Je, Yesu ni Mungu?

18 November 2026

Je, Yesu ni Mungu?

18 November 2026

Kutafuta Usafi Wetu na wa Kanisa

Umuhimu wa Usafi, kwa ajili ya mtu mwenyewe na kwa ajili ya kanisa, uliniongoza  kwa 2 Timotheo 2:22: “Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.”

Wengi huifikiria sehemu hii kuwa ni nasaha inayoelekezewa vijana. Katika muktadha huu, mtume anazungumzia vyombo vinavyotumika kwa ajili ya huduma katika nyumba kubwa. Nasaha hiyo ni kujitakasa mwenyewe ili kuwa chombo cha matumizi makubwa zaidi katika nyumba ya Bwana. Sehemu hii inawahusu vijana na wazee vilevile. Wote wameitwa kuutafuta usafi.

Kwa mtindo wa kawaida wa Paulo, mwito ni “kuvua” na “kuvaa” (tazama. Waefeso. 4:17–32; Wakolosai 3:1–17).

Kuvua. “Zikimbie tamaa za ujanani.” Ninapokaribia mwisho wa miongo saba ya maisha, ni wazi kwangu kwamba tamaa za ujanani si tatizo la vijana pekee. Tamaa hizo hutufuatilia maisha yetu yote. Huenda Paulo alikuwa akilenga mwelekeo wa vijana wa kupokea mafundisho potofu na yenye madhara ambayo huonekana kama ya hekima. Labda alikuwa akifikiria kutokuwa na subira na namna za zamani za kufikiri, kunakofuatana na kupenda mabishano; au labda tamaa ya kutaka wengine watufikirie kuwa sisi ni bora zaidi kuliko inavyopasa. Ni nani miongoni mwetu ambaye hajawahi kutamani kwamba shauku ingekuwa inahusishwa na vijana pekee?

Kuna tamaa nyingine ambazo mtu anaweza kuzihusisha na vijana: tamaa za ngono na kila namna ya uchafu wa uasherati katika mawazo au matendo. Fedha na mambo yote yanayoambatana nayo kama vile hadhi, heshima, na mamlaka ni majaribu yanayowakabili vijana na wazee kwa namna sawa. Tunaweza pia kuongezea ubinafsi uliokithiri, tamaa ya kujikuza,kujidai,  kujitukuza, na kiburi, pamoja na ukaidi wa kushupaza shingo. Tamaa hizi zinaonyesha mielekeo potofu inayowapata vijana na wazee kwa namna ileile. Hizi ni baadhi tu ya ishara za yale yanayopaswa kuvuliwa katika kuutafuta  usafi.

Kuvaa Kukimbia tamaa za dhambi si suala la kukatazwa tu au kujinyima tu. Usafi pia ni jambo linalopaswa kutafutwa kwa bidii. Katika 2 Tim. 2:22, Kujitahidi kuishi katika usafi kunaelezwa kwa njia tatu.

Haki. Tunajua kwamba haki ni kipawa kutoka kwa Mungu, inayotolewa kwa njia ya imani katika kifo cha Yesu cha kujitoa kuwa dhabihu na kufufuka kwake, ambayo hutukomboa kutoka katika dhambi (Warumi 3:22). Kuitafuta haki ni mchakato wa mabadiliko, kwa kuwa neema ya Mungu hurekebisha matendo yetu na tabia zetu ili ziendane na mapenzi ya Mungu yaliyofunuliwa. Kumtii Mungu na kufuatilia kwa makusudi kila kitu ambacho Mungu amekifunua kuwa kitakatifu lazima viwe alama ya mtoto wa Mungu.

Upendo. Kuitafuta haki daima kutazaa maisha ya upendo—upendo kwa Mungu na upendo kwa wengine. Upendo ni alama ya Mkristo. Upendo ndio unaowatambulisha Wakristo wa kweli kuwa wanafunzi wa Yesu(Yohana13:35). Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari. Upendo hufurahia kweli, hulinda, huamini, na hustahimili (1 Wakorintho 13). Wakristo wameitwa kumwiga Kristo kwa upendo wa kujitoa mhanga kwa ajili ya wengine (Waefeso 5:1–2).

Amani. Kuutafuta usafi ni kutafuta maisha ya amani. Tunda la kuhesabiwa haki ni kuwa na amani na Mungu (Warumi 5:1). Hata hivyo, amani si ya wima tu; amani pia ni ya mlalo. Paulo anahimiza, “Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote” (2 Timotheo 2:24). Naam, amani hutawala mioyo na nia za wale wanaompatia Mungu fadhaa zao (Wafilipi 4:7).

Tukiunganisha tena sehemu hizi mbili za wito wa mtume Paulo wa kuutafuta usafi, tunaona kwamba tunapaswa kukimbia hatari ya kiroho na kukimbilia mema ya kiroho. Tunaukwepa upande mmoja tunapoufuatilia upande mwingine. Huu ndio ujumbe thabiti wa Maandiko. Tunajikana ili tumfuate Kristo. Tunauvua utu wa kale na kuuvaa utu upya. Tunaikataa tamaa ya mwili na kusema ndiyo kwa Roho. Tunaweka mbali uongo, tukikumbatia na kusema kweli. Tunaacha mambo ya duniani na kufuata mambo ya mbinguni. Huu ndio mwito wa pande mbili wa maisha ya Kikristo—kuzikimbia tamaa zenye dhambi na kuutafuta usafi.

Mtume anaongeza kifungu katika 2 Timotheo 2:22 kinachosisitiza asili ya pamoja ya kuutafuta usafi: “pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.” Kuutafuta usafi kamwe si jitihada ya mtu peke yake. Kumwita Bwana kwa moyo safi ni alama ya kanisa. Katika takribani miaka hamsini ya huduma yangu, nimeona kwamba kila Mkristo aliye hai na anayekua, anayezikimbia tamaa zenye dhambi na kuutafuta usafi, ni sehemu muhimu ya familia ya kanisa la mahali pake. Kila Mkristo anahitaji mafundisho na maonyo ya ndugu wa kike na wa kiume katika Kristo, ambao ndani yao Neno la Kristo linakaa kwa wingi (Wakolosai 3:16). Afya ya kiroho na uchangamfu wake hupatikana kanisani.

Kanisa hutoa njia ambazo Mungu hutumia kututakasa, huku wachungaji wakilinda na kuangalia kwa uangalifu hali ya nafsi zetu. Tunahitaji wachungaji ambao mikono yao iko ndani ya manyoya ya kondoo, wakitafuta jambo lolote linaloweza kuhatarisha afya zetu za kiroho. Kuutafuta usafi kunahitaji kuwa chini ya uangalizi wa wachungaji. Zaidi ya hayo, mwendo wa Mkristo umejaa hatari. Kuna mbwa-mwitu watakaotaka kulimeza kundi. Kuna walimu wa uongo wanaotafuta wanafunzi kwa ajili ya mafundisho yao potofu. Kwa hiyo, Mungu ameweka waangalizi walitunze kanisa lake alilolinunua kwa damu yake mwenyewe (Mdo. 20:28–30).

Si kwamba uko tu chini ya uangalizi wa wachungaji, bali pia sisi ni sehemu ya kundi. Nimezungumza na Wakristo waliofikiri kwamba kukosa kwenda kanisani ni hasara yao binafsi tu. Walishindwa kuelewa hali ya ibada ya ushirika: kutiana moyo kwa kusikia wengine wakiimba sifa za Mungu, kuwaona wengine wakilisikiliza Neno la Mungu kwa makini, na kuwasikia wengine wakiomba. Kushiriki pamoja na wengine wamwitao Bwana ni njia muhimu ya neema.

Tunatafuta usafi kwa sababu ya kuipenda injili, lakini pia kwa ajili ya kanisa. Usafi ni jitihada takatifu tunapomwiga Kristo (Wafilipi 2:5). Jitihada ya kila Mkristo ya kumfuata Kristo na yote aliyo kwetu katika injili huwatia wengine moyo katika kuutafuta usafi na huchangia usafi wa kanisa.


Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.

Tedd Tripp

Tedd Tripp

Dkt. Tedd Tripp ni mchungaji mstaafu katika Kanisa la Grace Fellowship huko Hazleton, Pa., na rais wa Huduma za Shepherding the Heart. Yeye ni mwandishi wa kitabu kiitwacho Shepherding a Child's Heart.