Yesu Ndiye Hekalu Jipya

1 October 2026

Yesu Ndiye Hekalu Jipya

1 October 2026

Theolojia ya Agano kwa Watoto: Mwongozo wa Wanafunzi

Tunapowapeleka watoto wetu shule ya Jumapili au VBS(shule ya Biblia wakati wa Likizo), tunatarajia watapata nini? Tunawezaje kuwasaidia waunganishe wahusika wa Biblia wasio wazi na picha kubwa ya ujumbe wa Biblia? Ni ukweli upi hasa wa msingi ambao umebadilisha kwa kiasi kikubwa maisha ya Wakristo?

Mtaala mpya wa watoto wa Ligonier Ministries, Kukua katika Neno la Mungu, unafungua misingi ya Biblia katika mfululizo wa mwaka mzima, ukiandikwa kwa upekee kutoka katika muundo wa maagano ya Maandiko unaotupa picha kubwa ya mpango wa Mungu wa wokovu na namna anavyoshughulika na wanadamu. Hatuhitaji kungojea hadi watoto wetu wawe wakubwa ili tuwashirikishe katika ukweli wa msingi wa Biblia au kuwafundisha theolojia. Nyenzo hii inalenga kueleza vipengele muhimu vya theolojia ya agano viweze kueleweka kwa urahisi kupitia shughuli na maswali yanayolingana na hatua za ukuaji wa watoto.

Makanisa, wazazi, na walimu wameitwa kwa dhati kutii amri ya Yesu:“Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa mbinguni ni wa wale walio kama hawa” (Mathayo 19:14). Haya ni maudhui machache ambayo tunaweza kuanzia tunapoendelea kutafuta na kwa uaminifu kuifanya Biblia iweze kueleweka na watoto wetu katika kujifunza kwao kwa awali.

1. Muumbaji

Tunapowatambulisha watoto kwa theolojia ya agano, tunaweza kuanza tu na mwanzo. Mungu ndiye Muumbaji. Mungu aliumba kutoka katika visivyokuwapo kwa neno lake Amefunuliwa katika uumbaji Wake, lakini ni katika Neno Lake tu ndipo tunaweza kuelewa maana ya maisha, kifo, dhambi, na nafsi ya Kristo. Martin Luther alisema, “Ikiwa sijui matendo na nguvu za Mungu, simjui Mungu mwenyewe; na ikiwa simjui Mungu, siwezi kumwabudu, kumsifu, kutoa shukrani kwake, wala kumtumikia.”1

Mungu alifanya vitu vyote na kwa ukuu Wake anautunza uumbaji Wake kupitia agano (taz. Warumi 5; 1Wakoritho 15). Agano ni ahadi iliyo na baraka na wajibu.2 Maagano ya Mungu si ya kiholela wala ya kibiashara; bali yanaonyesha ufunuo wa nafsi yake takatifu na kazi zake katika uumbaji wake. Anatenda kulingana na asili Yake ya Utatu, wala si kimakosa kutokana na hisia kali, hali inayofaa, au kwa ubwana. Biblia inafunua maagano matatu ya msingi: agano la ukombozi, agano la matendo, na agano la neema.

2. Kristo

Maandiko yote yanaelekeza kwa Kristo. Kuanzia Mwanzo hadi Ufunuo, Biblia imejaa simulizi mbalimbali, na pamoja zinatunga simulizi kuu kuliko zote zilizowahi kusimuliwa—neema ya Mungu kwa uumbaji wake, ambayo hatimaye imefunuliwa katika kazi ya Kristo Theolojia ya Agano huunganisha Agano la Kale na Agano Jipya ili kumdhihirisha Mungu Mtakatifu katika sheria yake na katika kazi ya Kristo ya mara moja tu (Wagalatia 3:24–29). Badala ya kuisahau sheria, Kristo ametimiza Agano la Matendo kwa maisha yake yaliyokamilika, kifo chake cha dhabihu, na ufufuo wake kutoka kaburini, akiwaongoza wote wanaomfuata kuingia katika Agano la Neema (Mathayo 5:17).

Akiwa Mwanadamu halisi na Mungu halisi, Yesu Kristo ndiye Mpatanishi pekee kati ya Mungu mkamilifu na uanadamu uliovunjika. Ni kwa Baba kumtuma Mwana wake wa pekee; kwa maisha, kifo, na ufufuo wa upatanisho wa Mwana; na kwa nguvu ya kazi ya kuzaliwa upya ya Roho Mtakatifu ndipo tunapokea baraka zote za Agano la Neema. Tukiwa tumeunganishwa na Kristo kwa imani, Wakristo sasa wanaweza kumwita Mungu “Baba” na kujua amani, uhakika, na pumziko kamilifu linalopatikana kwa Mungu huyu wa uhusiano.

3. Kanisa

Agano la neema ni kwa ajili ya jumuiya ya waamini kutoka kila kabila, taifa, na lugha. Hakuna waumini walojitenga, wala hakuna upendeleo Ili kulielewe kanisa, lazima tuielewe theolojia ya Agano na umuhimu wa imani ya kihistoria ambako ibada ya pamoja ndiyo kipaumbele. Injili inaunganisha watu wa agano chini ya bendera moja: Yesu ndiye njia pekee (Yoh. 14:6). Ilikuwa katika Adamu wa kwanza kwamba wanadamu walikufa katika dhambi, na katika Adamu wa mwisho kwamba tunahesabiwa haki kwa imani (1Kor. 15:45). Imani hii hututoa katika utawala wa giza na kutuleta katika nuru ambamo wote wanaoliitia Jina la Kristo hawatatengwa wala kuwa peke yao tena.

Ijapokuwa huu ni ukweli wa papo hapo, bado tunaishi katika ulimwengu uliovunjika hadi Kristo atakaporudi au atakapoituita  nyumbani. Ibada ya Jumapili si suala la shughuli tunazozipendelea mwishoni mwa juma bali ni taswira pana ya yale tuliyoumbiwa: kukua katika kumjua Mungu Muumba wetu na katika pumziko la Utatu Mtakatifu analotualika kulishiriki ndani ya Kristo.

4. Mwito

Watoto wa agano—sawa na wote wanaoisikia injili ikitangazwa—wanapewa upendeleo na baraka ya kipekee: mwito wa mara kwa mara wa kuendelea katika njia ya Bwana. Tunapowafundisha watoto wetu theolojia ya agano, tunawapa  mfumo wa maisha unaojengwa juu ya ukweli wa milele. Lakini ikiwa mafundisho yetu yabaki kwenye kukariri au kurekebisha mwenendo, hatuwaita wakae ndani ya Mzabibu, yaani Bwana Yesu Kristo. Tunataka kuwaita watoto wetu wamwitikie Yesu kwa imani na wakue ndani ya Mzabibu kupitia njia za neema. Mwito huu, ndani ya muktadha wa kanisa la mahali fulani, ndicho kiini cha yale masimulizi mbalimbali ya Biblia: mwito wa imani wa kuamini ahadi za Mungu.

Kuna uharaka katika ujumbe huu ambao tunaweza kuuwasilisha kwa watoto wetu huku tukiwafundisha kwa uvumilivu na kuwaonya, “Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana” (Isaya 55:6). Tunapowafundisha watoto wetu theolojia ya agano, tunawaelekeza kwenye hatima ya safari ambamo wanaweza kujulikana kikamilifu, kuwa salama, na kuongozwa kando ya maji ya utulivu katika maisha haya na yale yajayo.

  1. Martin Luther, Bondage of the Will. ↩
  2. Tazama kitabu kipya na mfululizo wa mafundisho ya J.V. Fesko, Signed, Sealed, Delivered: An Introduction to Covenant Theology, kwa muhtasari wa ngazi ya watu wazima kuhusu theolojia ya agano. ↩

Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.

Meredith Myers

Meredith Myers

Meredith Lee Myers ni mhariri wa wavuti wa Tabletalk na Ligonier Ministries, na mhitimu wa Erskine Theological Seminary, Columbia, SC.