
Kumkumbuka R.C. Sproul, 1937-2017
Na Stephen Nichols, December 14, 2017
R.C. Sproul, mwanatheolojia, mchungaji, na mwanzilishi wa Ligonier Ministries, alifariki tarehe 14 Disemba mwaka wa 2017, akiwa na miaka 78, baada ya kulazwa hospital kutokana na matatizo ya pafu. Dkt. Amemuacha mpenzi wake wa utotoni na mkewe wa miaka hamsini na saba, Vesta Ann (Vooorhis); binti yake, Sherrie Sproul Dorotiak, na mumewe, Dennis; na mwanawe wa kiume, Dkt. R.C. Sproul Jr., na mkewe, Lisa. Sproul na mkewe wana wajukuu kumi na mmoja, mjukuu mmoja wa kike ambaye ni marehemu, na vitukuu saba.
R.C. Sproul alikuwa mwanatheolojia aliyelitumikia kanisa. Alipendezwa na Wanamageuzi si tu kwa maudhui ya ujumbe wao, bali pia kwa jinsi walivyousambaza ujumbe kwa watu. Walikuwa ni “Wanatheolojia katika uwanja wa vita” kama alivyowaita. Wengi walisikia juu ya zile sola tano za Wanamageuzi kwanza kupitia kwa mafundisho ya R.C. Sproul. Wakati R.C. Sproul alipofundisha juu ya Martin Luther, ni kana kwamba alikuwa amekutana na Mwanamageuzi wa karne ya kumi na sita. Kujitolea kwa R.C. kwa maandiko pekee kulimpelekea yeye kuwa na sehemu katika kuandika na kutetea Kauli ya Chicago juu ya Biblia kutokuwa na makosa (1978). Pia alihudumu kama rais wa Baraza la Kimataifa la Biblia isiyo makosa (1978). Kwa sababu ya kujitolea kwake kwa imani pekee, kuhesabiwa haki kwa imani pekee, R.C. alichukua msimamo jasiri wa upinzani dhidi ya Evangelicals and Catholics Together [Wainjilisti na Wakatoliki Pamoja] (ECT) mwaka wa 1994. Baadaye alipinga Mtazamo mpya kumuhusu Paulo na mtazamo wa Shirikisho la Maono (Federal Vision view). Kama wale Wanamageuzi, R.C. alikuwa tayari kuchukua msimamo jasiri kwa kiini na maandiko muhimu ya kihistoria ya ukristo wa orthodoksi. Alikuwa mtetezi wa mamlaka ya Neno la Mungu na injili.
R.C. aliyesomea uanafalsafa na theolojia, alikuwa mtetezi mkuu wa wale waliokuwa katika taaluma ya utetezi wa dini ya kiasili. Alijulikana kwa kuwa na msimamao wa nguvu kuhusu maisha kabla ya kuzaliwa, na wakati mmoja alisema kuwa kutoa mimba ni swala muhimu la kimaadili katika wakati wetu. Alikuwa, zaidi ya yote, mwanatheolojia. Aliyapenda mafundisho ya Mungu. Kupitia kwayo, alipata njia ya kumjua Mungu, kumpenda Mungu, na kumwabudu Mungu. Mafundisho ya Mungu huenda yakawa ndiyo kitovu cha gurudumu la kazi na urithi wa R.C. Sproul, unaoonekana katika maandishi, The Holiness of God (1985). Kama baba na babu katika imani, alisaidia kizazi kizima kukutana na Mungu wa Biblia.
Mtoto wa kiume wa Pittsburgh, Robert Charles Sproul alizaliwa tarehe 13 Febuari 1939, mtoto wa Robert Cecil Sproul na Mayre Anne (Yardis) Sproul. Usiku wa kuamkia Krismasi ya 1942, babake R.C., aliyekuwa na kampuni ya uhasibu mjini Pittsburgh, aliwasili Casablanca, Morocco, kuanza huduma yake katika jeshi katika Vita vya Dunia vya Pili. R.C. alichapa barua yake ya kwanza akiwa amepakatwa na mama yake, akibofya x’s na o’s, “Kisses and hugs,” chini ya barua kwa babake. Kutoka shule ya msingi hadi shule ya upili, R.C. alitumia muda wake mwingi katika uwanja wa riadha kuliko katika mashine ya kupiga chapa. Alipata ufadhili wa masomo ya riadha katika Westminster College, kaskazini mwa Pittsburgh. R.C. alienda chuoni akiwa hajaokoka, lakini katika mwaka wake wa kwanza alimpokea Kristo.
Kufikia wakati R.C. alipotoka chuoni, hakuwa ameokoka tu, pia alikuwa amepata “wokovu wa pili” katika mafundisho ya Mungu. Baadaye angeandika juu ya tajiriba hii katika kurasa za kwanza za The Holiness of God. Mnamo tareha 11, 1960, R.C. alimuoa Vesta, mpenzi wake wa utotoni. Alikuwa ndiyo amefuzu kutoka chuoni na R.C. alikuwa bado ana mwaka mmoja amalize. Alimpenda mara ya kwanza tu alipomuona, alipokuwa katika gredi ya pili na yeye akiwa gredi ya kwanza. Karibia kila wakati, imekuwa R.C. na Vesta.
Baada ya chuo, R.C. alienda Pittsburgh Thological Seminary, alikokuwa chini ya ushauri wa John Gerstner. Wakati mmoja R.C. alisema,” Ningalikuwa nimepotea bila Gerstner.” Kabla ya kufuzu kutoka seminari, R.C. alikuwa mchungaji kwanza katika kanisa la Presbyterian huko Lyndora, Pennsylvania, lililokuwa la wafanyikazi wa mikono, wakimbizi wa Hungari, ambao karibu wote walikuwa wafanyikazi wa Armco Steel Works. Baada ya seminari, alifanya mafunzo ya uzamili chini ya G.C. Berkouwer katika Free University huko Amsterdam. Alijifundisha Kidachi kwa kusikiliza mihadhara na kusoma vitabu vya kiada. Mwaka wa 2016, binti yake Sherrie, alimpatia nakala ya kitabu cha hadithi, Perry Mason, kwa Kidachi, alifurahi kuirudia tena lugha hiyo.
R.C. alirudi Marekani baada ya mwaka huko Netherlands. Tarehe 18 Julai, 1985, alifanywa kasisi katika Pleasant Hills United Presbyterian Church huko United States of America (UPCUSA). Baadaye angehamisha ujuzi wake wa huduma kwa Presbyterian Church huko Marekani (PCA). Baadaye alichukua kazi tatu za kufundisha kwa kifupi huko Westminster College (1965-66), Gordon College (1966-68) na Conwell Theological Seminary, iliyokuwa wakati huo katika chuo kikuu cha Philadelphia, Temple University. Halafu, R.C. alikuwa mchungaji wa College Hill Presbyterian Church huko Cincinnati, Ohio kwa miaka miwili.
Mwaka wa 1971, R. C. alianzisha Ligonier Valley Study Center, huko Stahlstown katika milima ya magharibi ya Pennsylvania. Huduma hiyo ilihamishwa hadi Orlando mwaka wa 1984, ambako imehudumia watu wa kitaifa na kimataifa kupitia uchapishaji, utangazaji, na ufundishaji. Ikiwa bado katika Ligonier Valley, huduma hii ilitoa toleo lao la kwanza la Tabletalk mwaka wa 1977. Gazeti hili la kila siku la tafakari la Neno la Mungu husambaza nakala 100,00, likiwa na wasomaji zaidi ya 250,000. Ligonier ilianzisha kipindi cha redio, the R.C. Sproul Study Hour mwaka wa 1982, halafu ikaanza kupeperusha hewani kipindi cha kila siku Renewing Your Mind mwaka wa 1994, ambacho kimefikia mamilioni.
Kutoka mwaka wa 1971 hadi 2017, R.C. Sproul alikuwa katika uongozi wakati ambapo Ligonier ilikuwa mwenyeji wa makongamano ya kitaifa ya kila mwaka nchini kote, makongamano ya kimataifa, na ziara za mafundisho; walitoa mfululizo wa mafundisho, vitabu, na vifaa vingine; nakuanzisha tovuti, blogu, RefNet, na Ligonier app. Katika kila juma moja, huduma hii hufikia watu zaidi ya milioni mbili ulimwenguni. Kama mpango wa kujiendeleza, baraza la Ligonier Ministries lilitangaza Ligonier Teaching Fellows, ambao sasa wanajumuisha Dkt. Sinclair B. Ferguson, Dkt. W. Robert Godfrey, Dkt. Stephen J. Nichols, Dkt. Burk Parsons, na Dkt. Derek W.H. Thomas. Chris Larson anahudumu kama rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Ligonier Ministries.
Katika jukwaa lake kama mwananchi kiongozi, R.C. alihudumu katika Baraza la kimataifa la Biblical Inerrancy, Evangelism Explosion, Prison Fellowship, na Serve International. [yaani, Kutokosea kwa Maandiko ya Biblia, Mlupuko wa Uinjilisti, Ushirika wa Magereza, na Serve International]. Mwaka wa 1980, R.C. alikubali kazi kama profesa wa theolojia na utetezi wa dini katika Reformed Theological Seminary (RTS). Yeye na Vesta walisafiri hadi Jackson, Mississippi, kwa miezi michache kila mwaka na alifundisha masomo kamili katika muda mfupi. Mwaka 1987, baada ya kuwa akiishi katika Florida ya Kati, RTS ilifungua chuo cha Orlando. R.C. alihudumu kama yule John Dyer Trimble Sr. Mwenyekiti wa Systematic Theology kuanzia mwaka 1987-1995. Baadaye alihudumu kama Profesa mtajika wa Systematic Theology na Utetezi wa dini katika Knox Theological Seminary, Fort Lauderdale, Florida, kutoka 1995-2004.
R.C. alirudi kwenye uchungaji. Kama alivyokumbuka, “Mwaka wa 1997, Mungu alifanya jambo ambalo sikulitarajia kamwe.” Jambo hilo lilikuwa ni kuanzishwa kwa Saint Andrew’s Chapel huko Sanford, Florida. Wakati wa kifo chake, R. C. alikuwa mchungaji mwenza na Burk Parson wa Saint Andrew’s. Alihubiri mahubiri yake ya mwisho tarehe 26, Novemba, 2017, juu ya Waibrenia 2:1-4, “Wokovu Mkuu mno.”
Wakati wa kifo chake, R.C. alikuwa Kansela wa chuo alichoanzisha mwaka wa 2011, Reformation Bible College. R.C. alihudumu kama rais wa kwanza, na kukipa chuo hicho jina, mtaala wake, na misheni yake ya kuelimisha wanafunzi katika kumjua Mungu na utakatifu wake katika utamaduni wa zamani wa Mageuzi. Kutoka katika dirisha la afisi yake katika jumba la utawala la Ligonier, R.C. angeangalia kulia na kuona chuo hicho na kuangalia kushoto na kuona kanisa.
R.C. alichapisha kitabu chake cha kwanza mwaka wa 1973: The Symbol: Maelezo juu ya Imani ya Mitume. Akikidhamini kwa afuataye: “Kwa Vesta: Kwa Warumi, mungu wa kike wa kipagani; kwangu, mke mcha Mungu.” Kitabu chake cha kwanza kinaashiria kazi yake inayowadia kama mwanatheolojia, na udhamini wa kitabu chake cha kwanza kunaonyesha mtindo wake wa asili. Kufikia kifo chake, alisifika kwa zaidi ya vitabu mia moja. Hivi vilijumuisha vitabu vya watoto, riwaya, juzuu tatu za tahariri juu ya Westminster Confession of Faith, tahariri juu ya vitabu kadhaa vya kibiblia, na juu ya mada yoyote ya mafundisho ya dini na maisha ya Kikristo. Yeye na wengine waliandika Classical Apologetics mwaka wa 1984 na kuandika Chosen by God mwaka wa 1986. Mwaka wa 1985 alitoa Holiness of God, moja kati ya maandishi muhimu katika karne ya ishirini. R.C. alihudumu kama mhariri mkuu wa Reformation Study bible. Aliandika zaidi ya dazeni mbili za nyimbo za dini. Ushirikiano wake na rafiki yake na mtunzi mwenza Jeff Lippencott ulitoa CD mbili, Glory to the Holy One (2015) na Saints of Zion (2017).
Uandishi wa nyimbo wa R.C ulikuwa uendelezi wa asili wa mapenzi yake ya muziki. Pamoja na Vesta, aliimba katika kwaya ya vijana huko Pleasant Hills United Presbyterian Church na kwaya shuleni. R.C. pia aliimba bezi katika bendi ya waimbaji wanne. Alikuwa mpigaji kinanda, baadaye katika maisha yake alicheza pia fidla, akijifunza katika chuo kipya cha Saint Andrew’s Conservatory of Music. R.C. pia alichora. Alikuwa mchezaji golfu mwenye bidii na mweledi. Alifurahia uwindaji, mafumbo, kusoma, hasa kusoma vitabu vya wasifu.
Mwalimu mkamilifu, R. C. Sproul alipenda na aliishi ili kufundisha maandiko kwa walei. Alikuwa mcheshi, mwenye vichekesho vingi. Mazungumzo na R.C. yalizunguka kwa urahisi kutoka kujihusisha na theolojia hadi kwa michezo na golfu (zaidi ya mchezo) na vichekesho. Alitamani kuona akili zikifanywa upya, mioyo ikigeuzwa, na maisha yakibadilishwa na injili. Alikuwa na kipawa cha ajabu cha kufanya mambo yawe wazi. Hakuwatisha wasikilizaji wake kwa msamiati wa kiufundi ama kuwatawala. Alifundisha maswala ya kina, maswala ya maudhui na mazito, kwa uwazi na dharura ya ajabu. Aliwafundisha wanafunzi wake wa funzo la mahubiri kutafuta mvuto wa kipekee uliopo katika maandishi na halafu kuhubiri mvuto huo.
Mara nyingi R.C. alikumbuka kukutana kwake kwa mara ya kwanza na Mungu wa Biblia. Kama Mkristo mpya na mwanafunzi wa mwaka wa kwanza chuoni, aliisoma Biblia kwa hamu. Jambo moja lilijitokeza katika usomaji wake: Mungu ni Mungu anayejishughulisha vilivyo. Zaburi, simulizi ya Uzia, Mwazo 15:17, wimbo wa utukufu wa Mariam, Luka 16:16-17, na bila shaka Isaiya 6—mvuto katika maandishi haya ulimteka R.C. muda alipoyasoma. R.C. alitufundisha hili: “Mungu ni mtakatifu, na sisi si watakatifu.” Katikati ni Mungu-mtu Yesu Kristo na kazi yake kamilifu ya utiifu na kifo chake cha upatanisho msalabani. Huo ndio uliokua ujumbe na urithi wa R.C. Sproul (1939-2017).