Mambo Matatu Unayopaswa Kujua Kuhusu Ufunuo
20 January 2026
Mambo Matatu Unayopaswa Kujua Kuhusu Sefania
27 January 2026
Mambo Matatu Unayopaswa Kujua Kuhusu Ufunuo
20 January 2026
Mambo Matatu Unayopaswa Kujua Kuhusu Sefania
27 January 2026

Mambo Matatu Unayopaswa Kujua Kuhusu Esta

Kitabu cha Esta hakitaji moja kwa moja jina la Mungu. Kwa hakika, hadithi hiyo haina sana mambo ya dini na uchaji kwa jumla. Wahusika wakuu hawaonekani kuwa Wayahudi wacha Mungu na waaminifu wanaojali mno kulishika agano la Mungu. Tunaweza kujifunza nini kuhusu Mungu na njia Zake katika kitabu kama hiki?

Licha ya upendo wangu kwa Esta na hadithi yake (mmoja wa binti zangu anaitwa Hadasha, jina la Kiyahudi la Esta), lazima nikiri kwamba kuna nyakati katika simulizi hii ambapo najiuliza matumaini ya kweli ya Esta na Mordekai yako wapi na kama matendo yao yanaakisi imani iliyoelezewa katika Waebrania 11. Licha ya hisia hizi za awali, ukichunguza kwa karibu, Esta anatufundisha ukweli wa kina wa kitheolojia ambao unaweza kuimarisha maisha ya Kikristo. Haya hapa  ni mambo matatu ya kujua kuhusu kitabu cha Esta.

1. Uaminifu wa Agano la Mungu: Kitabu cha Esta ni simulizi ya kusisimua kuhusu kukaribia kutokomezwa kwa ahadi za agano la Mungu.

Esta anatokea mbali sana na nchi ya ahadi. Baadhi ya Waisraeli walikuwa wamerudi Yerusalemu kutoka uhamishoni baada ya amri ya Koreshi mwaka 539 KK (tazama Ezra 1:1–4). Hata hivyo, baadhi waliamua kubaki Uajemi. Msomaji anatambulishwa haraka kwa mmoja wa Wayahudi waliobaki. Anachukuliwa haraka na kuingia katika maisha ya kifalme ya Kiajemi,na kuwa malkia baada ya mfalme wa Uajemi kuaibishwa na ujeuri wa malkia wake wa awali.

Kupitia ustadi wa hali ya juu wa kusimulia unaoambatana na msisimko, kejeli, na tashtiti, mwandishi anasimulia jinsi ishara ndogo isiyo ya maneno ilivyoanzisha ugomvi binafsi kati ya wanaume wawili (Hamani Mwamaleki na Mordekai Myahudi). Ugomvi huu karibu ungepelekea maangamizi ya watu wa agano la Mungu (na hivyo, ahadi Zake) kupitia mauaji ya kimbari yaliyoidhinishwa na serikali. Ni kupitia tu kipindi cha kukosa usingizi kwa mfalme mpumbavu na ujanja wa muda mfupi wa malkia aliyepotoka kimaadili kwamba hali inabadilika dakika za mwisho. Kiongozi wa mauaji ya kimbari, Hamani, anaishia kunyongwa katika mti aliouandaa kwa ajili ya Mordekai, adui yake, na Wayahudi wanaokolewa dhidi ya maangamizi.

Kitabu hiki kinasomeka kama riwaya ya kusisimua, na kama hujasoma hadithi hii kwa mkupuo mmoja, nakuhimiza ufanye hivyo. Mabadiliko ya matukio yanatufundisha jambo muhimu sana: Mungu amejitoa kutimiza ahadi Zake za agano kwa Abrahamu, Isaka, na Yakobo, na hakuna kikaragosi wa Shetani—sio Farao, sio Ahabu, sio Absalomu, sio Nebukadneza, sio Hamani—anaweza kuzuia ahadi ya agano la Mungu ya kuhifadhi watu kwa ajili Yake Mwenyewe.

2. Upaji wa Mungu usioonekana: Kitabu cha Esta kiko kimya kumhusu Mungu ili kutufundisha jambo fulani kwa sauti kubwa kumuhusu Mungu.

Simulizi zilizokaribia dhihaka katika kitabu cha Esta zinaonyesha kimaandishi kazi za utawala wa Mungu, ambazo Katekisimu ya Heidelberg inaelezea.

Upaji wa Mungu ni uweza mkuu na nguvu iliyopo daima ya Mungu ambayo Mungu hushikilia, kana kwamba kwa mkono wake, mbingu na dunia na viumbe vyote, na hivyo kuvitawala kiasi kwamba jani na unyasi, mvua na ukame, miaka ya mavuno na ya upungufu, chakula na kinywaji, afya na ugonjwa, ufanisi na umaskini—mambo yote, kwa hakika, hayaji kwetu kwa bahati bali kwa mkono wake wa ubaba.

Inaweza kuonekana kwamba kila kitu katika kitabu cha Esta kinatokea kwa bahati tu, lakini msomaji mwenye mawazo ya kimbinguni atatambua kwamba kuna Mwandishi Mkuu anayeongoza mambo yote kwa ajili ya mema ya watu wake wa agano—wale wanaompenda na walioitwa kwa kusudi lake (Rum. 8:28). Hakuna ajali katika upaji wa Mungu unaotunza. Kila tukio la bahati katika kitabu cha Esta linapiga kelele juu ya upaji kimya na usioonekana wa Mungu unaoongoza viumbe wake wote na matendo yao yote (WSC 11). Ukimya wa Mungu katika kitabu hiki unafundisha somo muhimu sana. Utawala wake wenye nguvu zote na utunzaji wa viumbe vyote ni kimya mno kiasi kwamba hauwezi kupuuzwa. Hakuna kitu kilicho nje ya upaji wake wa kimungu, hata ikiwa hatumuoni Mwandishi akielekeza mchezo wake.

3. Uchaguzi wa Mungu wa Watu Wenye Upungufu: Kitabu cha Esta kinaacha maswali mengi ya kimaadili bila majibu kuhusu wahusika wake wakuu, ambao ni watu wa agano la Mungu.

Sawa na mtindo wa simulizi za Kiebrania, mwandishi wa kitabu cha Esta anasimulia matendo bila kutoa tathmini ya kila kitendo. Hili limepelekea wahusika wawili wakuu —Esta na Mordekai—kuonekana kama mashujaa wa maadili na imani. Hata hivyo, simulizi hii ni mchanganyiko wa hofu na imani, na si rahisi kwa msomaji kuzitofautisha ipi ni ipi . Kuna maswali mengi yasiyo na majibu ambayo msomaji anaachwa nayo kuhusu tabia na matendo ya Esta na Mordekai. Baadhi ya maswali hayo ni pamoja na:

  • Kwa nini Mordekai na Esta hawakurudi katika nchi yao (Esta 2:5)?
  • Je, Esta hakujali sheria za chakula zilizowekwa na Bwana, au alikuwa tu mwathirika asiye na hatia wa hali zake (Esta 2:9)?
  • Kwa nini Mordekai alimshauri Esta asifichue urithi wake wa kidini (Esta 2:10, 20)?
  • Kwa nini Mordekai, badala ya kupinga, alimruhusu mpwa wake kupelekwa katika hekalu la mfalme (Esta 2:8) na katika chumba cha kulala cha mfalme wa mataifa, mtalaka wa hivi karibuni (Esta 2:15–18)?
  • Je, kukataa kwa Mordekai kumsujudia Hamani, ambako kulisababisha matokeo makubwa, ilikuwa kitendo kidogo au msimamo wa imani (Esta 3:2)?
  • Je, Esta alitenda kwa ubinafsi au hekima katika kukataa kwake kwa awali kumsihi mfalme kwa niaba ya watu wake (Esta 4:10–11)?
  • Je, Mordekai, baada ya Esta kukataa ombi lake la awali la kumwomba mfalme kuwaokoa Wayahudi, alitishia kumfichua mpwa wake au alikuwa akitoa onyo la neema (Esta 4:12–14)?
  • Je, Esther alikuwa mdanganyifu au mwenye busara katika maombi yake ya chakula cha jioni kwa mfalme na Hamani (Esta 5:4–8)?
  • Je, Esther alikuwa katili kwa kulipiza kisasi au alichukua fursa kwa haki katika ombi lake la kuwaruhusu Wayahudi kuua wanaume mia tatu zaidi na kuwanyonga wana kumi wa Hamani kwenye mti wa kunyongea (Esta 9:13–15)?

Wakati maswali haya yanaweza kuonekana kama shida zisizoshughulishika—kwa kuwa watu wa Mungu wanaohusika katika historia ya ukombozi, wanawezaje kuonyesha utata wa kimaadili wa aina hii?—badala yake yanatoa mwanga juu ya habari njema kwamba wokovu wa Mungu hautegemei uaminifu au ukosefu wa uaminifu wa watu wake. Yeye ni mwaminifu kwa ahadi za agano lake kwa ajili ya jina lake (tazama Isa. 48:9–11; Ezek. 20:44). Esther na Mordekai—kwa matendo yao ya dhambi, ya hofu na matendo yao ya haki, ya uaminifu—wanatekeleza mpango wa Mungu usioweza kuzuilika na thabiti wa “kuitendea mema Sayuni” (Zab. 51:18). Hii ndiyo maana halisi ya simulizi nzuri ya Hadassah. Ingawa ni “mti wa mirhi” rahisi (maana ya Kiebrania ya “Hadassah”) asiyeweza kufanya kila kitu vizuri, Malkia Esther ni chombo cha Bwana cha kuhifadhi baraka za agano lake na kutekeleza makusudi yake ya kiupaji. Hili halina utata wowote katika simulizi ya Esta.

Makala hii ni sehemu ya mkusanyiko wa Kila Kitabu cha Biblia: Mambo 3 ya Kujua.


Makala haya yalichapishwa kwanza katika Blogu ya Huduma za Ligonier.

Aaron L. Garriott
Aaron L. Garriott
Mchungaji Aaron L. Garriott ni mhariri mkuu wa jarida la Tabletalk, profesa msaidizi mkazi katika Chuo cha Biblia cha Reformation huko Sanford, Florida, na alihitimu kutoka Wheaton College na Reformed Theological Seminary huko Orlando, Florida. Yeye ni mzee anayefundisha aliyewekwa wakfu katika Kanisa la Presbyterian nchini Marekani.