Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kuhusu Jehanamu
6 September 2025
Mambo Matatu Unayopaswa Kujua Kuhusu Wakolosai
11 September 2025
Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kuhusu Jehanamu
6 September 2025
Mambo Matatu Unayopaswa Kujua Kuhusu Wakolosai
11 September 2025

Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kuhusu Kufanya Maamuzi Kibiblia

Maamuzi, maamuzi, maamuzi. Sote tunafanya maamuzi mengi katika siku moja tu. Kwa kweli, baadhi yanaonekana kuwa ya kawaida (kahawa ya kawaida au bila kafeini?), wakati mwengine hakika yana athari kubwa zaidi katika maisha (Nitahudhuria chuo gani? Je, nikubali fursa hii ya kazi? Je, nimchague nani awe mwenzi wangu wa ndoa?). Katika haya yote, waumini wanahitaji msaada na mwongozo wa Mungu. Ingawa si orodha kamili, haya ni  mambo matano ambayo kila Mkristo anapaswa kuzingatia katika kufanya maamuzi sahihi kibiblia.

1. Maamuzi ya kibiblia yamejekita kwenye Biblia.

Kwa kusema waziwazi, Biblia si tu sauti moja kati ya nyingi zilizo sawa ambazo tunaweza kuchagua. Ni chanzo pekee cha hekima isiyokosea, ushauri, mwongozo, na maelekezo ya kweli. Biblia si kitabu cha taarifa tu, bali ni sauti hasa ya Mungu wetu, sawa na kama vile angelikuwa anasema nasi kwa pumzi Yake mwenyewe (2 Timotheo 3:16). Au, kwa maneno mengine, Biblia si ya kutoa taarifa tu; ni ya uhusiano. Huyu ni Baba yetu wa mbinguni mwenye upendo akitupa mwongozo wake katika kufanya maamuzi yetu. Kwa hivyo, uamuzi wowote ambao ni ukiukaji wa wazi wa Maandiko si kuikataa Biblia tu; bali ni kumkataa Baba yetu. Na, bila shaka, kutakuwa na athari.

2. Maamuzi ya kibiblia yanafanywa kwa maombi.

Uamuzi wa kibiblia ni wa kimahusiano. Mungu husikia, hujali, na hujibu. Hatufanyi utafiti tu kutoka kwa kitabu cha mwongozo kisichokuwa na utu; tunatafuta mwongozo kutoka kwa mwongozaji Mwenyewe. Tunao uhusiano na Mwandishi. Ni hekima Yake; ni ushauri Wake; na umeandikwa kwa ajili ya watoto Wake, ambao Yesu alikufa kwa ajili yao na ambao amewafanya kuwa wana na kuwapenda. Anafurahia kutupa msaada wakati tunapomwomba.

Ni nani kati yenu, ikiwa mwanawe atamwomba mkate, atampa jiwe? Au kama akiomba samaki, atampa nyoka? Ikiwa basi ninyi, mlio waovu, mnajua jinsi ya kuwapa watoto wenu zawadi nzuri, je, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wanaomwomba! (Mathayo 7:9–11)

3. Maamuzi ya kibiblia ni ya kushauriana.

Biblia mara nyingi inapendekeza kufanya maamuzi ya busara kwa kushauriana na hekima ya wengine. “Fanya mipango kwa kutafuta mashauri” (Mithali 20:18). “bali hekima hupatikana kwa wale wanaozingatia ushauri” (Mithali 13:10). Bila shaka, “wengine” lazima wawe Wakristo wacha Mungu, waliokomaa, wenye ujuzi wa Kibiblia ambao wanatufahamu vizuri. Kuna faida kubwa katika kushauriana na wale ambao wanaweza kuthibitisha uamuzi wetu au kutuonya kuhusu hatari zinazoweza kutokea, changamoto, au maeneo mengine ambayo huenda hatujazingatia. Hii mara nyingi huvunjwa wakati wale tunaoshauriana nao ni wachanga zaidi au hata marafiki wasio Wakristo, ambao mara nyingi watasema kile tunachotaka kusikia. Kwa hivyo, tunafuata sharti la “kujua Biblia” kwa kuwa “mashauri ya waovu ni ya udanganyifu” (Mithali 12:5).

4. Maamuzi ya kibiblia yanategemea mpango wa Mungu wa kipekee.

Uamuzi wa kibiblia unazingatia kile ambacho Mungu anafanya katika utawala wake mkuu kama Mungu ambaye “anahifadhi na kuwaongoza viumbe wake wote, na matendo yao yote” (Westminster Shorter Catechism 11). Hii hakika siyo sababu pekee ya kuamua mapenzi ya Mungu katika kufanya maamuzi. Hata hivyo, Mungu anaweza kutupa fursa kwa kujibu maombi yetu au uongozi wake unaweza kutuelekeza katika njia ambayo hatukuwa tumeifikiria hapo awali. Watu wa Mungu wanaweza kumtumaini Yeye kutuongoza kwa njia ya kimungu tunapomtazama kwa imani kwa ajili ya mwongozo.

5. Maamuzi ya kibiblia ni mchanganyiko wa kanuni zilizotolewa na Mungu na kuidhinishwa na Biblia (na nyingine) kuchukuliwa pamoja.

Moja ya njia ambazo Wakristo wenye nia njema hufanya maamuzi yasiyo ya kibiblia ni kwa kutumia kipengele kimoja cha mchakato na kuacha vingine vyote. Masuluhisho ya aina mbili yanayotumiwa mara kwa mara kama “chanzo kimoja” ambacho watu huuamini kimakosa kwa ajili ya kutafuta mapenzi ya Mungu ni (1) kufikiri kwamba sisi ni wafasiri wasio na makosa wa utaratibu wa Mungu (“Niliona ishara hii” au “Nilikuwa na ndoto hii”) na (2) hisia zetu (“Ninajisikia tu kwamba hili ndilo Mungu anataka nifanye”). Wakati moja ya haya yanapochukuliwa kwa kupuuza kanuni nyingine zote, uamuzi unaofanywa utakuwa hauna usawa. Mungu ametupa Neno lake lote litumike pamoja na ahadi yake ya kutusaidia katika kufanya maamuzi.

Amani na ujasiri tulionao katika kufanya maamuzi ni kwamba Mungu anatupenda na daima atatimiza kusudi lake kuu katika kila uamuzi tunaofanya. Na hata kama “tukikosea”—ingawa kunaweza kuwa na athari hasi ambazo tunawajibika kikamilifu kwazo—Mungu bado ataangalia maisha yetu, pamoja na dhambi na makosa yetu yote, kwa ajili ya mema yetu na utukufu Wake. Amani na faraja tulio nayo inayotulinda dhidi ya upepo mkali wa hofu ni kwamba Yeye bado ni Mungu ambaye, kwa mapenzi yake ya enzi kuu, husababisha mambo yote kufanya kazi pamoja kwa ajili ya mema kwa wale wampendao Mungu na walioitwa kulingana na kusudi lake (Warumi 8:28).


Makala haya yalichapishwa kwanza katika Blogu ya Huduma za Ligonier.

David Boxerman
David Boxerman
Mchungaji David Boxerman ni mchungaji mstaafu wa Kanisa la Lakeside Presbyterian, Southlake, Texas, ambako alihudumu kama mchungaji mkuu kwa miaka ishirini na miwili.