Njia Tatu za Kuwafundisha Vijana Theolojia
10 April 2026
Ufuasi katika Familia
16 April 2026
Njia Tatu za Kuwafundisha Vijana Theolojia
10 April 2026
Ufuasi katika Familia
16 April 2026

Nawezaje Kukua Katika Imani Yangu?

Fikiria mtu anayezama katika bahari yenye dhoruba ambaye anatupiwa boya. Katika hali ya kukata tamaa, anashika boya hilo, anashikilia,na anaingia ndani yake. Hatimaye, anaanza kuongelea kwenye mawimbi ya kutisha. Bado akiwa amejaa hofu na mashaka, anawasiwasi huenda boya hilo likamwangusha kwa namna fulani, na amezwe na vilindi vya maji. Fikiria anatambua kwamba ndani ya boya hilo muna kijitabu kidogo kisicholowa maji. Mtu huyo mwenye wasiwasi—licha ya hali hiyo—anaanza kusoma na kugundua kwamba kijitabu hicho kinasifu  boya lake la kuokoa maisha. Anasoma kuhusu malighafi ambayo ilitumika kutengezewa, sura ya muundo wake, na sifa zake za ajabu za kuelea na kutegemewa. Anasoma jinsi lilivyopimwa kwa kina, jinsi lilivyobeba uzito mzito zaidi katika bahari kali, na kwamba hakuna mtu aliyelishikilia aliwahi kuzama. Jinsi anavyosoma, imani yake inaongezeka.

Je, bado yuko katikati ya dhoruba za bahari? Ndiyo. Je, mawimbi makubwa ya mara kwa mara yanaweza kumfanya awe na wasiwasi mkubwa? Ndiyo. Je, yuko salama zaidi au ana uhakika zaidi kuliko alivyokuwa? Hapana. Yuko salama na uhakika kama alivyokuwa mara ya kwanza aliposhika boya hilo la kuokoa maisha, ila sasa ana imani kubwa na inayoongezeka katika uwezo wake wa kumshikilia kupitia hatari na matatizo yote anayokabiliana nayo, hadi hatimaye anapotolewa kutoka kwenye maji na kuletwa salama kwenye nchi kavu.

Kukubali mipaka ya mfano huo, wacha nipendekeze baadhi ya mifano inayofanana katika ukuaji wa imani. Mwenye dhambi anapomwamini Yesu kwa mara ya kwanza, mwenye dhambi huyo huokolewa na kuwa salama. Hakuna mtu wala kitu kinachoweza kumng’oa kutoka mikono mwa Yesu. Yuko salama kadiri awezavyo kuwa. Lakini huenda asielewe kikamilifu usalama wake. Anajua ya kutosha kuja kwa Kristo lakini anahitaji kujua zaidi kumhusu Kristo ambaye amemjia. Ujasiri wake utaongezeka tu anapomjua zaidi Mwokozi ambaye anamwamini. Hili linawezaje kufikiwa vipi?

Kwanza kabisa, ukuaji wa kiroho huja kupitia Maandiko. Hiki ni kitabu ambacho si tu humfanya mtu kuwa na hekima kwa ajili ya wokovu kupitia imani katika Kristo, bali pia humfanya mtu wa Mungu kuwa kamili. Wakristo wanahitaji injili daima. Tunahitaji kuweka macho yetu kwa Kristo, kumfikiria Mtume na Kuhani Mkuu wa maungamo yetu, Kristo Yesu (Ebr. 3:1). Angalia jinsi dhidi ya mitego na huzuni zote za maisha ya Kikristo, usumbufu na udanganyifu wote wa mafundisho ya uongo, Mitume wanamweka Kristo na Yeye aliyesulubiwa mbele ya macho ya watu wa Mungu kwa ajili ya kuongeza imani yao. Kwa kujifunza Kristo katika Maandiko, tunamtazama Yesu, Mwanzilishi na Mkamilishaji wa imani yetu, na hivyo imani yetu inakua.

Njia ya pili ya kukua katika imani ni kwa kumwomba kwa Mungu ili Roho Wake afanye kazi ya imani kubwa zaidi. Yeye ndiye mtoaji wa imani, na hivyo lazima Yeye awe ndiye anayeipatia nguvu. Wanafunzi waliomba, “Tuongezee imani yetu!” (Luka 17:5). Baba mwenye shida alipiga kelele, “Naamini; nisaidie kutokuamini kwangu!” (Marko 9:24). Maombi kama haya yanatukumbusha kwamba imani ya kweli inaweza kuwa dhaifu au yenye nguvu zaidi na kutuonyesha kwamba mojawapo ya njia ambazo imani inaongezeka ni kwa kuiomba. Kwa kujibu, Kristo anatufunulia zaidi kuhusu Yeye Mwenyewe. Labda hatuna kwa sababu hatujaomba (Yakobo 4:2)?

Njia nyingine tamu ya kuongeza imani ni ushirika na watakatifu. Ulimwengu utanyonya imani yetu na Shetani ataishambulia, akitupotosha kutoka kwa Kristo, akituvuruga kutoka kwa ukweli, na kututaka tuzingatie mambo mengine. Njia moja ya kupendeza ya kukabiliana na hili ni kutumia muda na watu wa Mungu, tukizungumza juu ya yale yanayohusu ufalme (Malaki 3:16–18). Katika ushirika huo na watakatifu, hisia zetu za mambo ya mbinguni zinaburudishwa na kurejeshwa, na faraja zinawasilishwa (1 Wathesalonike 4:18, 5:11).

Hilo linatuleta kwenye tajiriba—yetu na ya wengine. Kusoma Biblia zetu kunatuonyesha jinsi imani ya watu wa Mungu inavyoongezeka kupitia majaribu. Ibrahimu, baba wa waaminifu, alipitia majaribio na ushindi wa imani (Rum. 4:20). Waandishi wa zaburi walijitia nguvu kwa kukumbuka matendo ya zamani ya Mungu. ina manufaa kusoma na kusikiliza waumini wengine, wa zamani na wa sasa, kuhusu jinsi Bwana alivyowasaidia na kuwategemeza. Fikiria kwamba kila wimbi lisilotuzamisha linathibitisha tena uimara wa Mwamba tunayesimama juu yake, ufanisi wa Mlinzi wetu Mkuu wa Maisha.

Sio imani yetu tu inayotuokoa. Kuna hatari ya kutegemea nguvu ya imani yetu, badala ya kumtegemea Bwana Mwenyewe. Ni Kristo anayetuokoa kwa imani. Kristo ndiye mtu mwenye nguvu ambaye imani imeunganishwa naye, na ni Yeye tunayemwamini, na Yeye ndiye anayeokoa. Tunapomtazama Yeye, imani yetu lazima iongezeke. Hivyo, katika maneno ya Isaac Watts:

Iwapo majeshi yote ya kifo,
Na nguvu za jehanamu zisizojulikana,
Zitaweka maumbo yao ya kutisha
Ya hasira na chuki,
Nitakuwa salama, kwa kuwa Kristo anaonyesha
Nguvu kuu na neema ya ulinzi.


Makala haya ni sehemu ya mkusanyiko wa Misingi ya Ufuasi wa Kikristo.

Jeremy Walker
Jeremy Walker
Mch. Jeremy Walker ni mchungaji wa Kanisa la Baptisti la Maidenbower nchini Uingereza. Yeye ni mwandishi wa vitabu kadhaa, ikiwa ni pamoja na Life in Christ: Becoming and Being a Disciple of the Lord Jesus Christ.