Ni ”Uzushi” Gani Mkubwa wa Kiprotestanti kuliko wote?

17 November 2026

Ni ”Uzushi” Gani Mkubwa wa Kiprotestanti kuliko wote?

17 November 2026

Je, Yesu ni Mungu?

Je, Yesu ni Mungu kweli? Hili ni swali muhimu sana la kujibu, na ni swali ambalo limepata majibu mengi tofauti. Kwa hakika Biblia inafundisha kwamba Yesu ni Mungu; Yeye ni Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili. Hebu tuliangalie hili kwa undani zaidi.

Ili kulijibu swali, “Je, Yesu ni Mungu?” tunahitajika kutafakari Mungu ni nani kulingana na Maandiko. Ufafanuzi bora sana unatoka katika Katekisimu Fupi ya Westminster 4: “Swali. Mungu ni nani? Jibu. Mungu ni Roho, asiye na mwisho, wa milele, asiyebadilika, katika asili yake, hekima yake, nguvu zake, utakatifu wake, haki yake, wema wake, na ukweli wake.” Zaidi ya hayo, kuna Mungu mmoja tu. Tunaposema kwamba Yesu ni wa asili ya uungu, hatusemi kwamba Yeye ni Mungu wa pili, bali kwamba Yeye ni Mungu Mwana—nafsi ya pili ya Utatu wa Mungu. Wala hatukanushi ubinadamu wake wa kweli katika kufanyika mwili, kwa maana Yesu Mpatanishi wetu ni Mungu kweli na mwanadamu kweli.

Maandiko yanashuhudia waziwazi uungu wa Yesu. Njia mojawapo tunayoona ukweli huu ni katika vifungu vya Agano Jipya vinavyomwita Yesu “Mungu”. Kwa mfano, mwanafunzi Tomaso alimtambua Yesu katika Yohana 20:28 kuwa “Bwana wangu na Mungu wangu,” na hilo linalingana na theolojia ya Injili ya Yohana. Kwa kweli, mara mbili katika sehemu ya mwanzo ya Injili ya Yohana, Yesu anatambuliwa kuwa “Mungu” (Yohana 1:1, 18; tazama pia 1 Yohana 5:20). Mahali pengine katika Injili, Yesu anazungumza juu ya jina moja la Mungu linalomjumuisha Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu (Mathayo 28:19). Agano Jipya halifundishi mtazamo wa Kimodali(modalism) kumhusu Mungu—yaani, halifundishi kwamba Mungu hujidhihirisha katika hali au namna tatu zinazofuatana. Wala Agano Jipya halifundishi kuchanganyikana kwa nafsi za uungu, bali linafundisha juu ya nafsi tatu za kiungu zilizopo milele: Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu (tazama pia Mathayo 3:16–17).

Barua za Paulo pia zinamzungumzia Yesu kuwa ni Mungu. Yesu ni Mungu juu ya wote (Warumi 9:5), naye ni Mungu wetu na Mwokozi wetu (Tito 2:13). Vivyo hivyo, Petro pia anamzungumzia Yesu kuwa ni Mungu wetu na Mwokozi wetu (2 Pet. 1:1). Andiko jingine muhimu ni Waebrania, ambapo Yesu Mwana anatambuliwa kuwa Mungu ambaye kiti chake cha enzi ni cha milele(Waebrania 1:8). Fundisho hili liko wazi wala halikutengwa  katika mtazamo wa mwandishi mmoja tu au andiko moja tu. Bali Matumizi ya neno “Mungu” kwa Yesu ni thabiti na yanapatikana katika aina mbalimbali za maandiko ya Agano Jipya na kwa waandishi mbalimbali.

Hata hivyo, vifungu vinavyofundisha uungu wa Yesu haviishii tu kwenye maandiko ambamo neno “Mungu” limetumiwa kwa Yesu. Mafundisho ya Agano Jipya kuhusu uungu wa Yesu yameenea zaidi sana. Moja ya njia za kawaida za kuelewa mafundisho ya Biblia kuhusu uungu wa Kristo (na wa Roho Mtakatifu) inapatikana katika Katekisimu Kubwa ya Westminster 11:

Inaonekanaje kwamba Mwana na Roho Mtakatifu ni Mungu, walio sawa na Baba? Jibu. Maandiko yanaonyesha kwamba Mwana na Roho Mtakatifu ni Mungu, walio sawa na Baba, kwa kuwapa majina, sifa, kazi, na ibada ambayo inamstahili Mungu peke yake.

Hapa pana njia nne ambazo kwazo tunajua kwamba Yesu ni wa asili ya Kiungu kulingana na Maandiko: Anapewa (1) majina, (2) sifa, (3) kazi, na (4) ibada; yote yanayostahili kutolewa kwa Mungu pekee. Ikiwa mambo haya yanahusishwa na Yesu katika Maandiko, basi vifungu hivyo vinatulazimu kufikia hitimisho kwamba Yesu ni wa asili ya uungu. Kwa kufafanua hili, tunaweza kuona vipengele hivi vyote vinne vikihusishwa na Yesu katika Waebrania 1.

Majina. Waebrania 1:8 inamtambulisha Yesu kuwa “Mungu” inapoinukuu Zaburi ya 45 inayotumiwa kumhusu Yesu: “Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele” Jina la Mungu linatumika waziwazi kwa Yesu.

Sifa. Waebrania 1:11–12 inatumia Zaburi 102 kwa Yesu,ikisisitiza kwamba Yeye hudumu milele. Hili linaelekeza kwenye umilele wa kiungu wa Yesu: Yeye hudumu milele wala habadiliki kamwe.

Kazi. Waebrania 1:2, 10 inasema kwamba Yesu ndiye wakala wa uumbaji na ndiye aushikiliaye ulimwengu kwa neno la uweza wake (mstari wa 3). Mungu peke yake ndiye Muumba. Ikiwa Yesu ni Muumba, basi lazima awe wa asili ya Kiungu.

Ibada. Biblia iko wazi kwamba Mungu peke yake ndiye anayepaswa kuabudiwa (Mathayo 4:10). Kwa hiyo, ni ishara ya Kiungu kwamba Yesu anaabudiwa na malaika (Waebrania 1:6).

Kwa ujumla, Agano Jipya sio tu kwamba linamtambua Yesu waziwazi kuwa ni “Mungu” kwa kutumia neno hilo, bali pia linamhusisha Yesu na majina, sifa , kazi, na ibada; yote ya kiungu. Tuna msingi imara wa maandiko unaotusaidia kuamini kwamba Yesu ni Mungu.


Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.

Brandon C. Crowe

Brandon C. Crowe

Dr. Brandon D. Crowe is professor of New Testament at Westminster Theological Seminary in Philadelphia and a teaching elder in the Presbyterian Church in America. He is author of several books, including Why Did Jesus Live a Perfect Life? and The Path of Faith: A Biblical Theology of Covenant and Law.