
Faraja ya Mungu Katika Kumpoteza Mtoto
11 June 2026
Mambo Matatu Unayopaswa Kujua Kuhusu Waebrania
18 June 2026Mambo Matatu Unayopaswa Kujua Kuhusu Yoeli
Kile ambacho watu wengi wanakijua kuhusu kitabu cha Yoeli ni unabii mkuu katika Yoeli 2:28–29, ambapo Mungu anaahidi kumimina Roho Wake juu ya wote wenye mwili ili kwamba jamii yote ya watu wa Mungu wapate kutabiri. Lakini maana ya mistari hiyo haiwezi kueleweka pasipo na ujumbe wa kitabu hicho. Kuna mambo matatu unayopaswa kujua kuhusu kitabu cha Yoeli ambayo yatakusaidia kuelewa ujumbe wake.
1. Tarehe ya kitabu cha Yoeli haijulikani.
Kwanza, muktadha wa kihistoria wa vitabu vingi vya kinabii ni muhimu kwa ujumbe wa kitabu hicho, lakini tarehe ya kitabu cha Yoeli haijulikani. Hekalu linafanya kazi, ambavyo ina maana kwamba linaweza kuwa hekalu la kabla ya uhamisho la Sulemani (lililoharibiwa mwaka 586 KK) au hekalu lililowekwa wakfu baada ya kurudi kutoka uhamishoni (516 KK). Hakuna mfalme anayetajwa, na wala hakuna adui mkuu wa Israeli au Yuda anayetajwa. Wasomi wamependekeza tarehe mbalimbali, lakini hakuna tarehe hata moja iliyokubalika. Kitabu kinaonekana kuakisi mtazamo wa kabla ya uhamisho ambao unahusiana na matukio yanayozunguka uharibifu wa hekalu la kwanza, kama vile dhabihu kukatizwa (Yoeli 1:9), tishio kutoka kwa jeshi la kaskazini (Yoeli 2:20), na ukombozi wa baadaye ulioelezewa (Yoeli 2:23–29). Wengine wanafikiri ni vigumu kukipa tarehe kitabu hiki kwa sababu kiligeuka kuwa maandiko ya liturujia yanayorudiwa wakati wa janga la kitaifa.
2. Tukio la kitabu ni janga la nzige.
Jambo la pili unalopaswa kujua kuhusu kitabu cha Yoeli ni kwamba tukio la kitabu hiki lina uhusiano na ujumbe wa kitabu chenyewe. Tukio la kitabu ni janga la nzige. Sura ya 1 ni mwito wa maombolezo ya pamoja kwa sababu ya janga la nzige ambalo lilikuwa la uharibifu sana kiasi kwamba hakuna jambo kama hilo liliwahi kutokea. Janga hilo limeelezewa katika Yoeli 1:4, ambapo makundi ya nzige yameharibu kila kitu kinachoweza kulika. Makundi tofauti yanaitwa ili kuomboleza kwa sababu ya matokeo: Walevi wanapaswa kuomboleza kwa sababu mizabibu imeharibiwa (Yoeli 1:5–7), makuhani wanapaswa kuomboleza kwa sababu dhabihu zimesitishwa (Yoeli 1:8–10), na wakulima wanapaswa kuomboleza kwa sababu hakutakuwa na mavuno (Yoeli 1:11–12). Makuhani pia wanaitwa kuwaongoza watu wa Mungu katika ibada ya maombolezo inayojumuisha kulia na kufunga (Yoeli 1:13–14).
Machafuko ya janga la nzige yanakuwa maelezo ya siku ya Bwana. Itakuwa siku ya hukumu kwa wale wanaomkataa Mungu na siku ya baraka kwa wale wanaomrudia Mungu. Janga la nzige linaanzisha hukumu inayokuja ya siku hiyo, iliyotajwa kwanza katika Yoeli 1:15:
Ole kwa siku hiyo!
Kwa maana siku ya BWANA iko karibu.
Uharibifu wa siku hiyo umeelezwa katika Yoeli 1:16–20 na mwito wa dharura wa tahadhari katika Yoeli 2:1–2, ambao unakamilika kwa kusisitiza tabia ya “siku” hiyo kama “siku ya giza na huzuni” na “siku ya mawingu na giza nene!” Giza hili linatanda juu ya milima, likionyesha jeshi kubwa na lenye nguvu lililojipanga kwa vita na mashujaa ambao hawawezi kuzuiwa. Watu wanauchungu kwa wazo la kukabiliana na jeshi hili, kwa kuwa ni zaidi ya jeshi la kidunia; ni jeshi la Bwana. Bwana anatoa sauti yake mbele ya jeshi hili na uumbaji wenyewe unatetemeka na jua na mwezi vinatiwa giza (Yoeli 2:10–11). Hakuna anayeweza kustahimili kwa sababu “siku ya BWANA ni kuu na ya kutisha sana” (Yoeli 2:11).
Katika Yoeli, siku ya Bwana ni zaidi ya tukio moja la kihistoria tu; inaelezea tukio la kieskatolojia (matukio ya siku za mwisho) linaloleta mwisho wa historia. Yoeli anatumia uharibifu ujao wa hukumu ya Mungu katika siku ya Bwana kuwaita watu wa Mungu kutubu (Yoeli 2:15–17). Anawaahidi baraka za kimwili katika kubadilisha uharibifu wa janga la nzige (Yoeli 2:21–27) na baraka za kiroho ambazo zingekuja na kumiminwa kwa Roho Mtakatifu wake (Yoeli 2:28–32).
Mtume Petro ananukuu Yoeli kuelezea matukio katika siku ya Pentekoste.
Jambo la tatu unalopaswa kujua kuhusu kitabu hiki ni kwamba Petro ananukuu kutoka kwa Yoeli 2:28–32 katika Matendo 2:17–21 ili kuelezea matukio ya siku ya Pentekoste. Baraka za kiroho ambazo Yoeli alikuwa amezitabiri zilikuwa zinatimia wakati Mungu alipomimina Roho Wake juu ya watu wote ili kila mtu anayeliitia jina la Bwana angeokolewe.
Zaidi ya hayo, kazi ya kinabii ya kunena neno la Mungu ilipanuka kujumuisha tabaka zote za jamii, pamoja na watu wa mataifa, ambao walikuwa wakizungumza kwa kuelewana kwa lugha zao wenyewe kama Roho alivyowapa uwezo wa kusema (Matendo 2:4). Badala ya hukumu ya mwisho dhidi ya maadui wa Mungu kutokea wakati huo (Yoeli 3:1–8), pamoja na urejesho kamili wa watu wa Mungu (Yoeli 3:17–21), makusudi ya Mungu ya wokovu yalikuwa yakitekelezwa kupitia kutangazwa kwa habari njema za Yesu Kristo kwa ulimwengu wote. Matokeo yake ni, tumepata ndani ya Yesu Kristo malipo ya awali ya wokovu wetu. Tunangojea ukamilifu wa wokovu wetu wakati Mwokozi wetu atakaporudi duniani kukamilisha siku ya Bwana katika hukumu ya mwisho ya maadui wa Mungu na urejesho kamili wa watu Wake. Wakati huo, tutahisi katika umilele wote uwepo Wake kamili na baraka za kiroho na kimwili zinazoambatana pamoja na uwepo Wake.
Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.


