
Utekelezaji wa Injili katika Nyakati Ngumu
10 November 2026Sababu Tatu za Kuwapeleka Watoto Wako Kanisani
Ingawa watoto wangu wote sasa ni watu wazima, bado nakumbuka vyema changamoto za kuwatayarisha wote watano kwenda kanisani, kisha kuwafikisha kwenye benchi la kanisa kwa wakati uliopangwa, na wakiwa na tabia nzuri. Haikuwa rahisi. Je, ilikuwa yastahili? Bila shaka ilikuwa hivyo. Yesu aliagiza kwamba watoto wadogo waletwe kwake, wala wasizuiliwe (Mathayo 19:14); tena akakasirishwa na wanafunzi waliowazuilia waliotaka kuwaleta watoto wao ili awabariki (Marko 10:14). Watoto wanahitaji kufahamu kuwa wa hapa na kwamba Yesu anatamani sana waje kwake. Kwa hiyo, ili kuimarisha shauku yako ya kukabiliana na changamoto hiyo, ninakupa sababu tatu za kuwapeleka watoto wako kanisani.
1. Ili kuwawezesha kuisikia na kuiona Injili.
Ijapokuwa kila familia ya Kikristo inapaswa kuwamiminia watoto wao Injili tangu utotoni na kila siku baadaye, ni muhimu watoto wako wasikie ujumbe wa Injili kutoka midomoni mwa watu wengine na kuuona ukitenda kazi katika maisha yao. Kutangaza wokovu ulio katika Kristo kunapaswa kuwa kipaumbele kabisa kwa mzazi, kwa maana Yesu alisema, “Kwa maana itamfaidi mtu nini kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?” (Mathayo 16:26). Kanisa la mahali fulani huwasilisha Injili ileile inayohubiriwa na wajumbe wa aina mbalimbali na ikitenda kazi katika mifano hai mbalimbali ya maisha.
Baada ya muda, watoto wanaweza kuanza kutozingatia wazazi wao wanapotumia maneno yale yale na ushawishi ule ule siku baada ya siku. Kanisani, Mungu anaweza kumuinua mshauri, mhubiri, au hata mwenzao awaletee ukweli wa Neno lake—ukweli unaowashawishi moyoni kuhusu dhambi na imani katika Kristo, mambo ya lazima katika wokovu wa roho zao—kwa wakati unaofaa kabisa. Wala hakuna namna ya kuwasilisha Neno la Mungu inayolingana kikamilifu na mahubiri yanayotolewa kwa ustadi, kwa nguvu za Roho Mtakatifu, katika muktadha wa ibada ya pamoja. Nani awezaye kupima ipasavyo athari ya mkusanyiko wa mahubiri 936 mazuri ya Jumapili asubuhi katika kipindi cha miaka kumi na minane juu ya moyo wa mtoto wako? Tena, wanapoona jinsi injili ilivyowageuza wanaume, wanawake, wavulana na wasichana wengine, na wanapoyaona matunda yanayokua katika maisha yao, kanisa hai linakuwa shahidi wa roho zao za thamani na uwezekano wa matokeo ya milele.
2. Kuwapa maono ya ibada ya mbinguni katika ibada ya pamoja.
Ufalme wa Kristo ni mkubwa mno kuliko familia yako. Mungu amekuwa akitenda kazi katika maisha ya mamilioni duniani kote na katika karne zote za historia. Mwishowe, kutakuwa na umati usioweza kuhesabika ukikusanyika kuzunguka kiti cha enzi cha Kristo, kutoka kila kabila, lugha, watu na taifa, ili kumpa utukufu kwa ajili ya wokovu wao (Ufunuo 7:9). Hakuna yeyote kati yetu aliyewahi kuona “kanisa la ulimwengu” (ule muungano wa kiroho wa waamini wote kutoka pande zote za dunia na katika vipindi vyote vya historia ya kanisa) ambalo Ufunuo linaliashiria, lakini tunaweza kupata taswira yake vyema zaidi kwa kuhudhuria ibada katika kanisa la mahali. Huko tunasikia uimbaji wa pamoja kutoka kwa watu wa rika zote na asili mbalimbali, sauti zikiungana katika ibada yenye shauku. Watoto wako watapata nafasi ya kuona kwa macho yao na kusikia kwa masikio yao wenyewe upendo ambao waamini hawa tofautitofauti walionao kwa Yesu.
Zaidi ya hayo, watapewa fursa ya kuhisi ukweli tele wa kiroho uliomo katika sakramenti—Meza ya Bwana na ubatizo. Taratibu hizi za Bwana haziwezi kuzitekeleza peke yao sebuleni nyumbani; nazo hutupatia vionjo vya ibada ya mbinguni. Tajiriba hii, ukizidishwa kwa zaidi ya miaka kumi na minane, itawapa kufahamu kazi yenye nguvu ya Mungu kote duniani na katika karne zote tangu Mwokozi wetu alipotembea duniani. Kwa msingi huu, wanapaswa kuweza kujiweka ndani ya kazi hii kuu ya Roho kwa unyenyekevu, imani, na mtazamo sahihi, mambo ambayo hayawezi kupatikana ndani ya familia yenu pekee, hata kama mmejitoa kwa bidii kiasi gani.
3. Kuwasaidia wajenge mazoea ya kutiifu kwa amri za Mungu.
Mungu amewaamuru Wakristo wasiiache mikusanyiko yao “kama ilivyo desturi ya wengine” (Waebrania 10:25). Ni rahisi kwa familia zenye shughuli nyingi kuingia katika mazoea ya kutohudhuria kanisa. Huenda walisikiliza Jumapili moja kwa matangazo ya moja kwa moja mtandaoni, kisha kupotoka na kuingia kwenye tabia hiyo isiyo na taabu Mungu alionya kwa uwazi dhidi ya kulegea katika kukusanyika kwa ibada ya pamoja, jambo linaloweza hata kuishia kuacha kabisa kuhudhuria kanisani. Hatuwezi kustawi katika kutembea kwetu na Kristo kama Wakristo wanaonda peke yao.
Kwa namna ya pekee kwa wazazi, watoto wetu hututazama kwa makini kila wakati ili kuona kile tunachoamini kweli na kukithamini. Ikiwa hatutaitii amri ya Waebrania 10, watoto wetu watatuona kwa haki kuwa wanafiki, na itakuwa rahisi sana kwao hatimaye kuchagua kutoufanya Ukristo kuwa sehemu ya maisha yao kabisa.. Lakini kwa kuwajengea mazoea ya kuhudhuria kwa uaminifu ibada za kanisani, tutakuwa tunaweka msingi wa maisha yao yote. Wataona kukosa kutii amri hii iliyo wazi kuwa jambo lisilowazika, na hilo litafungua njia ya utiifu kamili kwa yote ambayo Kristo amewaamuru wayatende (Mathayo 28:20).
Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.


