
Nguvu ibadilishayo ya utakatifu wa Mungu katika maisha ya kila siku
29 September 2026Yesu Ndiye Hekalu Jipya
Taswira gani inakujia unapofikiria juu ya hekalu katika Biblia? Huenda ukatafakari hema la kifahari jangwani, lililoungwa kwa mapazia yaliyotariziwa kwa uzuri, na pao za dhahabu zikiunda nafasi takatifu. Au labda unaweza kufikiria jengo kubwa sana lenye makerubi wakilinda mlango wa Patakatifu pa Patakatifu, huku miti ya komamanga ikiwa imechorwa katika kuta zilizopambwa kwa dhahabu. Unaweza hata kufikiria mawe makubwa yaliyochongwa kwa ustadi,yayoenda juu sana ya Yerusalemu kama ajabu ya Herode ya ulimwengu wa kale. Taswira hizi zote ni vielelezo sahihi vya nyakati tofauti zilizorekodiwa katika Biblia. Hata hivyo, kinachoshangaza, ni kwamba Maandiko yanatuambia kwamba tunapolifikiria hekalu, tunapaswa kumfikiria Yesu. Mambo mengine yote ni vivuli vinavyoelekeza Kwake.
Hekalu la kwanza kutajwa katika Maandiko ni bustani ya Edeni. Kama ilivyokuwa baadaye kwa Hema takatifu na hekalu, Mungu aliiumba Edeni iwe mahali Pake patakatifu, maskani ambamo angekaa pamoja na watu Wake. Kabla ya anguko, Edeni ilikusudiwa kuwa patakatifu pake. Kwa sababu hiyo, Mungu alitembea Edeni kama alivyotembea baadaye ndani ya hema (Mwanzo 3:8; Walawi 26:12; Kumbukumbu 23:14; tazama pia 2 Samweli 7:6–7). Edeni na Hema takatifu ya Kukutania ziliingiwa kutoka mashariki (Mwanzo 3:24; Kutoka 26:18–22); Edeni na hekalu la Sulemani vililindwa na makerubi (Mwanzo 3:24; Kutoka 26:31; 1 Wafalme 6:23–29) na ilijaa miti (Mwanzo 2:16; 1 Wafalme 6:20–36). Adamu na makuhani walipaswa “kutumikia na kulinda” patakatifu pao (Mwanzo 2:15; Hesabu 3:8; 8:26; 18:5–6). Edeni lilikuwa hekalu.
Kwa kuwa Adamu alianguka katika dhambi, alifukuzwa kutoka mahali patakatifu. Mungu alipowaokoa watu Wake kutoka Misri, kwa neema akaanzisha tena patakatifu ambapo wenye dhambi wangeweza kumkaribia kwa toba na ibada kupitia utoaji wa dhabihu zinazojirudia (Waebrania 10:1). Mungu akaweka hili “Hema la Kukutania,” yaani hekelu, ili akae pamoja na watu Wake (Kutoka 29:45–46). Lakini hema takatifu lilipokamilika, Israeli walitambua kwamba wingu takatifu la uwepo wa Mungu lilidai utakatifu wa kila anayekaribia. Kwa hiyo, hakuna aliyeweza kuingia— shata Musa (Kutoka 40:35). Mfano mtukufu zaidi wa hekalu lilijengwa na Mfalme Sulemani, na wingu lile lile likalifunika hekalu hilo, likidokeza kwamba hata makuhani hawangeweza kuingia mbele za Yule Mtakatifu (1 Wafalme 8:10–11).
Baada ya Nebukadneza kuharibu Hekalu la Sulemani na kuwapeleka Waisraeli uhamishoni, mfalme wa baadaye wa Uajemi, Koreshi Mkuu, aliwaruhusu Waisraeli kurejea katika nchi yao na kujenga hekalu jipya (Ezra 1; 2 Nyakati 36:22–23). Lakini wazee waliokuwa awali waliliona Hekalu la Sulemani walipoona jengo jipya, walilia kwa huzuni, kwa maana walijua kwamba Hekalu hili la pili halingetimiza yale manabii waliyotabiri (Ezra 3:12). Manabii wa Agano la Kale walitarajiai kwamba mataifa mengi—Wayahudi na Mataifa—wangekuja Yerusalemu na kuabudu katika Hekalu (tazama Isaya 2:1–5). Tena walielewa kwamba Hekalu hilo lingekuwa kuu sana kuliko lile la Sulemani; Hekalu hili jipya lingetikisa mbingu na nchi, Kuwa utukufu na wokovu kwa watu wote (Hagai 2:5–9), ndipo Mungu asemapo, “mimi nipo pamoja nanyi” (Hagai 2:4).
Hekalu ambalo watakatifu wa Agano la Kale walilitamani lilitimia katika Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili. Ni Yesu wa Nazareti ambaye amekuja kukaa, au “kupiga hema,” kati yetu (Yohana 1:14). Yeye ndiye uwepo wa kweli wa Mungu, ambamo utimilifu wote wa Uungu unakaa katika mwili (Wakolosai 2:9–10). Yesu Mwenyewe alisema hivyo alipowaambia Wayahudi, “Libomoeeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitaliinua” (Yohana 2:19). Wakati Wayahudi walidhani kwamba maneno yake yalipaswa kueleweka kwa maana ya moja kwa moja, Yesu alikuwa akinena kiroho juu ya nafsi Yake, hekalu la kweli la Mungu (Yohana 2:20–21). Kweli, kama kuhani, alijitoa Mwenyewe kupitia maisha Yake kamilifu na kifo Chake cha dhabihu, ili watenda dhambi wapate njia ya kuingia, kwa dhabihu Yake, katika uwepo wa hekalu la Mungu Mtakatifu (Waebrania 9:11–14; 10:19–20). Yesu ndiye kuhani, dhabihu, na hekalu, vyote kwa wakati mmoja.
Lakini Agano Jipya pia linaeleza hekalu kwa namna nyingine. Katika 1 Wakorintho 3:16–17, Paulo asema:
“Je, hamjui kwamba ninyi wenyewe ni hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu yeyote akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamwangamiza; kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, na ninyi ndio hilo hekalu.”
Paulo anapoandika kwamba “ninyi ni hekalu la Mungu,” neno “ninyi” si umoja bali wingi, jambo linalomaanisha kwamba Paulo analihutubia taifa la Mungu kwa pamoja kama kanisa. Kwa maneno mengine, kanisa la Yesu Kristo nalo ni hekalu. Kwa kweli, waamini wanafananishwa na sura ya Kristo (Warumi 8:29), maana Roho wake anakaa ndani yetu. Uwepo na nguvu za Mungu zimo kanisani mwake, akiilitia mafuta kwa Roho kwa ajili ya kazi ya kuubariki ulimwengu kwa injili (Mathayo 28:18–20; 2 Wakorintho 4:1–6). Sisi, mwili wa Kristo, tu hekalu ndani yake, kwa kuwa Yeye hutufanya tuwe kama Yeye. Hivyo, kanisa ndilo dhihirisho la wazi la utakatifu wa Mungu tunapomwakilisha Kristo katika dunia hii. Ndani ya Kristo, sisi ni mji juu ya mlima (Mathayo 5:14) na nuru kwa mataifa (Isaya 49:6 pamoja na Matendo 13:47), ili ulimwengu ulione hekalu la kweli kupitia sisi.
Ingawa Maandiko yanaelezea mahekalu yenye mapambo ya kifahari, kuta za dhahabu, na ujenzi wa ajabu, yote hayo yalikuwa vivuli vinavyoashiria mema yaliyokuja (Waebrania 9–10). Hatulitafuti tena hekalu lingine. Tunaye Yeye.
Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.


