
Mambo Matatu Unayopaswa Kujua Kuhusu 2 Petro
13 Septemba 2025
Mambo Matatu Unayopaswa Kujua Kuhusu Obadia
17 Septemba 2025Mambo Matatu Unayopaswa Kujua Kuhusu Nahumu
Kitabu cha Nahumu si rahisi kukisoma. Ingawa ujumbe wake wa hukumu dhidi ya Ashuru unaonyesha kwamba Mungu hataruhusu dhambi kushinda, inaweza kuwa vigumu kufurahia kikamilifu kitabu hiki kinavyosherekea kuanguka kwa Ninawi au kuelewa jinsi mtazamo thabiti wa adhabu unavyofungamana na injili. Masuala haya na mengine kadhaa ya fasiri yanaweza kushughulikiwa ikiwa wasomaji watazingatia mambo matatu yafuatayo.
1. Injili ndiyo muktadha wa ujumbe wa Nahumu (Nah. 1:2–8).
Sehemu ya kwanza kuu, Nahumu 1:2–8, ina sauti hasi iliyowazi. Nahumu anachukulia kwamba ni jambo la hakika kuwa wanadamu wote, siyo Waashuru tu (ambao hawajatajwa katika sehemu hii), wamekashifiwa mbele ya haki kamilifu ya Mungu (Nah. 1:2–3, 5–6, 8). Hivyo basi, ni habari njema sana kwamba Mungu pia ni “ngome katika siku ya taabu” ambaye hutoa “kimbilio” kutoka kwa hukumu hiyo hiyo kwa wale wanaojikabidhi kwa huruma Yake (Nah. 1:7).
Iliwekwa kama ilivyo mwanzoni mwa kitabu, sehemu hii inatumika kama ufunguo wa fasiri kwa yale yanayofuata katika sehemu nyingine za kitabu. Dhambi za zamani za Yuda, uamuzi wa neema ya Mungu kuyamaliza mateso yake (Nah. 1:12), na dhoruba ya hukumu inayokaribia kuiangukia Ashuru, yote ni mifano ya kazi ya Mungu yenye pande mbili ya hukumu na wokovu. Zaidi ya hayo, licha ya utawala wa Ashuru unaoonekana kutoweza kuzuilika katika Mashariki ya Karibu ya kale, ikiwa ni pamoja na kuitawala Ufalme wa Kaskazini wa Israeli chini ya karne moja kabla ya Nahumu, kuingilia kati kwa Mungu kutaonyesha kwamba madai ya ukuu wa ufalme huo yalikuwa ya uongo, kama yalivyokuwa madai yake kwamba miungu yake ilikuwa imewezesha ukuu huo.
2. Ashuru si adui wa mwisho wa Mungu.
Ingawa Nahumu anailaani vikali Ashuru, na hasa Ninawi kama mji wake mkuu, Waashuru wengi hawakuhusika katika uchokozi wake, na baadhi ya raia wake walikuwa Waisraeli waliotekwa. Hakika, kitabu hiki kinazingatia kwa uthabiti wafalme wa Ashuru (Nah. 1:11, 14), majeshi (sehemu kubwa ya Nah. 2), na wengine wanaohusika katika mpango wake wa unyonyaji na kujitukuza, na kinafunua kwamba hukumu ya Mungu itawaangukia hasa wao. Kwa wafalme kama Esarhaddon (aliyetawala 681–669 KK), ambao walijitambulisha kama “mfalme wa dunia . . . mkuu wa watawala wote” na walitegemea “miungu mikuu” kama vile Marduk na Nabu, Bwana anasema tu, “Wewe huna umuhimu” (Nah. 1:14), na anaifanya iwe hivyo. Adhabu ya Mungu dhidi ya Ashuru-kama-ufalme ni onjo la hukumu Yake dhidi ya “Babeli” kwenye kitabu cha Ufunuo, ambayo inawakilisha siyo tu Roma, bali Babeli na Ninawi kabla yake, pamoja na nguvu zote za kibinadamu baada yake ambazo zinajulikana kwa vurugu, kujitolea kwa tamaa ya vitu au anasa, na kujikweza kwa kumpinga Mungu (Ufu. 17–18).
3. Mungu atawashinda maadui Wake wote na kuwaokoa watu Wake kikamilifu.
Kama Mungu hangejitoa kwa hiari na kwa neema kuwaokoa wenye dhambi, maangamizi ya maadui Wake wote yangepelekea wote kuhukumiwa na kufa (Warumi 5:12–14). Kwa namna ya ajabu, neema ya Mungu imevamia dunia ambayo imejitolea kikamilifu kujitambua kwa kujitegemea kwa masharti yake yenyewe, iwe ni katika ubeberu wa Ashuru wa zamani au aina nyingine za uasi dhidi ya Mungu katika wakati wa sasa.
Kwa kuzingatia nguvu ya dhambi, hukumu na wokovu ni sababu ya kushangilia. Wakati uovu na wale wanaouendeleza wanapoanguka, waathiriwa wao huwa na sababu ya kushangilia (Nah. 3:19; Ufu. 19:1–5). Vivyo hivyo, wale wanaopokea kwa furaha wokovu wa Mungu husherehekea neema na rehema zake kwao (Nah. 1:15) na wanatarajia utimilifu wa makusudi yake ya wokovu (Nah. 2:2).
Kuishi katika hali ya tayari siku za mwisho– na bado sizo siku za mwisho, ujumbe wa Nahumu unawataka waumini kudumisha imani katika ahadi za Mungu na kubomoa migongano mingi ya ulimwengu dhidi ya ukweli wa kiungu. Kama vile Nahumu alivyofichua asili ya ubinafsi na kujiangamiza kwa kuabudu sanamu na ubeberu wa Ninawi, Wakristo wanapaswa kukosoa aina nyingi ambazo watu binafsi, vikundi, na tamaduni nzima zinavyonyanganya haki ya Mungu katika kumfafanua mwanadamu kama anayejitawala, kutokuwa na ujuzi wa asili wa Mungu, na mwenye uwezo kamili wa kufikia furaha kamilifu peke yake.
Nahumu pia anawaalika waumini kubomoa mali za muda mfupi ambazo wanadamu wanashikilia juu zaidi, iwe ni utajiri wa mali, hadhi ya kijamii, usafi wa maadili wanaojipatia kwa kuonyesha wema, au kuimarisha mamlaka. Sanamu hizi ni sanamu tu—zimetengenezwa na wanadamu, haziwezi kuokoa au kuridhisha, na tayari zimeonyeshwa kuwa hazina uwezo (Nah. 1:13). Ukosoaji wa Nahumu kuhusu ubeberu wa Ashuru, chanzo chake ni injili, na inawaonyesha wasomaji wake jinsi ya kuchambua utamaduni kwa kuzingatia kazi ya Mungu ya hukumu na wokovu, na hivyo kusaidia kuwaandaa waumini wawe stadi kushuhudia imani yao. Pia inatulinda tusivutwe na ahadi za dunia au kuruhusu tumaini letu kutetereka mbele ya madai yake ya kudumu kuwa ndio chanzo cha kila kitu kizuri—cheo ambacho Bwana anajiwekea Mwenyewe, na ukweli unaookoa kabisa na kuwaridhisha wale wanaomjua (Nah. 1:7).
Makala haya yalichapishwa kwanza katika Blogu ya Huduma za Ligonier.


