Sababu Tatu za Kuwapeleka Watoto Wako Kanisani

12 November 2026

Je, Yesu ni Mungu?

18 November 2026

Sababu Tatu za Kuwapeleka Watoto Wako Kanisani

12 November 2026

Je, Yesu ni Mungu?

18 November 2026

Ni ”Uzushi” Gani Mkubwa wa Kiprotestanti kuliko wote?

Hebu tuanze na swali la mtihani wa historia ya kanisa. Kadinali Robert Bellarmine (1542–1621) alikuwa mtu ambaye hakupaswa kupuuzwa. Alikuwa mwanatheolojia binafsi wa Papa Clement VIII na mmoja wa watu wenye uwezo mkubwa katika Harakati za Kupinga Mageuzo ndani ya Ukatoliki wa Kirumi wa karne ya kumi na sita. Katika tukio moja, aliandika: “Uzushi mkubwa wa Kiprotestanti kuliko wote ni _______ .” Kamilisha, eleza, na jadili kauli ya Bellarmine.

Ungejibuje? Ni uzushi gani mkubwa wa Kiprotestanti kuliko wote? Pengine kuhesabiwa haki kwa imani? Pengine Maandiko pekee, au mojawapo ya maneno mengine ya tahadhari ya Mageuzo?

Majibu hayo yana mantiki. Lakini hakuna hata moja yao yanamalizia sentensi ya Bellarmine. Alichokiandika kilikuwa: “Uzushi mkubwa wa Kiprotestanti kuliko wote ni uhakika wa wokovu.”

Tafakari ya muda inaeleza kwa nini. Ikiwa kuhesabiwa haki hakupatikani kwa imani pekee, katika Kristo pekee, kwa neema pekee — ikiwa imani inahitaji kukamilishwa na matendo; ikiwa kazi ya Kristo itarudiwa kwa namna fulani; ikiwa neema si bure na yenye mamlaka, basi kuna kitu kinachohitajika kufanywa, “kuongezwa” ili kuhesabiwa haki hatimaye kuwe kwetu. Hilo ndilo tatizo hasa. Kama kuhesabiwa haki mwishoni kunategemea kitu fulani ambacho tunapaswa kukamilisha, haiwezekani kufurahia uhakika wa wokovu. Kwa hiyo, kitheolojia, kuhesabiwa haki mwishoni kunategemea na hakujulikani, na haiwezekani kwa mtu yeyote (isipokuwa kwa ufunuo maalum, Roma ilikubali) kuwa na uhakika wa wokovu. Lakini ikiwa Kristo amefanya kila kitu, ikiwa kuhesabiwa haki ni kwa neema, bila kazi za kuchangia; kunapokelewa kwa mikono mitupu ya imani – basi uhakika, hata “uhakika kamili” unawezekana kwa kila muumini.

Si ajabu Bellarmine alifikiri kuwa neema kamili, huru, isiyozuiliwa ilikuwa hatari! Si ajabu kwamba Wanamageuzo waliipendelea barua kwa Waebrania!

Hii ndiyo sababu, mwandishi wa Waebrania anaposita kuvuta pumzi kwa muda katika kilele cha maelezo yake ya kazi ya Kristo (Waebrania 10:18), anaendelea na hoja yake kama vile Paulo “kwa hivyo”  (Waebrania 10:19). Kisha anatuhimiza kwa ”tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu ……….kwa imani timilifu,” (Waebrania 10:22). Hatuhitaji kusoma tena barua yote ili kuona nguvu ya kimantiki ya “kwa hiyo” yake. Kristo ni Kuhani wetu Mkuu; mioyo yetu ikiwa imenyunyizwa damu ya Kristo na kuwa safi kutokana na dhamiri mbaya nayo miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi. (Mstari wa 22).

Kristo amekuwa dhabihu ya mara moja kwa dhambi zetu, na amefufuliwa na kuthibitishwa katika nguvu za maisha yasiyoharibika kama kuhani wetu mwakilishi. Kwa imani ndani Yake, sisi ni wenye haki mbele ya kiti cha enzi cha Mungu kama vile Yeye alivyo mwenye haki. Kwa maana tumehesabiwa haki katika haki Yake, Kuhesabiwa haki kwake pekee yake ni kwetu pia! Na hatuwezi kamwe kupoteza kuhesabiwa haki huku zaidi ya Yeye kuanguka kutoka mbinguni. Hivyo basi, kuhesabiwa haki kwetu hakuhitaji kukamilishwa zaidi kuliko kule kwa Kristo!

Kwa mtazamo huu, mwandishi anasema, “kwa sababu kwa dhabihu moja amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa.” (Waebrania 10:14). Sisi na tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu kwa imani timilifu, “mioyo yetu ikiwa imenyunyizwa damu ya Kristo na kuwa safi kutokana na dhamiri mbaya nayo miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi” (Waebrania 10:22).

“Ah,” ilijibu Roma ya Kadinali Bellarmine, “fundisha hili na wale wanaoamini wataishi kwa uhuru na upinzani dhidi ya sheria.” Lakini sikiliza badala yake mantiki ya Waebrania. Kufurahia uhakika huu kunapelekea mambo manne: Kwanza, uaminifu usiotetereka kwa ungamo letu la imani katika Yesu Kristo pekee kama tumaini letu (m.23); pili, kuzingatia kwa makini jinsi tunavyoweza kuhamasishana katika “upendo na matendo mema” (m.24); tatu, ushirika unaoendelea na Wakristo wengine katika ibada na kila kipengele cha ushirika wetu (m.25a); nne, maisha ambayo tunahimizana kuendelea kumtazama Kristo na kuwa waaminifu kwake, kadri wakati wa kurudi kwake unavyozidi kukaribia (25b).

Ni mti mzuri unaozaa matunda mazuri, si kinyume chake. Hatuokolewi kwa matendo; tunaokolewa kwa ajili ya matendo. Kwa hakika sisi ni kazi ya mikono ya Mungu tukiwa kazini (Waefeso 2:9–10)! Hivyo, badala ya kuishi maisha ya kutojali maadili na kutojali kiroho, kazi ya Yesu Kristo iliyokamilika mara moja na inayozalisha imani yenye uhakika kamili, inawapa waumini msukumo wenye nguvu zaidi wa kuishi kwa ajili ya utukufu na furaha ya Mungu. Zaidi ya hayo, uhakika huu kamili umejikita katika ukweli kwamba Mungu Mwenyewe amefanya haya yote kwa ajili yetu. Ameufunua moyo wake kwetu katika Kristo. Baba hahitaji kifo cha Kristo ili kushawishiwa kutupenda. Kristo alikufa kwa sababu Baba anatupenda (Yohana 3:16). Yeye hajifichi nyuma ya Mwanawe kwa nia mbaya akitamani kututendea mabaya — kama siyo kwa ajili ya dhabihu ambayo Mwanawe alitoa! Hapana, mara elfu hapana! — Baba Mwenyewe anatupenda katika upendo wa Mwana na upendo wa Roho.

Wale wanaofurahia uhakika huo hawaendi kwa watakatifu au kwa Mariamu. Wale wanaomtazama Yesu pekee hawahitaji kutazama kwingineko. Ndani Yake tunafurahia uhakika kamili wa wokovu. Uzushi mkubwa kuliko wote? Ikiwa ni uzushi, basi na nifurahie huu “uzushi” uliobarikiwa zaidi! Kwa maana ni ukweli na neema ya Mungu mwenyewe!


Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.

Sinclair B. Ferguson

Sinclair B. Ferguson

Dkt. Sinclair B. Ferguson ni Profesa wa Theolojia ya Kimsingi katika Seminari ya Reformed Theological Seminary. Awali alihudumu kama mhudumu kiongozi wa Kanisa la Kwanza la Presibiteri huko Columbia, S.C. Yeye ni mwandishi wa vitabu vingi, ikiwa ni pamoja na Katika Mwaka wa Bwana Wetu.