
Lengo la Maisha ni Lipi?
22 October 2026Roho Yako hufanyika nini Unapokufa?
Sote tumewahi kufikiria kuhusu hili. Ni nini hutokea punde tu tunapotoa pumzi ya mwisho, moyo unapokoma kudunda, na roho yetu inapoitoka mwili wetu ambao sasa umekufa? Ukweli nausemwe, wengi wetu tuogopa kufa, hata kama hatuogopi kifo. Kufa mara nyingi ni mapambano yenye uchungu. Kufa mara nyingi hutokea katika mazingira tatanishi ya kitabibu, nako kwa kawaida huwa mchakato mbaya. Hata hivyo, kwa kuamini ahadi kwamba kifo humaanisha kuingia katika uzima wa milele mbele ya Bwana, na pia kwa kumtumainia Kristo katika nguvu zake za kuwafufua wafu, Wakristo hawapaswi kuogopa matokeo ya kifo, hata kama wanaweza kuhisi hofu kuhusu mchakato wa kufa.
Hadithi na hekaya kuhusu mauti na kufa zimeenea mno. Hali hii, kwa sehemu, ni kwa sababu Maandiko Matakatifu hayafafanui mchakato wa kufa, ijapokuwa yanazungumza juu ya watu kadhaa waliokufa lakini wakafufuliwa tena na Yesu.Kufa kwa Lazaro huja akilini (Yohana 11), miongoni mwa wengine (kwa mfano, mwana wa mjane wa Naini katika Luka 7:11–17). Lakini hatuna simulizi la moja kwa moja (hata kutoka kwa Lazaro) kuhusu kile watu hawa walikipitia walipokufa. Tunaweza tu kushangaa Lazaro alikuwa akiwaza nini alipokufa mara ya pili, safari hii akiingia katika uzima wa milele. Sasa, tunajua miili yetu ya ufufuo itakuwaje, kwa kuwa Paulo anatupa maelezo ya ajabu ya mabadiliko kamili yatakayotukia Kristo atakaporudi na sisi kufufuliwa katika kutoharibika (1 Wakorintho 15:35–49). Lakini hakuna taarifa nyingi za kibiblia kuhusu hali ya kati—kile kipindi ambacho roho za waamini waliokufa wanasubiri ufufuo wa miili yao na kuondolewa kabisa kwa laana (mauti).
Ni vivyo pia kwamba asili ya swali lenyewe (Hufanyika nini kwa roho zetu tunapokufa?) huwachochea watu kukisia. Nakumbuka bibi yangu aliyemcha Mungu (binti wa mchungaji) akisimulia zamu za kukesha kando ya vitanda vya washirika wa kanisa wanaokaribia kufa. Alieleza jinsi ambavyo kabla ya kutoa pumzi ya mwisho, anayekaribia kufa mara nyingi hufumbua macho, hutazama juu mbinguni, huonyesha aina fulani ya furaha na matarajio, kisha hukubali lisilozuilika. Alisadiki kuwa watakatifu hawa hupewa mwanga mfupi wa kile (au nani) wanachowasubiri. Huenda ikawa hivyo; lakini kwa uwezekano uleule, mwitikio wa kibayokemikali wa ubongo wakati mwili unapozimika unaweza kuzalisha shughuli mbalimbali za kihisia. Simulizi kama hizi, ingawaje za dhati, ni hadithi fupi tu, wala hazitoi msingi wa kujengea mafundisho.
Sote tumesikia hadithi kuhusu wale wanaodaiwa kufa kisha wakarejea katika maisha baada ya mauti. Hadithi kama hizo zinavutia sana, jambo linaloeleza kwa nini kuna kiwanda kidogo cha vitabu kuhusu matukio ya karibu na kifo—vinavyojenga visa vya mwandishi kutembelea mbinguni kibinafsi kabla ya kurejea na kuandika kitabu kuhusu aliyoyapitia. Kwa kawaida, vitabu hivi huonyesha kukutana na wapendwa waliofariki, mara nyingi hujumuisha maelezo ya mbingu (mara nyingi yakiwa ni mandhari ya kidunia yaliyotiwa chumvi); simulizi za kukutana na Yesu, kuzungumza na Mungu; na maelezo kuhusu mambo ya mbinguni.
Lakini masimulizi haya yote yanayooweza kuwa bandia yanakinzana na tunachojua Biblia inasema kuhusu kuingia katika uwepo wa Mungu. Isaya 6:1–7 inatukumbusha. Isaya alishindwa na kutostahili kwake alipopewa maono ya Bwana. Simulizi za Biblia za kukutana na Mungu—kama vile Musa alivyouona kidogo utukufu wa Bwana (Kutoka 33:18–23) au Yesu kujidhihirisha kwa wanafunzi wake wawili njiani kuelekea Emau (Luka 24:37)—huzua hofu kuu, kama si woga wa kutisha, kwa kuwa katika uwepo wa Mungu Mtakatifu. Simulizi za Biblia hazilingani kabisa na hali ya nasibu —au hata hali ya kipuzi ya aina ya fasihi ya “Niliiona mbingu” au “Nilitembea na Yesu.” Kwa kuwa Biblia haifafanui mchakato wala mawazo ya wanaokaribia kufa, wengi wamejitahidi kujaza pengo hilo kwa hadithi za kubuni. Cha kusikitisha, wamefanikiwa sana. Watu wengi huzikubali hekaya hizi kana kwamba ni ukweli.
Kwa shukrani, Biblia hutupatia hoja mbili za marejeleo kuhusu hali za kati zinazotusaidia kujitayarisha kwa kifo. Kwanza, katika vifungu kadhaa vinavyojulikana, Paulo anashughulikia moja kwa moja suala la nini kinawatokea waamini kati ya kufa kwao na kurudi kwa Kristo. Kulingana na Wakorintho wa Pili 5:8, Paulo hufundisha kwamba katika saa ya kifo cha muumini tunaingia mara moja katika uwepo wa Bwana. Mtume anaandika, “Tungependa zaidi kuondoka katika mwili huu na kuwa nyumbani pamoja na Bwana.” Paulo pia aliongea alivyotamani “kuondoka nikakae pamoja na Kristo, jambo hilo ni bora zaidi;” (Wafilipi 1:23). Tunapokufa, mara moja tunakuwa “pamoja na Kristo” na tunaingia katika uwepo wa Mungu. Hili kwa kawaida ndilo tunalomaanisha tunaposema “mbinguni.”
Pili, maono ya mbinguni yaliyoelezwa na Yohana katika Ufunuo 4–6 hutuonyesha kidogo ule uhalisia ambao hapo awali haukuonekana, tutakaouona tunapofariki. Sisi tuliomtumainia Kristo peke yake tutaungana na watakatifu waliokombolewa mbele ya kiti cha enzi cha mbinguni, katika uwepo wa Mungu. Tukiwa na fahamu timamu, tukijua tulipo, na kumsifu Mungu kwa furaha. Kwa kusema kwa uwazi, maono haya ya mbinguni ndiyo taswira iliyo wazi zaidi tuliyonayo ya kile kinachofanyikia roho zetu tunapokufa. Ndani ya sura hizi tatu, Yohana hutoa taswira ya utukufu wa mbinguni, ambako Mungu anakaa miongoni mwa watu wake hadi ufufuo wa miili yetu mwishoni mwa nyakati. Hivi ndivyo mbingu ilivyo—waliokombolewa wakiishi katika uwepo wa Mungu Mtakatifu, wakimpa Muumba na Mkombozi wetu sifa na utukufu wote.
Ingawa mandhari hiyo ni ya ajabu, na kwa namna nyingi yapita ufahamu wetu, yafaa kutambua kwamba watakatifu walioko mbinguni wanalia: “Ee Bwana Mwenyezi, mtakatifu na wa kweli, hata lini huta hukumu na kulipiza kisasi damu yetu juu yao wakaao juu ya nchi?” (Ufunuo 6:10). Wale ambao tayari wako mbele za Mungu, mbele ya kiti chake cha enzi—waliokufa mbele yetu na sasa wako katika hali ya mpito, kipindi kilicho kati ya kifo na kurejea kwa Bwana—wanatamani siku ile ambayo Yesu Kristo atarejea duniani siku ya ufufuo na ya hukumu.
Basi, nini hutokea kwa roho za waamini tunapokufa? Mara moja tunaingia katika uwepo mtukufu wa Bwana, ambako tunasubiri ufufuo wa miili yetu mwisho wa nyakati.
Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.


