Hamasa kwa ajili ya Upendo

21 July 2026

Je, Biblia Inasema Nini Kuhusu Wachungaji Wanawake?

6 August 2026

Hamasa kwa ajili ya Upendo

21 July 2026

Je, Biblia Inasema Nini Kuhusu Wachungaji Wanawake?

6 August 2026

Je, Kanisa Limejaa Wanafiki?

Karibu miaka thelathini iliyopita, rafiki yangu wa karibu na mfanyikazi mwenzangu, Archie Parrish, ambaye wakati huo aliongoza mpango wa Evangelism Explosion (EE) huko Fort Lauderdale, alikuja kwangu akiwa na ombi. Alionyesha kwamba katika maelfu ya ziara za kiinjilisti ambazo timu za EE zilizifanya, walihifadhi rekodi ya majibu ambayo watu walitoa katika mijadala ya injili. Walikusanya maswali na pingamizi ambazo watu walikuwa wakizitoa mara nyingi kuhusu imani ya Kikristo, na kuyaweka pamoja maswali na pingamizi hizi katika makundi kumi waliyokutana nayo mara nyingi zaidi. Daktari Parrish aliniomba ikiwa ningeandika kitabu cha kujibu pingamizi hizo kwa ajili ya wainjilisti kukitumia katika kazi yao ya kufikia watu. Matokeo ya juhudi hiyo ni kitabu changu Objections Answered, ambacho sasa kinaitwa Reason to Believe. Miongoni mwa pingamizi kumi za juu zilizotolewa ilikuwa pingamizi kwamba kanisa limejaa wanafiki. Wakati huo, Daktari D. James Kennedy alijibu pingamizi hili kwa kusema, “Kweli, kuna nafasi kwa ajili ya mmoja zaidi.” Aliwaonya watu kwamba ikiwa wangepata kanisa lililo kamilifu, hawapaswi kujiunga nalo, kwani hilo lingeliharibu.

Neno mnafiki lilitoka katika ulimwengu wa maigizo ya Kigiriki. Lilitumika kuelezea barakoa ambazo wachezaji walitumia kuigiza majukumu fulani. Hata leo, ukumbi wa michezo unaashiriwa na barakoa pacha za vichekesho na msiba. Katika enzi za kale, wachezaji fulani walicheza zaidi ya nafasi moja, na walionyesha jukumu lao kwa kushikilia barakoa mbele ya uso wao. Hiyo ndiyo asili ya dhana ya unafiki.

Lakini shtaka kwamba kanisa limejaa wanafiki ni uongo ulio wazi. Ingawa hakuna Mkristo anayefikia kipimo kamili cha utakaso katika maisha haya, kwamba sote tunapambana na dhambi inayoendelea haihalalishi hukumu ya unafiki. Mnafiki ni mtu ambaye hufanya mambo yale anayodai hafanyi. Wanaolitazama kansa la Kikristo kutoka nje wanaona watu wanaosema kuwa wao ni Wakristo na wanawaona wakitenda dhambi. Kwa kuwa wanaona dhambi katika maisha ya Wakristo, wanakimbilia kuhukumu kwamba kwa hivyo watu hawa ni wanafiki. Ikiwa mtu anadai kuwa hana dhambi na kisha anaonyesha dhambi, hakika mtu huyo ni mnafiki. Lakini kwa Mkristo kuonyesha tu kwamba yeye ni mwenye dhambi hakumfanyi awe na hatia ya unafiki.

Mantiki iliyogeuzwa inakwenda hivi: Wanafiki wote ni wenye dhambi. Yohana ni mwenye dhambi; kwa hiyo, Yohana ni mnafiki. Yeyote anayejua sheria za mantiki anajua kwamba hitimisho hili la kimantiki hii si sahihi. Ikiwa tungebadilisha tu shtaka kutoka “kanisa limejaa wanafiki” hadi “kanisa limejaa wenye dhambi,” tungelikuwa wepesi kukiri kuwa na hatia. Kanisa ni taasisi pekee ninayoijua inayomhitaji mtu kukiri kuwa yeye ni mwenye dhambi ili kuweza kuwa mshirika. Kanisa limejaa wenye dhambi kwa sababu kanisa ni mahali ambapo wenye dhambi wanaozikiri dhambi zao huja kutafuta ukombozi kutoka kwa dhambi zao. Kwa hivyo kwa maana hii, kwa sababu tu kanisa limejaa wenye dhambi haihalalishi hitimisho kwamba kanisa limejaa wanafiki. Tena, unafiki wote ni dhambi, lakini si dhambi zote ni dhambi ya unafiki.

Tunapoangalia tatizo la unafiki katika enzi ya Agano Jipya, tunaliona likionyeshwa waziwazi katika maisha ya wale waliodai kuwa wao ni wenye haki zaidi. Mafarisayo walikuwa kundi la watu ambao kwa ufafanuzi walijiona kama wametengwa na dhambi za kawaida za umati. Walianza vizuri, wakitafuta maisha ya utauwa na utiifu wa sheria ya Mungu. Hata hivyo, tabia yao iliposhindwa kufikia viwango vyao, walianza kujihusisha na unafiki. Walijifanya kuwa wenye haki zaidi kuliko walivyokuwa. Walitoa sura ya nje ya haki, ambayo ilitumika tu kuficha upotovu mkubwa katika maisha yao.

Ingawa kanisa halijajaa wanafiki, hakuna namna ya kukana kwamba unafiki ni dhambi ambayo haijazuiliwa au kuwekewa mipaka kwa Mafarisayo wa Agano Jipya tu. Ni dhambi ambayo Wakristo lazima wakabiliane nayo. Kiwango cha juu cha tabia ya kiroho na haki kimewekewa kanisa. Mara nyingi tunaona aibu kwa kushindwa kwetu kufikia malengo haya ya juu, na tunaelekea kujifanya kana kwamba tumefikia kiwango cha juu zaidi cha haki kuliko tulivyokifikia kiuhalisia. Tunapofanya hivyo, huwa tunavaa barakoa ya mnafiki na kujiweka chini ya hukumu ya Mungu kwa ajili ya dhambi hiyo mahsusi. Tunapojikuta tumejifunga katika aina hii ya kujifanya, kengele ya tahadhari inapaswa kulia akilini mwetu kwamba tunahitaji kurudi haraka kwenye msalaba na kwa Kristo na kuelewa mahali ambapo haki yetu ya kweli inapatikana. Tunapaswa kuitafuta ndani ya Kristo, si barakoa inayoficha nyuso zetu, bali kabati zima la mavazi, ambayo ni haki Yake. Hakika, ni chini ya kivuli cha haki ya Kristo, iliyopokelewa kwa imani, ambapo yeyote kati yetu anaweza kuwa na tumaini la kusimama mbele ya Mungu mtakatifu. Kuvaa mavazi ya Kristo kwa imani si kitendo cha unafiki. Ni kitendo cha ukombozi.


Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.

Ken Jones

Ken Jones

Rev. Ken Jones is pastor of Glendale Missionary Baptist Church in Miami. He is contributor to several books, including Experiencing the Truth: Bringing the Reformation to the African-American Church. Rev. Jones is cohost of the podcast Saints and Sinners Unplugged.