Je, Kimsingi Asili ya Mwanadamu Ni Nzuri au ni ya Dhambi Kabisa?

23 June 2026

Je, Kimsingi Asili ya Mwanadamu Ni Nzuri au ni ya Dhambi Kabisa?

23 June 2026

Ghadhabu ya Mungu ni nini?

Ghadhabu ya Mungu ni jibu la Mungu wetu mtakatifu na mwenye haki dhidi ya dhambi na wenye dhambi ambao hawajafunikwa na upatanisho wa Kristo. Ingawa watu wengi hawapendi kumfikiria Mungu kama mwenye ghadhabu, Maandiko mara nyingi yanarejelea utekelezaji wa ghadhabu ya Bwana dhidi ya uovu. Agano la Kale na Jipya yanashuhudia kwa wingi kwamba Mungu hutekeleza ghadhabu juu ya udhalimu (tazama Kumbukumbu la Torati 9:8; 2 Wafalme 23:26; Zaburi 21:9; 90:11; Isaya 13:9; Mika 5:15; Sefania 1:18; Yohana 3:36; Warumi 1:18; Waefeso 5:6; Ufunuo 16:1).

Ghadhabu ya Kimungu na Sifa za Mungu

Mungu anatekeleza ghadhabu Yake juu ya udhalimu kwa sababu ya Yeye alivyo. Maandiko yanashuhudia kwamba Mungu ni mwenye haki na mwenye usawa (Kumbukumbu la Torati 32:4; Danieli 9:14; Warumi 1:17; Warumi 5:3). Asingaliweza kuwa mwenye haki na mwenye usawa ikiwa asingaliadhibu uovu na watenda maovu, hivyo kumimina ghadhabu Yake juu ya dhambi ni sambamba kabisa na sifa Yake ya haki. Wenye dhambi lazima walipie makosa yao, na Mungu hawezi kuwaondolea hatia bila kutekeleza ghadhabu Yake ya haki, la sivyo atakuwa si mwenye haki (Kutoka 34:6–9). Mungu ni upendo (1 Yoh. 4:7–8), na mojawapo ya mambo anayoyapenda ni haki (Zaburi 33:5). Kwa kuwa Mungu ni mkamilifu, upendo Wake juu ya haki lazima uwe mkamilifu; kwa hivyo, lazima achukie “njia ya waovu” (Mithatli 15:9; tazama pia Kumbukumbu la Torati 32:4).

Bwana hawezi kuonyesha ghadhabu isipokuwa pana dhambi, na hakuwezi kuwa na dhambi bila kuwepo kwa viumbe wanaotenda dhambi. Kwa hiyo, ghadhabu ya kiungu haiwezi kudhihirishwa pasipo viumbe na kuanguka kwake katika dhambi. Kwa sababu hiyo, wanatheolojia wengi wameainisha ghadhabu kama sifa ya Mungu iliyo ya uhusiano (relative attribute) na si sifa ya Mungu iliyo ya asili kamili (absolute attribute). Sifa ya kiungu iliyo ya asili kamili ingekuwa dhahiri au kutekelezwa hata kama Bwana hakuwa ameumba chochote. Sifa za Mungu zilizo za asili kamili inajumuisha  mambo kama vile umilele na ujuzi wa yote (omniscience). Iwe Mungu aliwahi kuumba ulimwengu au la, Angekuwa wa milele na mwenye kujua yote.

Sifa za kiungu za kiuhusiano hazionyeshwi isipokuwa kuna kitu nje ya Mungu ambacho Anaweza kuhusiana nacho. Kama ilivyoelezwa hapo juu, ghadhabu ni sifa ya kiungu inayotegemea uhusiano kwa sababu kama kusingekuwa na wenye dhambi, kusingekuwa na udhihirisho wa ghadhabu ya kiungu. Hata hivyo, si kwamba ghadhabu (au sifa nyingine yoyote ya kiungu ya uhusianao) ni kitu ambacho Mungu anakipata kwa sababu ya uumbaji. Mungu anaitikia dhambi kwa ghadhabu kwa sababu ya asili Yake jinsi alivyo—wema na haki. Ghadhabu ya kiungu inadhihirishwa kwa sababu kiumbe amebadilika, kuwa mwenye dhambi, si kwa sababu Mungu Mwenyewe hubadilika. Wenye dhambi wanakutana na ghadhabu wanapokuja mbele ya Mungu ambaye asili yake ni haki , si kwa sababu Bwana anachukua sifa mpya katika anguko hilo. Hata hivyo, Mungu hawezi kubadilika (Malaki 3:6).

Tajiriba ya Ghadhabu ya Mungu

Maandiko yanaweka wazi kwamba ghadhabu ya Mungu ni ya kutisha. Biblia mara nyingi huzungumzia joto kali la ghadhabu ya Mungu (Kutoka 32:11; Maombolezo 4:11), na hata inaelezea mahali pa ghadhabu ya milele ya Mungu juu ya wenye dhambi ambao hawageuki kutoka katika dhambi zao kumwelekea Kristo kama “ziwa la moto” (Ufunuo 20:10). Akichukua kutoka Isaya 66:24, Yesu anasema kwamba jehanamu, “funza wao hafi” (Marko 9:42–49). Kwa picha hii, Mwokozi wetu anaonyesha hukumu ya Mungu kama uharibifu usio na mwisho, unaoangamiza mwenye dhambi. Manabii na Mitume huzungumzia uharibifu mkubwa na maangamizi katika “siku ya Bwana,” ambayo inaweza kumaanisha kumwagwa kwa hukumu ya Mungu katika nyakati maalum za kihistoria pamoja na hukumu yake ya mwisho mwishoni mwa wakati (Isaya 13:6; Ezekieli 30:3; Yoeli 1:15; 2 Petro 3:10).

Kwa sababu ya maelezo yaliyotajwa hapo juu, watu wengi wanaweza kufikiria ghadhabu ya Mungu kuwa inajumuisha tu maonyesho ya kushangaza ya hukumu ya moto. Hata hivyo, ni muhimu, maonyesho kama hayo ya hukumu kwa kweli ni utimilifu wa ghadhabu ambayo ilimwagwa kwanza mapema zaidi. Maandiko kama Warumi 1:18–32 yanaonyesha kwamba Mungu mara nyingi hatekelezi ghadhabu yake yote mara moja bali kwa muda. Ghadhabu yake, Paulo anatuambia, inajumuisha kuwaacha watu katika dhambi zao na kuwaruhusu kuzama zaidi ndani yake. Mungu mara nyingi huwaruhusu wenye dhambi wasiotubu kushiriki katika dhambi wanazotamani kwa muda mrefu kabla ya kuiangamiza katika hukumu ya moto. Mungu katika ghadhabu yake atawakabidhi wasiotubu kwa dhambi zao.

Tumaini kwa Wale Walio Chini ya Ghadhabu ya Mungu

Kuna siku ya mwisho ya ghadhabu inayokuja juu ya wenye dhambi. Kwa bahati nzuri, Mungu pia ni mwenye rehema, na Amemtoa Yesu Kristo ili kutuokoa kutoka kwenye ghadhabu ijayo (1 Wathesalonike 1:10). Yesu Kristo ni Mungu Mwana, ambaye alifanyika mwili ili kubeba adhabu ya Mungu wetu mwenye haki dhidi ya dhambi. Katika Yesu Kristo, Mungu anamimina ghadhabu Yake, akiichukua juu Yake mwenyewe. Kwa hiyo anajionyesha kuwa mwenye haki, kwa kuwa dhambi inaadhibiwa katika Kristo, na pia mwenye rehema tele, kwa kuwa upatanisho wa Kristo unamaanisha kwamba sasa anaweza kuwa mwenye neema, au mwenye fadhili, kwa wenye dhambi wanaogeuka kutoka dhambi zao na kumtumaini Yesu (Warumi 3:21–31). Bwana anafurahia kuonyesha upendo thabiti na rehema (Mika 7:18), na wote wanaomwamini Yesu pekee kwa ajili ya wokovu wataokolewa kabisa kutoka kwenye ghadhabu ya milele ya Mungu (Waebrania 7:25).


Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.


Robert Rothwell

Robert Rothwell

Rev. Robert Rothwell is senior writer for Ligonier Ministries, associate editor of Tabletalk magazine, resident adjunct professor at Reformation Bible College, and associate pastor of Spruce Creek Presbyterian Church in Port Orange, Fla.