Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kuhusu Theolojia ya Agano
4 September 2025
Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kuhusu Kufanya Maamuzi Kibiblia
9 September 2025
Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kuhusu Theolojia ya Agano
4 September 2025
Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kuhusu Kufanya Maamuzi Kibiblia
9 September 2025

Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kuhusu Jehanamu

Kwa sababu mada ya jehanamu ni ngumu kutafakari, wengi ndani na nje ya kanisa wamejaribu kulifanya jepesi wazo hilo, kwani Mungu mwenye upendo anawezaje kuwapeleka watu mahali pabaya kiasi hicho? Lakini Mungu hajatutaka tumtoe kwenye lawama kuhusu jehanamu, wala haruhusu kupunguzwa kwa ukali wa ukweli huo. Mengi ya yale tunayojifunza kuhusu jehanamu, kwa kweli, yanatoka kwa Yesu Mwenyewe mwenye upendo, ambaye mafundisho yake kuhusu jehanamu yanaendeleza mafundisho ya Agano la Kale. Haya ni mambo matano muhimu ya kujua kuhusu jehanamu.

1. Jehanamu ni mahali halisi pa mateso yanayofahamika, yasiyo na mwisho.

Fundisho la kimakosa lijulikanalo kama maangamizi ya milele, au hali ya kutokufa kwa masharti, linaeleza kwamba waovu huangamizwa kabisa katika hukumu ya mwisho. Hawahitaji kuwa na wasiwasi kuhusu adhabu ya milele inayofahamika baada ya maisha haya. Kinyume na mtazamo huu, Biblia inaonyesha jehanamu kuwa ni mahali pa mateso yanayofahamika na ya kudumu. Mateso ya jehanamu hayana mwisho (Yuda 13; Ufunuo 20:10). Katika Luka 16, kwa mfano, tajiri anaelezewa kama “akiwa katika mateso” (Luka 16:23) huko kuzimu na akiwa na ufahamu wa hali yake ya kusikitisha, bila shaka akipendelea kupoteza uwepo wake kuliko kuendelea katika mateso.

Pia hakuna msingi wa kibiblia kwa “nafasi ya pili.” Hali ya makazi ya wakazi wa jehanamu inadumu milele. Kifo kina ashiria wakati wa kubadilisha anwani ya kudumu. Kwa hiyo, mawazo kwamba roho zilizoko jehanamu hatimaye zitaharibiwa (maangamizi) au kwamba zitapewa nafasi ya pili hayana kibali cha maandiko.

2. Jehanamu ni mojawapo ya sehemu mbili pekee ya kuwa hatima ya kila mwanadamu.

Wakati mtu anapokufa, mwili wake unazikwa na roho yake inapelekwa mara moja mbele ya Mungu, ambapo ataingizwa mbinguni au kutupwa jehanamu. Maungamo ya Imani ya Westminster 32.1 inaelezea hivi:

Miili ya watu, baada ya kifo, hurudi mavumbini, na kuona uharibifu: lakini roho zao, ambazo hazifi wala hazilali, zikiwa na uwepo wa milele, hurudi mara moja kwa Mungu aliyewapa: roho za wenye haki, zikiwa zimekamilishwa katika utakatifu, hupokelewa katika mbingu za juu zaidi, ambako hutazama uso wa Mungu, katika nuru na utukufu, zikisubiri ukombozi kamili wa miili yao. Na roho za waovu hutupwa jehanamu, ambako hukaa katika mateso na giza totoro, wakihifadhiwa kwa hukumu ya siku kuu. Mbali na sehemu hizi mbili, kwa roho zilizotenganishwa na miili yao, Maandiko hayatambui mahali pengine.

Katika siku ya mwisho, kila roho itaunganishwa tena na mwili wake. Wakati huo, wenye haki wataingia katika uzima wa milele, wakati waovu watatupwa katika “mateso ya milele” (Maungamo ya imani ya Westminster, WCF 33.2). Tena, mbali na sehemu hizi mbili, kwa roho zilizoungana tena na miili yao katika ufufuo, Maandiko hayakubaliani na sehemu nyingine yoyote.

3. Jehanamu ni mahali pa uwepo wa ghadhabu ya Mungu.

“Adhabu za milele” za jehanamu zinaelezewa na maungamo ya Westminster 33.2 kama mahali pa adhabu “pamoja na uharibifu wa milele mbali na uwepo wa Bwana, na utukufu wa nguvu zake.” Mara nyingi, jehanamu hufikiriwa kama mahali pa kutengwa na uwepo wa Mungu. Lakini Mungu yupo kila mahali—Hawezi kukosa kuwa mahali fulani. Badala yake, Maandiko yanaona jehanamu kama hali si ya kutokuwepo Kwake bali ya uwepo Wake wa ghadhabu, kutoridhika Kwake kusikoisha na adhabu. Mungu wetu, ambaye ni “moto ulao” (Waebrania 12:29), atamimina “ghadhabu na hasira” Yake (Warumi 2:8) juu ya waovu katika jehanamu.

Ikiwa hii inasikika vibaya kwa Mkristo, ni kwa sababu ni upande wa Mungu ambao hauwiani na uzoefu wetu wa Mungu kama watoto Wake wapendwa. Kile ambacho waovu watakipata jehanamu ni ghadhabu ya Mungu ambayo ilizimwa kwa ajili ya watu Wake na Kristo, lakini uhalisia wa jehanamu kwa wale waliokataliwa ni wa kusikitisha zaidi kuliko hata maelezo ya mfano wake, kama vile ishara yoyote inavyoweza tu kuwakilisha na kuashiria uhalisia kwa njia isiyo kamilifu. Pengine maelezo ya Biblia kuhusu jehanamu kwa njia ya ishara yanatokana na ukweli kwamba adhabu isiyo na mwisho kutoka kwa Mungu mtakatifu ni mateso yasiyoweza kuelezeka.

4. Wakaazi wa jehanamu ni wale ambao wamechagua kuwa huko.

Jehanamu ni hatima ya wale ambao wamechagua kupenda giza badala ya nuru (Yohana 3:18–21). Hili linaweza kuonekana kupingana na kilio cha hamu cha tajiri, “Baba Ibrahimu, nihurumie, na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu” (Luka 16:24). Lakini angalia kwamba yule tajiri hakuwa na tamaa ya kumtaka Mungu ghafla; bali anachotamani ni kupata nafuu kutoka kwa adhabu ya Mungu.

Wakalvinisti wanaweza na wanapaswa kuthibitisha kwa urahisi kwamba kila mtu anapokea mwishowe kile alichochagua kwa hiari—ama kumwabudu Mungu kwa kufanywa upya na Roho Mtakatifu au kumlaani Mungu. Wale ambao wako jehanamu hawawezi na hawatadai kutotendewa haki, kwa kuwa wamepewa kile wanachostahili na kile walichochagua. Biblia haioni kuwa kuna mkanganyiko kati ya jehanamu kuwa adhabu ambayo Mungu anawapa waovu na jehanamu kuwa mahali ambapo wanadamu walichagua kwa hiari. Jehanamu, basi, ni hatima ya “kukabidhiwa” tamaa zetu wenyewe na tamaa za mwili (Warumi 1:24).

5. Jehanamu huenda sambamba na asili ya Mungu.

Jehanamu si doa jeusi kwenye rekodi ya Mungu. Si jambo la aibu kwenye wasifu Wake ambalo haliambatani na uhalisia wake. Hapana, jehanamu huenda sambamba na haki takatifu ya Mungu inayodai adhabu ya dhambi iwe sawia na kiwango cha hatia ya mtu. Haki ya Mungu na wema Wake si sifa zinazopingana. Zote zina kubaliana kabisa, na mbingu na kuzimu ni maonyesho ya hayo maelewano mtakatifu. Kama Mungu hakuwa wa haki, maangamizi ya milele, imani ya wokovu ya wote, au mitazamo mingine yoyote isiyo ya kibiblia kuhusu maisha baada ya kifo yangekuwa yanawezekana.

Fikiria wema na haki ya Mungu katika kazi ya Mwana Wake. Je, kazi ya Kristo haingekuwa bure kama kusingekuwa na jehanamu? Ikiwa waovu wangeangamizwa au kwa namna fulani kuingizwa mbinguni, je, dhabihu ya Kristo isingekuwa haina maana? Hakika, kukataa kuwepo kwa jehanamu si tu kwamba hakulingani na tabia ya Mungu, bali ni sawa na kumkanyaga Mwana wa Mungu chini ya miguu (Waebrania 10:29). Tabia ya Mungu—haki Yake na wema Wake—inadai utekelezaji wa adhabu kamili kwa dhambi juu ya waovu milele.

Ingawa mengi zaidi yanaweza kusemwa kuhusu jehanamu, labda tutafanya vyema kukumbuka kwamba maelezo mengi ya Biblia kuhusu jehanamu yanalenga kukuza neema ya Kristo ambaye ametuokoa kutoka humo, na kuchochea bidii ndani yetu kuwaonya wengine wakimbie maumivu ya jehanamu kwa kumgeukia Kristo kwa imani ya kweli na toba.


Makala haya yalichapishwa kwanza katika Blogu ya Huduma za Ligonier.

Aaron L. Garriott
Aaron L. Garriott
Mchungaji Aaron L. Garriott ni mhariri mkuu wa jarida la Tabletalk, profesa msaidizi mkazi katika Chuo cha Biblia cha Reformation huko Sanford, Florida, na alihitimu kutoka Wheaton College na Reformed Theological Seminary huko Orlando, Florida. Yeye ni mzee anayefundisha aliyewekwa wakfu katika Kanisa la Presbyterian nchini Marekani.