
Anatujali
29 October 2026Kazi ya Mchungaji ni Nini?
Wakati mwanangu alipokuwa katika shule ya chekechea, alileta nyumbani wasifu wa juu juu aliokuwa ameuandika shuleni. Ulikuwa na picha yake na taarifa za msingi kumhusu yeye na familia yake. Moja ya maswali yaliyoulizwa lilikuwa, “Baba yako anafanya kazi gani?”
Ningependa jibu lake lingekuwa kitu kama, “Yeye ni mtumishi wa kanisa,” “Anahubiri Neno la Mungu,” au labda, “Anawaambia watu habari za Yesu.” Lakini hapana—hakukuwa na hata moja kati ya hayo hapo juu. Nilihuzunika, jibu lake lilikuwa tu, “Anafanya kazi kwenye kompyuta yake na kunywa kahawa.”
Ingawa ninaamini kwamba uelewa wa mwanangu kuhusu kazi ya baba yake umekomaa kadiri miaka ilivyosonga, tukio hilo la kuchekesha lilinifanya nigundue kwamba swali “Kazi ya mchungaji ni nini?” huenda si rahisi kujibuka, hata kwa watu wazima.
Basi, Kazi ya Mchungaji ni nini?
Mwito Maalum
Kazi ya mchungaji, kwanza kabisa, hutiririka kutoka katika mwito wake. Mwito wa huduma ya injili ni tofauti na mwito wa kawaida wa wokovu. Mtume Paulo anamkumbusha mfuasi wake kijana, Timotheo, kuhusu mwito huu maalum kupitia “kuwekewa mikono,” akiuita “wito mtakatifu” (2 Timotheo 1:6–9). Ni kweli ni mwito mtakatifu, kwa maana mhudumu ametengwa na kupitia kanisa ili kumwakilisha Bwana Yesu Kristo kwa maneno na matendo kama balozi wake, aliyepewa funguo za mamlaka za ufalme (2 Wakorintho 5:20; Mathayo 16:19.
Mamlaka haya ya uwakilishi hayapaswi kamwe kutumiwa kwa kujipandisha cheo (2 Wakorinth o4:5), wala kuwatawala kwa mabavu wale walio chini ya uangalizi wako (1Petro 5:3). Kinyume chake, wadhifa wa mchungaji ni wa utumishi wa unyenyekevu, kielelezo kutoka kwa Bwana wetu mwenyewe, aliyewaosha wanafunzi wake miguu (Yohana 13:1–17). Wanaohudumu kwa namna hii, wakiwa na mwito huu na kusudi hili mbele ya macho yao, wanaheshimiwa na Bwana—tena wanapaswa kuheshimiwa na mkutano waliokabidhiwa kuutunza (1Timotheo 5:17).
Kutokana na mwito huu majukumu matatu makuu yanatokea .
1. Kuongoza
La kwanza ni kuongoza kanisa la Bwana Yesu Kristo. Mchungaji ni kiongozi. Hata hivyo, uongozi huu usichanganywe na ule wa ulimwengu wa biashara, ambamo mara nyingi mafanikio hupimwa kwa matokeo ya mwisho.
Uongozi katika kanisa la Kristo, juu ya yote, ni uongozi kwa mfano—mfano wa utauwa na kufanana na Kristo. Yoshua alipowaongoza watu wa Mungu kuingia nchi ya ahadi, Bwana hakumpa mikakati ya kijeshi kuwa ufunguo wa ushindi. Badala yake, alimwagiza Joshua: “Usiache Kitabu hiki cha Torati kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani. Ndipo utakapofanikiwa na kisha usitawi” (Yoshua 1:8).
Vivyo hivyo, Paulo alipolihutubia kanisa la Korintho—kanisa lililogubikwa na migawanyiko na mkanganyiko wa maadili— Paulo aliwaelekeza kwa mfano wake mwenyewe kama mwongozo wa utauwa: “Igeni mfano wangu, kama ninavyuiga mfano wa Masihi” (1 Wakorintho 11:1).
Ni katika msingi huu wa uadilifu wa kibinafsi na kielelezo cha utauwa ndipo mhudumu anaweza kuwaongoza watu wa Mungu katika ibada ya Mungu na katika huduma ya kanisa.
2. Kutoa
Pili, mchungaji ameitwa kutoa kwa kanisa la Bwana Yesu Kristo. Kujitoa huku huja kupitia kwa huduma ya Neno, sakramenti, na sala. Hizi ndizo njia maalum—ingawa za kawaida—za neema ambazo Mungu ameziweka ili kuwahudumia watu wake kikamilifu na vya kutosha, akiweka wazi manufaa ya ukombozi wao ndani ya Kristo.
Kazi ya mhudumu ni kutoa kwa uaminifu na kwa uthabiti njia hizi kwa kundi lililokabidhiwa chini ya uangalizi wake. Asikengeushwe kupita kiasi na mambo mengine, hata yawe ya halali vipi. Mtume Petro anaweka umuhimu huu wazi katika Matendo 6, wakati mahitaji ya haraka yalipojitokeza kanisani kuhusu mgao wa kila siku wa chakula. Petro anajibu, “Haitakuwa vyema sisi kuacha huduma ya neno la Mungu ili kuhudumu mezani… Nasi tutatumia muda wetu kuomba na katika huduma ya neno” (Matendo 6:2, 4).
Mkazo huu haupunguzi umuhimu wa huduma nyingine ndani ya kanisa; bali unazipanga kwa usahihi chini ya msingi wa kutoa lishe ya kiroho. Petro alijifunza umuhimu huu moja kwa moja kutoka kwa Bwana wetu, aliyemkabidhi mara tatu, “Lisha kondoo wangu” (Yohana 21:17).
3. Kulinda
Tatu, mchungaji anapaswa kulilinda kanisa la Bwana Yesu Kristo. Wajibu huu unarudi hadi kwa Adamu, mtu wa kwanza, aliyewekwa katika bustani ya Edeni “ailime na kuitunza” (Mwanzo 2:15). Adamu aliagizwa kulipalilia bustani na kuilinda dhidi ya chochote kingeweza kuzuilia kustawi kwake. Kwa masikitiko, Adamu alishindwa katika jukumu hili la ulinzi, akidanganywa na nyoka kupitia mkewe Eva, na hivyo kuzamisha wanadamu wote katika dhambi.
Hadi leo, dhambi na Shetani wanaendelea kuisumbua dunia—na hasa kanisa. Kwa hiyo, mhudumu anapaswa awe makini katika kulilinda kundi. Ameitwa kuonya dhidi ya hatari za kiroho na kupigana vita dhidi ya mashambulizi ya yule mwovu (Waefeso 6:10–20). Katika kufanya hivyo, hutangaza kwamba ushindi wa mwisho tayari umepatikana kwa Bwana Yesu Kristo aliyefufuka na kupaa. Hata katikati ya mapambano yanayoendelea na anguko la ulimwengu na wa mioyo yetu, kanisa limesimama likiwa mshindi ndani Yake.
Zaidi ya hayo, mchungaji hana budi kujitahidi kudumisha amani na usafi wa kanisa. Mtume Paulo anawahimiza wazee wa Efeso katika agizo hili zito:
Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake. Lichungeni kanisa lake Mungu alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua kwamba baada yangu kuondoka, mbwa-mwitu wakali watakuja kati yenu, ambao hawatalihurumia kundi… Kwa sababu hiyo kesheni. (Matendo 20:28–31)
Majukumu hayo matatu—kuongoza, kutoa mahitaji, na kulinda—yanaweza kufupishwa vyema na mfano wa Biblia unaotumiwa mara nyingi kuhusu viongozi wa watu wa Mungu: mchungaji. Hata cheo cha “mchungaji” kinatokana na taswira hii ya kuchunga, kulisha, na kulea kundi la Kristo.
Kielelezo hiki cha uchungaji hupata mfano bora kabisa, nguvu yake endelevu, na usalama wake wa milele, katika Mchungaji Mkuu, Bwana Yesu Kristo, “yeye anayetoa uhai wake kwa ajili ya kondoo” (Yohana 10:11). Kwa sababu hiyo, Mtume Petro anawapa wahudumu wa Injili wosia huu usiopitwa na wakati:
lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa …kwa hiari,…bali kuweni vielelezo kwa hilo kundi. Naye Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa, mtapokea taji la utukufu lisiloharibika. (1 Petro 5:2–4)
Bwana, kwa neema yake, na awainue wachungaji wengi ambao kwa uaminifu watalichunga kanisa la Bwana Yesu Kristo.
Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.


