R. Beeke na Paul M. Smalley,Reformed Systematic Theology, Juz. 1 (Crossway, 2004), 569. ↩
  1. D.A. Carson, For the Love of God: A Daily Companion for Discovering the Riches of God’s Word, Juz. 2 (Good News Publishers, 2006), kama ilivyonukuliwa kwenye Goodreads.com. ↩

Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.

Drew DiNardo

Drew DiNardo

Dkt. Drew DiNardo ni mchungaji mkuu wa St. Stephen Reformed Church huko New Holland, Pa.