
Ibrahimu alikuwa nani?
17 September 2026Kufafanua Changamoto za kuwa Mama kwa Neema
Majira haya ya masika yanaleta mabadiliko makubwa kwangu katika kuwa mama: mwanangu wa mwisho atahitimu kutoka shule ya sekondari. Ni mstari wa kumalizia unaoashiria mwisho wa kipindi hiki cha malezi. Nimeuona ukikaribia kwa muda, nami nimejazwa hisia mseto—furaha kwa ajili ya mwanangu anapoingia kipindi inachofuata cha maisha; huzuni ninapotazamia kutomwona nyumbani kila siku. Nimefika mwisho wa safari tunakoelekea sote, ilhali nimejaa shaka kuhusu kilichoko upande wa pili.
Nilipoanza safari hii, nilihisi kulemewa na yote nisiyoyajua. Nilihisi upungufu mbele ya mambo mengi mapya na yasiyojulikana. Nilipungukiwa na hekima ya kufanya maamuzi magumu ya malezi na niliogopa kukosea. Tangu wakati huo, nimekumbana na hali nyingi ngumu katika kuwa mama, nami natarajia nyingi nyingine. Hata hivyo, nikitazama nyuma, naona neema ya Mungu ikitenda kazi na uaminifu wake ukikutana nami katika taabu zangu zote.
Popote ulipo katika safari yako ya kuwa mama—iwe katika miaka ya mwanzo, ya kati, au wakati watoto wameondoka nyumbani—Mungu atakutana nawe mahali ulipo. Hutoa neema yake. Tunaliona hilo katika maisha ya wakina mama watatu katika Biblia. Katika hali ya kila mmoja wao, Mungu aliwapa walichohitaji na kuwapa neema yake.
Mungu Anaona na Anajua
Katika simulizi ya Hajiri, tunaona mama mtarajiwa ambaye Mungu alimwona katika taabu zake. Kama kijakazi wa Sarai, akawa sehemu ya mpango wa Sarai wa kuleta ahadi za Mungu zitimie (Mwanzo 16). Alipokimbia hasira ya Sarai akafika nyikani, Mungu akakutana naye akamdhihirishia neema yake. Hapo akamwita Mungu El Roi; “Wewe u Mungu unionaye …” “Je! Ni kweli nimemwona yeye anionaye?” (Mwanzo 16:13). Baadaye, alipojikuta tena jangwani na akadhani kwamba yeye pamoja na mwanawe wangekufa, Mungu akamwona. Alisikia kilio chake. Alimkidhia tena mahitaji yake kwa neema Yake: “Usiogope; maana Mungu amesikia” (Mwanzo 21:17).
Tunapopambana kama akina mama, Mungu hukutana nasi pale tulipo na neema yake tele. Yeye ni El Roi, Mungu anayeona. Yeye huona hofu zetu, huzuni zetu, na wasiwasi wetu. Anajua mahangaiko yetu kuhusu watoto wetu. Husikia vilio vyetu vya msaada, naye hutukomboa. Ushahidi mkuu wa hili unaonekana katika ukombozi wa Mungu kutoka katika dhambi zetu msalabani, alipomtoa Mwanawe mwenyewe kulipa adhabu tuliyostahili. Kwa njia ya imani katika kazi ya Kristo kwa ajili yetu, tumekombolewa kutoka katika dhambi, na sasa sisi ni mali ya Mungu: “Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu?” Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja naye?” (Rum. 8:31–32).
Mungu yuleyule aliyemwona Hajiri jangwani anaona na husikia vilio vyetu tunapomwomba msaada.
Mungu hukomboa kwa sababu ya fadhili za agano lake
Katika kitabu cha Ruthu, tunamkuta Naomi, aliyepoteza kila kitu katika nchi ya Moabu. Mumewe alikufa, kisha wanawe wawili wakafuata. Huzuni yake ilikuwa nzito; hakuweza kufikiria kwamba maisha yangeleta furaha tena. Mungu alimkimu kupitia mkaza mwanawe Ruthu, ambaye aliacha watu wake ili ajiunge na Naomi katika safari yake ya kurejea Bethlehemu. Kisha akamkimu tena, katika mashamba ya nafaka, kwa kumpatia Ruthu mume mwenye upendo na kwa Naomi mjukuu. Maudhui inayojirudia katika simulizi yao ni upendo wa huruma ya Mungu. Upendo huo ni zaidi ya wema wa kawaida; ni ahadi ya agano la Mungu kwa watu Wake.
Mungu hukutana na mama walio katika hali za kukata tamaa kwa upendo Wake wa huruma. Kwa akinamama waliopo katika mazingira magumu, kwa sisi tulio katika misimu migumu ya malezi, tunaweza kutumainia upendo usiotetereka wa Mungu kwetu. Upendo ulio mwaminifu. Upendo unaookoa na kukimu. Upendo unaotimiza ahadi. Upendo usiokoma kamwe.
Mungu yule yule aliyemkomboa Naomi katika huzuni yake na kumuonyesha yeye na Ruthu upendo wa huruma ni mwaminifu katika upendo Wake kwetu.
Mungu Hututayarisha kwa Mwiito Wetu
Siku moja, kijana mdogo Mariamu alikutana na malaika Gabrieli, aliyemwambia kwamba angemzaa Mwokozi wa ulimwengu. Nakumbuka vyema upungufu niliohisi kama mama mchanga; siwezi hata kufikiria ilikuwaje kwa Mariamu kusikia habari kama hizo. Wimbo wake unatukumbusha jinsi Mungu anavyotenda kazi katika maisha yetu kwa neema Yake:
Kwa kuwa Yeye aliye mwenye uweza amenitendea mambo makuu,
na jina Lake ni takatifu.
Na rehema Zake ni kwa wale wamchao
kizazi hata kizazi.” (Luka 1:49–50)
Mungu hatuiti kuwa mama kwa sababu tayari tunajua tunachofanya. Hachagui kutukabidhi watoto wa kuwalea kwa sababu sisi tuna uwezo au hekima. Bali, kwa wingi wa neema yake hutuandaa kwa kazi ya kuwa mama: “u wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima na uchaji wa Mungu, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe;” (2Pet 1:3). Anatupa yote tunayohitaji kuwalea watoto wetu. Hutupatia hekima, nguvu, na uvumilivu. Hii ni habari njema kwa akina mama.
Mungu yule yule aliyemmiminia Mariamu neema, anatumiminia hiyo hiyo pia.
Kila mmoja wa akina mama katika Maandiko alikutana na neema ya Mungu maishani mwao, akidhihirisha uaminifu wake. Akina mama, popote mlipo leo, muwe na tumaini kwamba Mungu atakutana nanyi hapo mlipo kwa neema yake.
Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.


