Ufuasi katika Familia

16 April 2026

Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kuhusu Utakatifu

30 April 2026

Ufuasi katika Familia

16 April 2026

Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kuhusu Utakatifu

30 April 2026

Mambo 5 Unayopaswa Kujua Kuhusu Kupambana na Dhambi

1. Tishio ni halisi.

Biblia inaweka wazi kwamba tunakabiliwa na majaribu makubwa yanayotokana na dunia, mwili, na shetani. Hao wote ni maadui wakubwa.

Dunia haiko upande wetu. Mfumo wa dunia mara nyingi unanjama ya kutusukuma upande fulani. Hii ndiyo sababu Paulo anawaonya Wakristo wote, “Msifuatishe namna ya dunia hii” (Warumi 12:2). Kuifuatisha dunia katika kile inachokithamini, kile inachoruhusu, na jinsi inavyofafanua mafanikio kunaweza kubadilika kutoka utamaduni mmoja hadi mwingine, lakini lazima kipingwe na kupimwa dhidi ya Maandiko katika kila hatua.

Mwili wetu pia unapigana dhidi yetu. Sisi ni wenye dhambi kwa asili, tumeelekea mbali na Mungu na kuelekea kwa tamaa zetu za dhambi. Wakati mwingine, katika muujiza wa kuzaliwa upya, Mungu kwa neema huondoa baadhi ya mielekeo yetu ya dhambi, lakini mabaki ya maisha yetu ya dhambi hubakia. Hatuwezi tu kuifuata mioyo yetu na kutarajia kwamba itatuongoza katika mwelekeo sahihi.

Kisha kuna shetani. Maandiko yanatuonya kuwa macho, kwa sababu “mshitaki wenu ibilisi huzunguka zunguka kama simba angurumaye, akitafuta mtu wa kummeza” (1 Petro 5:8). Ikiwa muuaji stadi aliajiriwa ili akuuwe, ungelikuwa macho kila wakati. Ungelifunga kila mlango na kuangalia kila kona kama yuko. Shetani ana nguvu zaidi kuliko mwanadamu yeyote. Lazima daima tuwe makini na waangalifu.

2. Majaribu huanza kabla ya wewe kujua.

Wakati tunapoanguka katika dhambi, mara nyingi ni kwa sababu tumeshindwa kujilinda mapema. Hatuwezi kujihusisha katika shughuli zetu za kawaida kana kwamba hatuwezi kushawishiwa na dhambi. Mara nyingi, njia bora ya kupambana na dhambi ni kuepuka maeneo na shughuli zinazotuelekeza kwenye majaribu. Kwa baadhi ya watu, hili linamaanisha kwamba wanahitaji kujishughulisha, kwa kuwa upweke unaoleta kusinywa huwaingiza katika majaribu. Wengine wanahitaji kuepuka watu fulani, ambao ushawishi wao utawaweka kwenye njia ya dhambi. Wengine wanahitaji mifumo ya ulinzi ili kuwaweka mbali na maudhui fulani. Kuna mambo tunajua hatupaswi kamwe kutazama, maeneo ambayo hatupaswi kamwe kwenda, na nyakati ambazo hatupaswi kamwe kuwa peke yetu. Ingawa watu hawa, maeneo, na matukio hayawezi kuwa ni dhambi moja kwa moja, kushirikiana nao au nayo kunaweza kutufanya tuweze kushawishiwa na majaribu na kutuweka katika hatari kubwa ya kuanguka katika dhambi.

3. Mapambano dhidi ya dhambi lazima yashughulike na moyo.

Yesu anaweka wazi kwamba dhambi hutoka ndani (Mathayo 15:19). Mioyo yetu ndio chanzo, na hivyo kupambana na dhambi lazima kushughulike na mtu wa ndani. Ni lazima tuwe waangalifu ili kuikuza mioyo yetu kulingana na Neno la Mungu.

Zaburi 119:11 inaweka hili kwa ufupi:

Nimeliweka neno lako moyoni mwangu,

ili nisikutende dhambi.

Mwandishi wa zaburi alijua kwamba moyo wake unahitaji kufurika Neno la Mungu ili kumwepusha na dhambi. Jambo hilo ni kweli kwetu sote.

Hatuwezi tu kuifuata mioyo yetu na kutarajia kwamba itatuongoza katika mwelekeo sahihi.

Hii ndiyo sababu usomaji wa Biblia wa kila siku, kukariri Biblia, na maombi kulingana na Neno la Mungu ni muhimu sana. Kile tunachofikiria kitaonekana katika maneno na matendo yetu. Kwa kuzingatia hili, Mtume Paulo anaandika, “Hatimaye ndugu, lolote lililo la kweli, lolote lililo la heshima, lolote lililo la haki, lolote lililo safi, lolote lililo la kupendeza, lolote lililo la sifa, ikiwa kuna lolote lenye kustahili sifa, fikirieni mambo haya” (Wafilipi 4:8).

4. Mungu wa Utatu anatuwezesha.

Licha ya majaribu tunayokabiliana nayo kama Wakristo, Bwana yuko upande wetu. Biblia inasema kwamba wale waliozaliwa mara ya pili, “wakiutazama utukufu wa Bwana, wanabadilishwa kuwa mfano huo huo, kutoka utukufu mmoja hadi mwingine. Kwa maana hii inatoka kwa Bwana ambaye ni Roho” (2 Wakorintho 3:18). Wakristo wana ahadi kwamba “yeye aliyeanzisha kazi njema ndani yenu ataikamilisha hata siku ya Kristo Yesu” (Wafilipi 1:6). Na tena, “Ni Mungu afanyaye kazi ndani yenu, kutaka na kutenda kwa ajili ya mapenzi yake mema” (Wafilipi 2:13).

Zaidi ya hayo, tunaambiwa waziwazi:

Hakuna jaribu lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita uwezo wenu, bali pamoja na jaribu hilo pia atatoa na mlango wa kutokea, ili muweze kustahimili. (1 Wakorintho 10:13)

Ambapo maadui tunaokabiliana nao ni wenye nguvu, Mungu ni mwenye nguvu zaidi. Roho wake Mtakatifu —ambaye alimfufua Yesu kutoka kwa wafu—anafanya kazi katika miili yetu leo. Biblia inawakumbusha Wakristo kwamba “yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia” (1 Yohana 4:4).

5. Haifikii kikomo hadi utukufu.

Hadi tuingie katika uwepo wa Mwokozi wetu, tunaweza kutarajia kuwa katika vita dhidi ya dhambi. Biblia inaweka wazi kwamba “tukisema hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe, na kweli haimo ndani yetu” (1 Yohana 1:8).

Vita dhidi ya dhambi inamaanisha kwamba wakati wetu duniani ni wakati wa vita vya kiroho. Kamwe hatupaswi kutarajia kuweza kupumzika hadi tuingie katika pumziko la milele la mbinguni.

Lakini siku moja, tutabadilishwa. Wakati Yesu atakapotukaribisha katika nyumba yetu ya milele, tutakuwa kama Yeye. Vita vitakuwa vimekwisha, na mapambano yatakuwa yameshinda.


Makala haya ni sehemu ya mkusanyiko wa Misingi ya Ufuasi wa Kikristo.

Jonathan L Master

Jonathan L Master

Daktari Jonathan L. Master ni rais Greenville Presbyterian Theological Seminary huko Greenville, South Carolina, na mzee anayefundisha katika Kanisa la Presbyterian nchini Marekani. Yeye ni mwandishi wa vitabu kadhaa, Growing in Grace: Becoming more like Jesus na Reformed Theology: Blessing of the Faith.