
Je, Ungamo la Dhambi ni Nini?
26 May 2026
Kupata Tumaini Katikati ya Ugonjwa Mbaya
2 June 2026Je, Mungu Kweli Anajali?
Katika kina cha kukata tamaa au katika hali ya juu ya wasiwasi, waumini mara nyingi hujiuliza—hata kama kwa kimoyomoyo tu—iwapo Mungu kweli anawajali. Ikiwa ni wewe, nina habari njema.
Swali la Kawaida
Kwanza, huko peke yako. Katika historia yote Waumini wamekuwa wakijiuliza swali hili. Nabii Habakuki aliiangalia hali ya watu wa Mungu—waliokandamizwa na kuonewa na wasio haki—na akalia,
Ee Bwana, hata lini nitakuomba msaada,
lakini wewe husikizi (Habakuki 1:2; tazama pia 1:3, 13).
Watunga zaburi mara nyingi walimsihi Mungu “ajitokeze,” wakiwa na shaka kuhusu utunzaji Wake wakati maumivu yalionekana kutopata majibu (Zaburi 35:23; 44:23). Ingawa walijua kwamba Mungu halali kamwe (Zaburi 121:4), fikira zao kwamba hatendi lolote wakiwa katikati ya mateso kuliwatia shaka ikiwa kweli anajali.
Mapambano haya hayakujikita katika Agano la Kale pekee. Katika wakati wa kukata tamaa, wanafunzi walimlilia Yesu, “Mwalimu, je, hujali kwamba tunaangamia?” (Marko 4:38, msisitizo umeongezwa). Hata katika mambo ya kawaida, waumini wanakabiliana na swali hili. Martha, akiwa amelemewa na kazi yake, aliuliza ikiwa Yesu alijali kwamba aliachwa kuhudumu peke yake (Luka 10:40). Katika nyakati na hali mbalimbali, wakati Mungu haingilii kati katika mateso yetu haraka kama tunavyotarajia (au kutozuia mateso hayo tangu mwanzo), waumini wa zama zote wametilia shaka kuhusu Kujali Kwake.
Jibu la Kipekee
Pili, Mungu hakuachi peke yako kujiuliza ikiwa anakujali. Amedhihirisha kukujali kwake kwa namna ya ajabu na kustaajabisha mno: kumtuma Mwana wake wa pekee. Yohana anatueleza hivyo anapoandika: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwana wake pekee” (Yohana 3:16). Hii inamaanisha kwamba Kristo anaelewa kikamilifu kuchanganyikiwa, maumivu, na hofu inayotokana na kuishi katika dunia inayougua dhambi na anaweza kuchukuliana nawe (Waebrania 4:15).
Zaidi ya hayo, kujali kwa Mungu kunadhihirishwa kupitia kazi za Roho Mtakatifu. Yesu alipoahidi Roho, alimuelezea kama “Msaidizi mwingine” ambaye hatatuacha kamwe (Yohana 14:16). Tofauti na marafiki wa kibinadamu, ambao wanaweza kuchoka au kuchanganyikiwa, Roho Mtakatifu anabaki nawe daima. Hapumziki, hajifichi, na hakuachi. Huu ni utekelezaji wa ahadi ya msingi wa agano la Mungu kwako: “Sitakuacha wala sitakupungukia” (Kumbukumbu 31:8; Waebrania 13:5). Hii ni kweli hata wakati hisia zako zinapokuambia kwamba uko peke yako, umetelekezwa, na nje ya uangalizi wa Mungu.
Mateso Yanaelekeza kwenye Kujali kwa Mungu
Hatimaye, lazima utambue kwamba kujali kwa Mungu hakumaanishi kwamba utaepuka mateso na kuvunjika moyo. Badala yake, kujali kwake kunamaanisha kwamba utayavumilia na hata kukua kupitia hayo. Hii inaweza kuonekana kinyume cha mantiki. Hata hivyo, Mungu anatueleza kwamba mateso, mbali na kutuangamiza, yanazalisha uvumilivu, tabia, na tumaini (Warumi 5:3–5).
Baadhi ya mateso huja kama nidhamu ya upendo kutoka kwa Baba yetu, iliyokusudiwa kwa ajili ya mema yetu (Waebrania 12:7–11), ambayo ina maana kwamba mateso yetu—hata yanapokuwa ya kinidhamu—si ishara ya kuachwa na Mungu bali ni ishara ya kujali Kwake.
Mateso mengine huturuhusu kushiriki katika maisha ya Kristo. Paulo anatangaza kwa ujasiri kwamba sisi ni “warithi pamoja na Kristo, ikiwa tunateseka pamoja naye ili tupate kutukuzwa pamoja naye” (Warumi 8:17). Hata Kristo Mwenyewe alijifunza utiifu kupitia mateso (Waebrania 5:8). Ikiwani tuwe kama Yeye, lazima tujifunze kwa mkono huo huo. Mbali na kuwa mzigo, hii ni zawadi—heshima ya kushiriki katika tajiriba ya Mwokozi wetu.
Hitimisho
Wakati unapojaribiwa kutilia shaka kama Mungu anajali, angalia msalaba. Hapo, upendo wa Mungu umeonyeshwa kikamilifu. Asingeweza—kwa kweli, asingeliweza—kuacha watu Wake baada ya kulipa gharama kubwa sana. Na asingeweza kulipa gharama kubwa kama hiyo kama asingelikuwa anawajali sana watu Wake—asingalikuwa anakujali wewe-tangu mwanzo. Mateso yako sio lazima iwe ishara kwamba Mungu ameondoa kibali Chake; badala yake, inaweza kuwa ushahidi wa kazi Yake inayoendelea ndani yako.
Jipe moyo. Wakati unapokuwa na shaka na imani yako inapokuwa dhaifu, Yeye hatakuacha. Siku moja, utakapotazama nyuma baada ya jaribu hili ukiwa mahali pa amani, utaona kwamba haikuwa nguvu ya kushikilia kwako msalaba iliyokudumisha, bali ilikuwa nguvu ya mikono Yake yenye makovu ya misumari iliyokubeba, iliyokulinda, iliyokutia nguvu, na ambayo haijakuacha wala kukusahau kamwe.
Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.


