
Njia za Baba katika Nyakati Ngumu
8 October 2026
Lengo la Maisha ni Lipi?
22 October 2026Toba ni nini?
Marko 1:14–15 ameandika maneno ya kwanza ya Yesu katika huduma Yake ya mahubiri hadharani: “Wakati umetimia, ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema.” Kwa kuwa tangazo la kwanza la Yesu la Injili lilijumuisha mwito wa kutubu dhambi, tunaweza kufikia uamuzi kwamba toba ni sehemu ya muhimu ya uanafunzi wa Kikristo. Ili tumfuate Yesu kwa uaminifu, lazima tuweze kujiuliza swali hili: Toba ni nini?
Toba Iletayo Uzima
Maungamo ya Imani ya Westminster na Katekisimu husaidia kwa kufupisha mafundisho ya biblia kuhusu mambo mengi, yakiwemo “toba iletayo uzima,” ambayo wanatheolojia wengine huiita “toba ya kiinjili.” Misemo yote miwili hutofautisha toba ya kweli iokoayo na huzuni ya kidunia isiyo toba ya kweli hata kidogo. Mtume Paul anazungumzia huzuni ya kimungu iletayo wokovu bila majuto, na anatuonya kuhusu huzuni ya kidunia ambayo huzaa mauti tu (2 Wakorintho 7:10–11) La muhimu, anatofautisha huzuni kwa sababu dhambi zetu zimemkosea Mungu na kuwaumiza wengine na huzuni kwa sababu ya matokeo ya dhambi. Toba isiyookoa ni huzuni ya jinsi dhambi zetu zivyotudhuru sisi tu au simanzi kwa sababu tumefumaniwa tukifanya kosa. Hii ndiyo aina ya huzuni aonayo mtoto anapokutwa mkono wake ukiwa ndani ya gudulia la biskuti, si pale anapokuwa mkweli kwamba amevunja kanuni za wazazi wake. Ndiyo aina ya hizuni ambayo Esau alionyesha alipoacha haki ya mzaliwa wa kwanza na baraka—huzuni si kwa sababu aliacha wema wa Mungu kwa bakuli la mchuzi, bali huzuni kwa sababu alipoteza urithi bora (Mwanzo 25:29–34; 27:1–41; Waebrania 12:16).
Vipengele vya Toba ya Kweli
Tofauti na toba ya kidunia isiyookoa, toba iletayo uzima ni kugeuka kutoka dhambini ili tuweze kumrudia Mungu kwa njia ya Kristo. Ungamo la Imani la Westminster 15.2 hutusaidia kufafanua vipengele vya toba ya kweli iokoayo. Linasema kwamba, “kwa [toba iletayo uzima], mwenye dhambi, kutokana na kuona na kutambua si hatari tu, bali pia uchafu na chukizo la dhambi zake, kuwa zipo kinyume na asili takatifu ya Mungu na sheria yake ya haki; na kwa kutambua rehema yake katika Kristo kwa wale watubuo, huona huzuni kuu kwa ajili ya dhambi zake na kuzichukia, hata kuziacha zote na kumgeukia Mungu, akiwa amekusudia na kujitahidi kutembea pamoja naye katika njia zote za amri zake.”
Kwanza, toba iletayo uzima hutambua si tu kwamba dhambi ni hatari kwetu, bali pia kwamba ni chafu na ya kuchukiza, kwa kuwa kila kosa ni uvunjaji wa sheria ya haki ya Mungu na linamvunjia heshima ya sifa Yake takatifu kabisa. Tunaona hili likidhihirika katika Zaburi 51:4, ambapo Daudi anakiri kwamba dhambi yake kuhusu Bathsheba na Uria ilikuwa dhambi dhidi ya Mungu peke Yake. Huu ni ushairi mbalagha. Bila shaka, kupanga mauaji ya Uria kulikuwa dhambi dhidi ya Mungu na pia dhidi ya Uria. David anamaanisha kwamba makosa yake, kwanza kabisa na kwa kiwango cha juu kabisa, ni dhambi dhidi ya Mungu. Kwa kuwa Bwana ni Muumba Mtakatifu na Mtoaji wa Sheria, nasi tumeumbwa kwa Mfano Wake, kila dhambi ni dhambi dhidi ya Mungu kabla haijawa dhambi dhidi ya mtu mwingine yeyote. Dhambi dhidi ya wengine ni dhambi dhidi ya mfano wa Mungu ulio ndani yao; hivyo, kwa namna hiyo hiyo, ni kama jaribio la kumuumiza Mungu. Dhambi zote ni “uhaini wa kiulimwengu,” kama R.C. Sproul alivyosema mara kwa mara. Ni majaribio ya kumbadilisha Mungu na amri Zake kwa sisi wenyewe na viwango vyetu.
Toba iletayo uzima haitambui tu kwamba dhambi zetu kimsingi ni dhidi ya Mungu, bali pia hushika rehema ya Mungu iliyo ndani ya Kristo kwa wanaotubu, kiasi kwamba mtenda dhambi huchochewa kumgeukia Bwana, kukiri dhambi, na kuomba msamaha (WCF 15.2). Hili pia tunaliona katika Zaburi 51, ambamo Daudi anakiri dhambi yake na kuomba rehema ya Mungu. Tafakari pia tofauti kati ya Yuda Iskariote na Mtume Petro. Wote wawili walitenda dhambi ya kuhuzunisha; Yuda alimkabidhi Yesu kwa wenye mamlaka, naye Petro alikana kwamba alikuwa mwanafunzi wa Yesu (Mathayo 26:14–16, 69–74). Wote wawili walihuzunika juu ya dhambi yao (Mathayo 26:75; 27:3–4). Hata hivyo, huzuni ya Yuda ilimalizikia katika kujiua, ilhali ya Petro ilisababisha kurudishwa katika huduma (Mathayo 27:5–10; Yohana 21:15–19). Kwa nini tofauti hii? Licha ya dhambi yake, Petro aliendelea kumkaribia Yesu—kwanza kuona kaburi tupu, kisha kula naye ufukweni (Yohana 20:1–10; 21:1–14). Petro alimkimbilia Yesu, akijua kwamba Yeye ni mwingi wa rehema kwa wanaotubu; Yuda alikimbia mbali na Yesu na kuishia kufa katika mikono yake mwenyewe, kwa sababu hakuamini rehema ya Mwokozi.
Hatimaye, katika toba iletayo uzima, mwenye dhambi huhuzunishwa na kuzichukia dhambi zake kiasi kwamba huziepuka, akiwa na azimio jipya la kumtii Mungu pamoja na juhudi ya kuweka azimio hilo katika matendo (WCF 15.2). Kwa maneno mengine, toba si kusema tu kwamba mtu anajutia dhambi zake halafu asifanye jitihada zozote kurekebisha maisha yake. Tunapaswa kuvua matendo ya giza na kumvaa Kristo (Warumi 13:11–14), tukikumbuka kwamba tumeumbwa upya katika Kristo, na kwa hiyo tutafute kuishi kama viumbe vipya jinsi tulivyo. Kugeuka huko kutoka dhambini hutokea kwa uamuzi thabiti wakati wa uongofu wetu, lakini huendelea kila siku katika maisha yetu yote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu,tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutokana na udhalimu wote (1Yoh. 1:8–9).
Wajibu na Fadhila za Toba
Haya yote hayamaanishi kwamba hatukutubu kweli iwapo tutatenda dhambi ileile zaidi ya mara moja. Yanamaanisha kwamba tunapaswa kuhoji uhalisia wa toba yetu ikiwa tunaipenda dhambi yetu na hatufanyi jitihada zozote kuiacha. Kwa wote wanaomjua Kristo, toba iletayo uzima ni wajibu wa kutimiza na pia ni fadhila inayotuwezesha kubaki katika ushirika usiokatizwa na Mwokozi wetu. Na tuchukie dhambi, tuombe msamaha, tujifunze njia ya Kristo, nasi tujitahidi kuitii sheria ya Mungu badala ya kuivunja.
Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Huduma za Ligonier.
Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.


