
Kwa kuwa Mungu ni Mwenye Enzi, Binadamu Wako Huru Vipi?
23 Juni 2025
Vyanzo vya Theolojia ya Kimfumo
23 Juni 2025Je, Mageuzo Yameisha?

Kumekuwa na maoni kadhaa yaliyotolewa juu ya mada hii na wale ambao ningewaita “wanainjili wa zamani.” Mmoja wao aliandika, “Luther alikuwa sahihi katika karne ya kumi na sita, lakini swali la kuhesabiwa haki si suala sasa.” Mwanainjili mwingine aliyejitangaza mwenyewe alitoa maoni katika mkutano wa waandishi wa habari niliouhudhuria kwamba “mjadala wa karne ya kumi na sita wa Mageuzo kuhusu kuhesabiwa haki kwa imani pekee ulikuwa dhoruba ndani ya kikombe cha chai.” Bado Mwanatheolojia mwingine maarufu wa Ulaya amedai katika maandishi kwamba mafundisho ya kuhesabiwa haki kwa imani pekee si suala muhimu tena katika kanisa. Tunakabiliwa na kundi la watu ambao wanajulikana kama Waprotestanti lakini ambao kwa dhahiri wamesahau kabisa kile wanachopinga.
Kinyume na baadhi ya tathmini hizi za kisasa kuhusu umuhimu wa mafundisho ya kuhesabiwa haki kwa imani pekee, tunakumbuka mtazamo tofauti wa Wanamageuzi ngangari wa karne ya kumi na sita. Luther alitoa maoni yake maarufu kwamba mafundisho ya kuhesabiwa haki kwa imani pekee ndicho kipengele ambacho kwacho kanisa linasimama au linaanguka. John Calvin aliongeza sitiari nyingine, akisema kwamba haki ni bawaba ambayo kwayo kila kitu hugeuka. Katika karne ya ishirini, J.I. Packer alitumia sitiari inayoonyesha kwamba kuhesabiwa haki kwa imani pekee ni “Atlasi ambayo mabegani mwake kila mafundisho mengine husimama.” Baadaye Packer aliondoka kwenye sitiari hiyo yenye nguvu na kurudi kwenye sitiari dhaifu zaidi, akisema kwamba kuhesabiwa haki kwa imani pekee ni “maandishi madogo ya injili.”
Swali tunalopaswa kukabiliana nalo kwa kuzingatia mijadala hii ni, kipi kimebadilika tangu karne ya kumi na sita? Naam, kuna habari njema na kuna habari mbaya. Habari njema ni kwamba watu wamekuwa wastaarabu zaidi na wenye uvumilivu katika mabishano ya kitheolojia. Hatuoni watu wakiteketezwa au wakiteswa kwa sababu ya tofauti za mafundisho ya imani. Tumeona pia katika miaka iliyopita kwamba ushirika wa Kirumi umebaki imara katika masuala mengine muhimu ya imani ya Kikristo, kama vile uungu wa Kristo, upatanisho wake mbadala, na uvuvio wa Biblia, ambapo wengi wa Waprotestanti walio huru wameyaacha mafundisho haya maalum kabisa. Tunaona pia kwamba Roma imeendelea kuwa imara katika masuala muhimu ya maadili kama vile utoaji mimba na mtazamo wa kimaadili. Katika karne ya kumi na tisa Mkutano wa Kwanza wa Vatikani, Roma uliwaita Waprotestanti ‘‘waasi na wagawanya kanisa.” Katika karne ya ishirini katika Vatikani II, Waprotestanti walitajwa kama “ndugu waliojitenga.” Tunaona tofauti kubwa katika kauli za mabaraza haya tofauti. Habari mbaya, hata hivyo, ni kwamba mafundisho mengi ambayo yaliwatenganisha Waprotestanti wa kiorthodoksi na Wakatoliki wa Kirumi karne nyingi zilizopita yametangazwa kuwa mafundisho rasmi yasiyopingika tangu karne ya kumi na sita. Karibu maagizo yote muhimu kuhusu Mariolojia yametangazwa katika kipindi cha miaka 150 iliyopita. Mafundisho ya kutokosea kwa Papa, ingawa kwa vitendo yalikuwa yakitumika hata kabla ya kufafanuliwa rasmi, yalifafanuliwa na kutangazwa rasmi kuwa de fide (yaani, jambo linalopaswa kuaminiwa kwa ajili ya wokovu) mwaka 1870 katika baraza la kwanza la Vatikani. Pia tunaona kwamba katika miaka ya hivi karibuni ushirika wa Kirumi umechapisha katekisimu mpya ya Kikatoliki, ambayo inathibitisha bila shaka mafundisho ya Baraza la Trent, ikiwa ni pamoja na ufafanuzi wa Trent wa mafundisho ya kuhesabiwa haki (na hivyo kuthibitisha laana za baraza hilo dhidi ya mafundisho ya kimageuzo ya kuhesabiwa haki kwa imani pekee). Pamoja na uthibitisho wa Trent kumekuja uthibitisho wazi wa mafundisho ya Kirumi ya toharani, msamaha wa dhambi, na hazina ya thawabu.
Katika majadiliano kati ya wanatheolojia wakuu kuhusu suala endelevu muhimu la mafundisho ya kuhesabiwa haki kwa imani pekee, Michael Horton aliuliza swali hili: “Ni nini katika miongo ya hivi karibuni ambacho kimeifanya injili ya karne ya kwanza isiwe muhimu?” Mgogoro kuhusu kuhesabiwa haki haukuwa juu ya hoja ya kiufundi ya theolojia ambayo ingeweza kuwekwa pembeni mwa hazina ya ukweli wa kibiblia. Wala haingeweza kuchukuliwa tu kama dhoruba katika kikombe cha chai. Dhoruba hii ilienea mbali zaidi ya ukubwa wa kile kikombe cha chai. Swali hili, “nifanye nini ili niokolewe?” bado ni swali muhimu kwa mtu yeyote ambaye amekumbana na ghadhabu ya Mungu.
Hata muhimu zaidi kuliko swali ni hilo jibu, kwa sababu jibu hilo linagusa moyo wa ukweli wa injili. Katika uchambuzi wa mwisho, Kanisa Katoliki la Kirumi lilithibitisha huko Trent na linaendelea kuthibitisha sasa kwamba msingi ambao Mungu atamtangaza mtu kuwa mwenye haki au asiye na haki unapatikana katika “haki ya asili” ya mtu. Ikiwa haki haimo ndani ya mtu, mtu huyo katika hali mbaya zaidi huenda kuzimu na katika hali bora zaidi (ikiwa kuna uchafu wowote uliobaki katika maisha yake) huenda toharani kwa muda ambao unaweza kufikia mamilioni ya miaka. Katika tofauti kubwa na hilo, mtazamo wa kibiblia na Kiprotestanti kuhusu kuhesabiwa haki ni kwamba msingi pekee wa haki yetu ni haki ya Kristo, ambayo haki hiyo inahesabiwa muumini, ili wakati mtu anapokuwa na imani ya kweli kwa Kristo, yote yanayohitajika kwa wokovu yanakuwa yake kwa sababu ya kuhesabiwa haki ya Kristo. Swala la msingi ni hili: je, msingi ambao nina hesabiwa haki ni haki yangu mwenyewe? Au ni haki ambayo, kama Luther alivyosema, ni ‘haki ya kigeni’—haki ambayo ni ‘extra nos’, yaani haki iliyo nje yetu sisi binafsi—haki ya mwingine, yaani, haki ya Kristo? Kuanzia karne ya kumi na sita hadi sasa, Roma daima imefundisha kwamba kuhesabiwa haki kunategemea imani, kwa Kristo, na kwa neema. Tofauti, hata hivyo, ni kwamba Roma inaendelea kukataa kwamba haki inamtegemea Kristo pekee, inapokelewa kwa imani pekee, na inatolewa kwa neema pekee. Tofauti kati ya mitazamo hii miwili ni tofauti kati ya wokovu na kinyume chake. Hakuna suala kubwa zaidi linalomkabili mtu ambaye ametengwa na Mungu mwenye haki.
Kwa wakati huu Kanisa Katoliki la Kirumi lilipokemea fundisho la kibiblia la kuhesabiwa haki kwa imani pekee, lilikana injili na kuacha kuwa kanisa halali, pasipo kutilia maanani uthibitisho wake wote wa mafundisho sahihi ya Kikristo. Kulikubali kama kanisa halisi wakati linaendelea kukataa mafundisho ya kibiblia la wokovu ni sifa mbaya. Tunaishi katika wakati ambapo mgogoro wa kitheolojia unachukuliwa kuwa si sahihi kisiasa, lakini kutangaza amani wakati hakuna amani ni kusaliti moyo na roho ya injili.
Makala haya yalichapishwa kwanza katika Blogu ya Huduma za Ligonier.