Je, Tunaweza Kuiamini Biblia?

25 August 2026

Je, Tunaweza Kuiamini Biblia?

25 August 2026

Je, Yesu alikuwa mkamilifu?

Hakuna mtu aliye mkamilifu. Ni methali ya kisasa inayoashiria ukweli. Sote twaujua udhaifu wetu na mipaka yetu, nasi tuwepesi kuitumia methali hii kujitetea.

Hata hivyo biblia inatupa mbadala kwa kanuni hii.  Mara nyingine tunasikia hii pia: “Kumewahi kuwa na mtu mmoja tu mkamilifu.” Mtu huyo ni Yesu Kristo.

Ni Kweli kabisa, Yesu ndiye mwanadamu mkamilifu pekee kuwahi kuishi. Lakini Biblia hufundisha hili wapi, na kwa namna gani? Cha kushangaza, baadhi ya maandishi pia yanasema kwamba Yesu alifikia ukamilifu. Hebu tuchunguze ukamilifu wa Yesu Kristo.

Mwana wa Mungu Mwenye Uungu

Kabla hatujazungumzia mahsusi kuhusu maisha ya kibinadamu yaliyokamilifu ya Yesu, tunapaswa kutambua kwamba Yeye ni Nafsi ya milele, ya Uungu. Kwa maneno mengine, Yeye ni Mwana wa Mungu wa milele (Yoh 1:1). Yupo tangu milele katika ukamilifu wote unaotambulisha sifa za Mungu. Yeye ni “asiye na mipaka, wa milele, na asiyebadilika, katika asili yake, hekima yake, uweza wake, utakatifu wake, haki yake, wema wake, na ukweli wake” (Katekisimu Fupi ya Westminster, 4).

Kwa maneno mengine, Yesu ni mkamilifu kwa asili ya yake ya kuwa mwana wa Kimungu. Yeye hana dhambi hata kidogo.

Ubinadamu Kamili wa Yesu

Tofauti na asili yake ya kuwa mwana wa Kiungu, tunapozungumza kuhusu maisha kamilifu ya Yesu, tunamzungumzia kwa kadiri ya ubinadamu Wake katika kufanyika mwili—yaani, ukamilifu wa asili Yake ya kibinadamu. Jambo hili linaweza kuangaliwa kwa mitazamo mbalimbali.

Kwanza, Yesu hakujumuishwa katika dhambi ya Adamu. Hili ndilo linalonuiwa na andiko kama Warumi 5:12–21. “Wote wamefanya dhambi” katika Adamu (Rum. 5:12), lakini Yesu analeta hoja mbadala. Dhambi moja ilisababisha hukumu kwa wote walio katika Adamu, ilhali tendo moja la haki linaleta kuhesabiwa haki kwa wote walio katika Kristo (Rum. 5:18–19).

Iwapo wanadamu wote walitenda dhambi katika Adamu, na ilhali Kristo analeta haki na uzima, basi Yesu hakuwa miongoni mwa “wote” waliotenda dhambi katika Adamu. Haki anayotuhesabia hutokana na nafasi yake ya kipekee kama kichwa cha agano na kama mwakilishi mwenye haki kikamilifu. Hili linaafikiana na ujumbe wa malaika Gabrieli kwa Maria kwamba mtoto atakayemzaa atakuwa mtakatifu, Mwana wa Mungu (Luka 1:35).

Yote haya yanamaanisha kwamba Yesu hakuwa na asili iliyoanguka yenye kulemea katika dhambi. Yesu ana asili ya kibinadamu isiyoanguka, isiyo na dhambi. Yeye ni mwenye haki kikamilifu.

Pili, Yesu aliishi maisha ya kibinadamu makamilifu ya utiifu. Hili nalo linapaswa kumrejelea Adamu. Kutokutii kwa Adamu kulileta hukumu, lakini Agano Jipya linamdhihirisha Yesu kuwa Adamu wa pili na wa mwisho, mwakilishi ambaye utii wake unabatilisha maasi ya Adamu wa kwanza.

Pamoja na Rum 5:12–21, simulizi la majaribu katika Marko linamwoyesha Yesu kuwa Adamu mpya—mwakilishi anayetii hata katika majaribu. Huenda hii ndiyo sababu wanyama wa mwituni wametajwa, ikiibua taswira ya bustani ya Edeni (Marko 1:12–13).

Vivyo hivyo, baada ya Yesu kubatizwa (Luka 3:21–22), Luka anajumuisha ukoo wa Yesu akiufatilia hadi kwa Adamu (Luka 3:23–38). Baada ya hapo, Yesu anatii jangwani (Luka 4:1–13). Hili tena linaunganisha utiifu wa Yesu na utambulisho wake kama Adamu mpya.

Paulo naye anashughulikia hili katika 1Kor 15. Yesu ndiye Adamu wa mwisho ambaye kupitia kwake huja ufufuo wa wafu (1Kor 15:21–22,45). Ufufuo wa Yesu ulikuwa uthibitisho wa kifo chake kisicho cha haki. Kwa kuwa hakuwa na dhambi, kuuawa kwake kama mhalifu kulikuwa udhalimu; na kufufuka kwake kunadhihirisha utiifu wake mkamilifu (taz. 1Tim 3:16). Ufufuo wake unaonyesha utiifu wa maisha yake yote (taz. Ebr 2:14–18).

Tatu, Waebrania inapotaja kwamba Yesu “alifanywa mkamilifu” (Ebr 2:10; 5:9; 7:28), hili lazima lieleweke katika muktadha wa historia ya wokovu,wala si kuhusu asili yake ya kiungu. Hakuna dhambi ndani ya Yesu kama Mwana wa Mungu wa milele, Zaidi ya hilo, hakuwahi kamwe kutenda dhambi katika maisha yake duniani. Kwa hiyo, “kufanywa mkamilifu” kunarejelea kufaulu kwa huduma yake kama Kuhani wa mwisho na mkamilifu, anayetupa ukaribu mkubwa zaidi na Mungu kuliko makuhani wa awali (taz. Ebr 5:7–10; 6:19–20; 9:11–14; 10:5–14).

Yesu aliweza kuwasilisha dhabihu ya mwisho kwa sababu Yeye ni Mwana wa Mungu wa milele, aishiye milele kwa kadiri ya nguvu ya uzima usioweza kuangamizwa (Ebr. 7:15–28). Kufufuka kwa Yesu na njia ya kumfikia Mungu anayoitoa kunathibitisha ukamilifu wa dhabihu Yake ya kujitoa Mwenyewe, na hivyo pia ukamilifu wa maisha Yake hapa duniani.

Hitimisho

Kwa kuwa hakuna yeyote kati yetu aliye mkamilifu, ni Habari Njema kweli kwamba Yesu ndiye mkamilifu. Yesu ni Adamu wa pili na wa mwisho, ambaye utiifu Wake mkamilifu ndio msingi wa kuhesabiwa kwetu haki tunayonufaika nayo kwa imani. Uzima wa milele unapatikana ndani Yake (Yoh. 1:4; 20:31). Yeye si mwanadamu wa kawaida tu; Yeye ni Mwana wa Mungu wa milele. Hata hivyo Yeye ni mwanadamu wa kweli—Mungu-mwanadamu aliyefanya kwa ajili yetu yale tusiyoweza kujifanyia sisi wenyewe.

Kama Kuhani mkamilifu, Yesu ndiye Mpatanishi wa pekee anayetoa kufika kuliko kamili kwa Mungu (Ebr. 10:14). Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri ili tupokee rehema na tupate neema ya kutusaidia wakati wa uhitaji (Ebr. 4:14–16).


Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.

Brandon C. Crowe

Brandon C. Crowe

Dr. Brandon D. Crowe is professor of New Testament at Westminster Theological Seminary in Philadelphia and a teaching elder in the Presbyterian Church in America. He is author of several books, including Why Did Jesus Live a Perfect Life? and The Path of Faith: A Biblical Theology of Covenant and Law.