
Kutafuta Usafi Wetu na wa Kanisa
25 November 2026Kuenenda kwa Hekima mbele ya Walio nje katika Ulimwengu wa Kidijitali
Wewe na mimi tunakabiliwa na maamuzi mengi kila siku. Wakati mwingine maamuzi hayo huwa magumu. Katika nyakati hizo, unageukia wapi ili kupata hekima? Labda unamgeukia baba yako au babu yako. Pengine ni mchungaji wa familia yenu, ambaye ametumika kwa uaminifu wiki baada ya wiki kwa miongo mingi. Na bila shaka, Kitabu cha Mithali. Lakini nadhani mahali pamoja ambapo Wakristo wengi wenye kufikiri kwa makini wasingeshauri mtu akimbilie ni mitandao ya kijamii. Ingawa ukweli na hekima vinaweza kupatikana humo, ni kwa kiwango kidogo na mara nyingi huzamishwa na kelele nyingi pinzani na maoni ya harakaharaka.
Licha ya ukweli huu, mitandao ya kijamii ndiyo sehemu ambayo tunazidi kutumia muda wetu mwingi, na tafiti zinaendelea kuonyesha kwamba vijana wanatumia masaa mengi kila siku kwenye mitandao ya kijamii na karibu muda wote wako mtandaoni. Hili linaibua maswali kuhusu jinsi Wakristo wanavyoweza kustawi katika kizazi hiki kipya cha kidijitali, hasa vijana Wakristo ambao hata hawajui kwamba ni kitu “kipya,” kwa kuwa hiki ndicho tu ambacho wamekijua. Wakristo wanahitaji kuwa na mtazamo wa kuchukua hatua za makusudi mapema ikiwa tunataka kupinga mwelekeo wa utamaduni wa leo na kukataa kuruhusu dunia itufanye kuwa wafuasi wake.
Aya moja inayonijia mara nyingi akilini tunapozungumzia changamoto za kizazi cha leo cha kidijitali inapatikana katika Wakolosai. Mtume Paulo anawaambia wasomaji wake, “Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati” (Wakolosai 4:5). Ingawa imekuwa kweli daima kwamba tangu anguko sisi sote tunahitaji hekima, hasa mbele ya watu walio nje, hitaji hilo ni kubwa zaidi leo, ambapo chapisho moja tu kwenye mitandao ya kijamii linaweza kuonekana na mamilioni, kama si mabilioni, ya watu walio nje— idadi kubwa ambayo huenda hata Paulo hangeweza kuifikiria?
Kwa Paulo, msukumo wa kufuata hekima mbele ya watu walio nje ulikuwa ni “matumizi mema ya wakati”—yaani, kutumia kila nafasi vizuri kwa ajili ya uinjilisti, tukiwa na maneno “yaliyokolea munyu” na tukijua jinsi ya “kumjibu kila mtu” (aya ya 6). Kama Mtume Petro katika 1 Petro 3:15, Paulo anachukulia kuwa mwenendo wa maisha ya Mkristo,mwendo wake wa hekima, utachochea maswali kutoka kwa ulimwengu unaomtazama. Lakini je, jinsi Wakristo wanavyoshiriki katika mazungumzo kwenye mitandao ya kijamii, hata pengine namna tunavyotumia vifaa vyetu vinavyotuunganisha daima, kunatofautiana vipi na ulimwengu unaotuzunguka? Inaonekana wazi kutokana na Maandiko kwamba kunapaswa kuwe na tofauti, lakini kwa huzuni, mara nyingi tunakosa hekima ambayo tumeamriwa kuitafuta na kuitumia katika maisha ya Kikristo.
Tofauti moja kati ya Mkristo na mtu wa kidunia ni uwepo wa tunda la Roho (Wagalatia 5:22–23). Tunda hili linaweza kuonekana katika yale tunayosema, yale tusiyosema, na hata katika namna ya sauti tunayotumia tunapoyasema. Upendo ni tunda la kwanza ambalo Paulo alilitaja, naye Yesu alisema, “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yohana 13:35). Hata hivyo, ninaogopa kwamba kama tungechunguza kwa pamoja maneno ya Wakristo mtandaoni, tungegundua kwamba tunapenda kuwa sahihi kuliko tunavyopendana.
Zaidi ya hayo, dunia huichukulia mitandao ya kijamii kwa mtazamo wa kimatendo tu. Ikiwa chapisho litapata mwitikio mkubwa na kuvutia algoriti zinazochagua maudhui yanayoonyeshwa kwenye taarifa za watumiaji wengine, litasambazwa kwa watu wengi. Ulimwengu unaendeshwa na kutafuta kuthibitishwa na wenzi na hata watu wasiowafahamu— wingi wa nayopendwa (likes) ni bora zaidi. Kwa upande mwingine, Wakristo wanapaswa kusukumwa na shukrani na hamu inayowezeshwa na Roho ya kumpendeza Mungu na Mkombozi wao, daima wakitazamia siku watakaposikia maneno haya: “Vema, mtumwa mwema na mwaminifu” (Mathayo 25:21). Hii ni tofauti kubwa sana, na Paulo alitarajia kwamba tofauti hiyo ingeonekana wazi kwa wale wanaotuzunguka. Katika kizazi cha ushawishi wa mitandaoni, ni muhimu kukumbuka kwamba idadi ya wafuasi si ya maana sana kama lilivyo swali la kama kweli unamfuata Yeye aliye wa maana.
Ikiwa mimi na wewe tutahitaji “kuukomboa wakati” (Wakolosai 4:5) kama Paulo anavyoamuru, tunahitaji kwanza kukiri nafasi nyingi zilizopo mtandaoni za kuwa mabalozi wa Kristo badala ya kupuuza tu fursa hizi za Agizo Kuu. Omba kwamba Bwana atusaidie kuwa mawakili wema na atujalie macho ya kiroho ya kuona hitaji lililopo. Hata hivyo, tunahitaji pia kukiri kiasi cha muda tunachoweza kuupoteza kwa urahisi mtandaoni tusipokuwa waangalifu, na kwa kufanya hivyo kukosa fursa za Agizo Kuu zinazojitokeza katika maeneo halisi ya wajibu wetu, iwe kama wenzi wa ndoa, wazazi, watoto, wafanyakazi, wanafunzi, au majirani. Mkristo mwenye hekima hutambua hali zote mbili.
Moja ya aya za kutisha zaidi katika Biblia kwangu ni onyo la Yesu kwamba tutatoa hesabu kwa “kila neno lisilo na maana” tunalolinena (Mathayo 12:36). Bila shaka hili linajumuisha pia yale tunayochapisha kwenye mitandao ya kijamii. Fikiria jinsi ambavyo mitandao ya kijamii huenda imeongeza na kuzidisha idadi ya maneno yasiyo na maana yanayonenwa na kuenezwa leo ikilinganishwa na hata miongo michache tu iliyopita. Na kama uwakili wetu wa kila neno linalonenwa utaletwa hukumuni, basi hakika uwakili wa kila dakika nao pia utaletwa hukumuni. Kama mwalimu mmoja wa Biblia alivyosema, mojawapo ya matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii yatakuwa kuthibitisha siku ya mwisho kwamba kutokuomba hakukutokana na ukosefu wa muda.
Ninapotafakari mara nyingi hitaji la hekima na matumizi ya hekima ya ukweli wa kibiblia kwa ajili ya kizazi chetu cha kidijitali, sijawahi kufikia hitimisho kwamba tayari nimefika. Sisi sote bado ni kazi inayoendelea. Kwa hiyo, mara nyingi mimi hurudia ahadi hiyo ya ajabu iliyotolewa na Yakobo “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa” (Yakobo 1:5). Hili ni ombi ambalo haliwezi kuombwa kupita kiasi, na ni ombi ambalo ninajua ninahitaji kuliomba mara nyingi zaidi. Bwana na alijalie kanisa Lake hekima linayohitaji ili kuvitumia vizuri vyombo na teknolojia za kizazi cha leo cha kidijitali, ili hatimaye Yeye apokee utukufu wote.
Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.



