Je, Yesu alikuwa mkamilifu?

1 September 2026

Je, Yesu alikuwa mkamilifu?

1 September 2026

Ninawezaje Kukua katika Hekima?

Maandiko yanatufundisha kwamba tunaishi katika ulimwengu wa mambo yanayopingana—kati yao ni hekima na upumbavu. Haya mawili yanawakilisha njia mbili tofauti zinazounda maisha ya mtu binafsi. Hekima huambatana na njia ya uzima, na upumbavu njia ya mauti.

Hekima mara nyingi hufafanuliwa kama maarifa ya kivitendo au matumizi ya maarifa kwa ustadi. Kama Wakristo, twapaswa kwenda hatua zaidi kwa kumbuka maneno ya Sulemani: “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa” (Mithali 1:7). Kwa mtazamo wa Kibiblia, hekima hutumia maarifa ya Mungu katika maisha; kwa maneno mengine, hekima ni ustadi wa kuishi kwa kumcha Mungu.

Ustadi huo unahitajika katika kila nyanja za maisha. Sharti tuwe na hekima katika maneno yetu, mahusiano, familia, kazi, hisia, ujinsia, uongozi, uraia, mipango, na usimamizi na matumizi ya rasilimali. Hakuna jambo katika ratiba yetu ya kila siku lisilohitaji hekima, kwa kuwa lengo letu ni kuishi kwa ustadi katika yote kwa heshima na utukufu wa Mungu.

Basi, tunawezaje kukua katika hekima? Pengine itasaidia kufikiria jinsi tunavyokua katika ustadi wowote. Tunapotaka kujifunza kufanya jambo vyema, inahitaji jitihada za makusudi, mafundisho, na utekelezaji. Kukua katika ustadi wa hekima si tofauti.

Jitihada za Makusudi

Ustadi wa hekima ni jambo tunaloliomba na pia tunalolitafuta. Hatimaye, hekima ni fadhila tuliyopewa ndani ya Yesu Kristo. Mtume Paulo asema kwamba ndani ya Yesu “zimo hazina zote za hekima na za maarifa” (Kol. 2:3). Bwana wetu anamiliki hiyo hekima kwa ajili ya wateule wake; kama Paulo asemavyo kwingineko, Yeye “amekuwa kwetu hekima itokayo kwa Mungu” (1 Kor. 1:30). Tukiwa tumekubaliwa kuwa watoto katika familia ya Mungu, tumeahidiwa hekima ndani ya Yesu inayotupa ujasiri wa kuomba na uhakika kwamba Mungu wetu mkarimu atatoa (Yak. 1:5). Hata hivyo, utoaji wa hekima haujatenganishwa na namna inavyokuja.

Biblia pia hufundisha kwamba kukua katika hekima huja kwa jitihada ya makusudi. Hekima si sifa ya kuzaliwa nayo, wala haiji yenyewe kwa sababu ya umri. Tena, mfalme mwenye hekima anaelekeza kwamba lazima tuifuate:

Ukiitafuta kama fedha

na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa,

ndipo utakapoelewa kumcha Bwana

na kupata maarifa ya Mungu. (Mit. 2:4–5)

Tunakua katika hekima kwa kuomba na kwa kutafuta: “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata” (Mt. 7:7).

Kufundishwa na Mungu

Kukua katika ujuzi wa kiwango fulani pia kunahitaji mafundisho, na vivyo hivyo ndivyo ilivyo kwenye hekima. Tunajifunza kuhusu hekima kutoka kwenye Neno la Mungu na kutoka ulimwenguni. Biblia yasema,

Kwa kuwa Bwana huwapa watu hekima;

 kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.” (Mit. 2:6)

Mafundisho kutoka katika Maandiko huja kwa namna nyingi, lakini Biblia daima inasisitiza thamani ya wazazi kuwafundisha watoto wao hekima. Hili linaonyeshwa wazi na Sulemani, kwa kuwa sehemu ya kwanza ya Methali inachukua muundo  wa baba anayemfundisha mwanawe. Anasema:

Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba;

sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu.

Ninawapa mafundisho ya maana,

kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu.

Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu, 

ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu

baba alinifundisha akisema,

“Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote.” (Mith. 4:1–4)

Pia tunatiwa moyo na mfano wa Timotheo, ambaye tangu utotoni aliyajua Maandiko Matakatifu, ambayo yaliweza kumkupa hekima hata kupate wokovu (2 Tim. 3:15). Kuna sababu nzuri ya kuamini kwamba alikuwa msikivu wa mafundisho ya mama yake na bibi yake walipokuwa wakimfunza hekima hiyo (tazama 2 Tim. 1:5).

Uumbaji nao ni “kitabu” kinachoweza kutufundisha kuhusu hekima ya Mungu. Hii ni kwa sababu Hekima ilikuwa na nafasi katika uumbaji, hivyo alama ya Hekima iko kila mahali (Mith. 8:22–31). Kwa kukumbuka, maneno ya Aguri karibu na mwisho wa Mithali yanasema,

Vitu vinne duniani ni vidogo;

lakini vina akili nyingi sana.” (Mith. 30:24–28)

Anaendelea kutaja hekima ya chungu, pimbi, nzige, na mjusi. Hata sehemu ndogo na duni za uumbaji hutufunza kanuni za kuishi kwa ustadi na kwa kumcha Mungu.

Kutekeleza Hekima

Hakuna ustadi unaopatikana au kuimarishwa isipokuwa tujitoe kikamilifu kuufanyia kazi. Sulemani alisema,

Mwanangu, usisahau mafundisho yangu,

lakini moyo wako uishike amri zangu. (Mith. 3:1)

Hii ndiyo sababu hekima na upumbavu hulinganishwa na njia—kusudi kuu la njia ni kuikanyaga na kutembea. Tukitaka kukua katika hekima, hatuna budi kuitumia hekima: tusiwe wasikilizaji tu bali pia watendaji wa hekima. Tunapofanya hivyo, huenda tukaendelea taratibu, lakini ukuaji wetu umeahidiwa:

Njia ya wenye haki ni kama nuru ya kwanza ya mapambazuko, 

ambayo hungʼaa zaidi na zaidi hadi mchana mkamilifu.

Lakini njia ya waovu ni kama giza nene; 

hawajui kinachowafanya wajikwae. (Mith. 4:18–19)

Kukua katika hekima si tofauti na kujifunza na kukua katika ustadi wowote. Katika hali ya kawaida kabisa, tunaifuatia kwa juhudi za makusudi, tukiendelea kupokea mafundisho kutoka kwenye Neno na uumbaji, na kuyatekeleza maonyo yake, kuishi kwa utauwa wa ustadi mpaka, kwa neema ya Yesu, tutakapofanywa wakamilifu katika ulimwengu ujao.


Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.

Kyle Borg

Kyle Borg

Rev. Kyle Borg is senior pastor of Winchester Reformed Presbyterian Church in Winchester, Kans. He is author of What Is Love?