Toba Inaonekanaje?
19 Juni 2025
Yesu Kristo: Mwanakondoo wa Mungu
20 Juni 2025
Toba Inaonekanaje?
19 Juni 2025
Yesu Kristo: Mwanakondoo wa Mungu
20 Juni 2025

Tunamaanisha Nini Tunapozungumzia “Utakatifu wa Maisha ya mwanadamu”?

xr:d:DAFXk0WDSFg:25,j:45162075609,t:23011320

Katika kauli ya kibiblia, utakatifu wa maisha ya binadamu umejikita na kuimarishwa katika uumbaji. Binadamu haonekani kama ajali ya ulimwengu bali kama matokeo ya uumbaji uliofanywa kwa uangalifu na Mungu wa milele. Utu wa binadamu unatokana kwa Mungu. Mwanadamu kama kiumbe mwenye kikomo, na mtegemezi, amepewa thamani kubwa na Muumba wake.

Maelezo ya uumbaji katika Mwanzo yanatoa mfumo wa utu wa binadamu:

Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu. wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.’ Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,kwa mfano wa Mungu alimuumba;mwanaume na mwanamke aliwaumba.” (Mwa. 1:26–27)

Kuumbwa kwa mfano wa Mungu ndiko kunakowatofautisha wanadamu na viumbe wengine wote. Muhuri wa sura na mfano wa Mungu unamuunganisha Mungu na wanadamu kwa njia ya kipekee. Ingawa hakuna hati ya kibiblia ya kumwona mwanadamu kama mungu, kuna heshima ya juu inayohusishwa na uhusiano huu wa kipekee na Muumba.

Mwanadamu huenda akawa si safi tena, lakini bado ni mwanadamu. Kwa kadiri tulivyo binadamu, kwa maana pana, tunabakia na sura ya Mungu. Sisi bado ni viumbe wenye thamani. Huenda hatustahili tena, lakini bado tuna thamani. Huu ni ujumbe wa Biblia wa ukombozi unaosikika kwa nguvu. Viumbe ambao Mungu aliwamba ni viumbe walewale ambao ameguswa ili kuwakomboa.

Vifungu vingi vya Agano la Kale vinazungumzia utu wa maisha ya binadamu kama unavyotokana na uumbaji wa kiungu, vikiwemo vifuatazo:

“Roho wa Mungu ameniumba,
na pumzi ya Mwenyezi hunipa uhai.” (Ayubu 33:4)

Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu.
Yeye ndiye alituumba; sisi tu mali yake; sisi tu watu wake, kondoo wa malisho yake.” (Zaburi 100:3)

Ole wake yeye ashindanaye na Muumba wake,
yeye ambaye ni kigae tu kati ya vigae juu ya ardhi!
Je, udongo wa kufinyangia humwambia mfinyanzi,‘Unatengeneza nini wewe?’Je,kazi yako husema, ‘Haina mikono’?
Ole wake amwambiaye baba yake,‘Umezaa nini?’
Au kumwambia mama yake,‘Umezaa kitu gani?’
“Hili ndilo asemalo Bwana,yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na Muumba wake:
Kuhusu mambo yatakayokuja;
je, unaniuliza habari za watoto wangu,au kunipa amri kuhusu kazi za mikono yangu?
Mimi ndiye niliyeumba dunia na kumuumba mwanadamu juu yake;
Mikono yangu mwenyewe ndiyo iliyozitanda mbingu,
nikayapanga majeshi yake yote ya angani.” (Isaya 45:9–12)

“Lakini, Ee Bwana, wewe ndiwe Baba yetu.;
Sisi ni udongo, wewe ndiye mfinyanzi;
sisi sote tu kazi ya mkono wako.” (Isa. 64:8)

Inavutia kwamba Yesu Kristo alitoa maelezo muhimu zaidi ya mtazamo wa Agano la Kale kuhusu utakatifu wa maisha:

“Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue. Yeyote atakayeua atapaswa hukumu.’ Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote atakayemkasirikia ndugu yake, atapaswa hukumu. Tena, yeyote atakayemwambia ndugu yake, ‘Raka’ atapaswa kujibu kwa Baraza la Wayahudi. Lakini yeyote atakayesema ‘Wewe mpumbavu!’ atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu.” (Mathayo 5:21–22)

Maneno ya Yesu yana umuhimu mkubwa kwa uelewa wetu wa utakatifu wa maisha. Hapa Yesu alipanua maana ya sheria ya Agano la Kale. Alikuwa akizungumza na viongozi wa kidini ambao walikuwa na uelewa finyu na wa kawaida wa Amri Kumi. Wale walioshikilia sana sheria katika siku Zake walikuwa na uhakika kwamba ikiwa wangetii vipengele vya sheria vilivyoelezwa waziwazi, wangejipongeza wenyewe kwa kuwa na maadili ya hali ya juu. Walishindwa, hata hivyo, kuelewa athari pana zaidi. Kwa mtazamo wa Yesu, kile ambacho sheria haikukieleza kwa undani kilikuwa kimedokezewa waziwazi na maana yake pana.

Sifa hii ya sheria inaonekana katika jinsi Yesu alivyofafanua kuhusu marufuku dhidi ya uzinzi:

“Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini.’ Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.” (Mathayo 5:27–28)

Hapa Yesu alieleza kwamba mtu anayejizuia kufanya tendo la uzinzi si lazima awe ameitii sheria yote. Sheria kuhusu uzinzi ni ngumu, ikijumuisha sio tu kitendo halisi cha ngono haramu bali pia kila kitu kinachotokea kati ya kutamani na uzinzi. Yesu alielezea kutamani kama uzinzi wa moyo.

Sheria haikatazi tu tabia na mitazamo fulani hasi, bali kwa maana nyingine inahitaji tabia na mitazamo fulani chanya. Yaani, ikiwa uzinzi umekatazwa, basi usafi wa mwili na utakaso vinahitajika.

Wakati tunapotumia mifumo hii iliyowekwa na Yesu juu ya marufuku dhidi ya mauaji, tunaelewa wazi kwamba, kwa upande mmoja, tunapaswa kujiepusha na mambo yote yaliyomo katika ufafanuzi mpana wa mauaji, lakini kwa upande mwingine, tunaamriwa kwa dhati kufanya kazi ya kuokoa, kuboresha, na kutunza maisha. Tunapaswa kuepuka mauaji katika nyanja zake zote na, wakati huo huo, tufanye yote tuwezayo kuendeleza maisha.

Kama vile Yesu alivyozingatia kutamani kuwa sehemu ya uzinzi, ndivyo Alivyotazama hasira isiyo na sababu na kashfa kama sehemu za mauaji. Kama kutamani ni uzinzi wa moyo, vivyo hivyo hasira na kashfa ni mauaji ya moyoni.

Kwa kupanua wigo wa Amri Kumi hadi kujumuisha mambo kama kutamani na kashfa, Yesu hakumaanisha kwamba kutamani mtu ni uovu sawasawa na kufanya uasherati. Vivyo hivyo, Yesu hakusema kwamba kashfa ni uovu kama mauaji. Alichosema ni kwamba sheria dhidi ya mauaji inajumuisha sheria dhidi ya chochote kinachohusisha kumjeruhi binadamu mwenzako bila haki.

Je, yote haya yanahusiana vipi na suala la utoaji mimba? Katika mafundisho ya Yesu tunaona uthibitisho mwingine wenye nguvu wa utakatifu wa maisha. Mauaji ya moyoni, kama vile kashfa, yanaweza kuelezewa kama uuaji  “unaoweza” kutokea. Ni mauaji yanayoweza kutokea kwa sababu, mfano, hasira na kashfa yana uwezo wa kusababisha tendo kamili la mauaji ya kimwili. Bila shaka, hayasababishi matokeo hayo kila wakati. Hasira na kashfa vimekatazwa, siyo sana kwa sababu ya kile kingine ambacho yanaweza kusababisha, bali kwa sababu ya madhara halisi yanayofanya kwa ubora wa maisha.

Tunapounganisha mjadala wa utakatifu wa maisha na suala la utoaji mimba, tunafanya uhusiano wa jambo lililo gumu kueleza lakini muhimu. Hata kama haiwezi kuthibitishwa kwamba kijusi ni mtu halisi anayeishi, hakuna shaka kwamba ni mtu mwenye uwezo wa kuishi. Kwa maneno mengine, kijusi ni mtu anayekua. Hayuko katika hali ya kuganda. kijusi yuko katika mchakato wa mabadiliko—bila kuingiliwa au bila janga lisilotarajiwa, hakika atakuwa mtu hai kamili.

Yesu Kristo anaona sheria dhidi ya mauaji ikijumuisha sio tu kitendo halisi cha mauaji, bali pia vitendo vya uuaji vinavyoweza kutokea. Yesu alifundisha kwamba ni kinyume cha sheria kuwa na uwezekano wa kitendo cha mauaji ya maisha halisi. Je, basi, ni athari gani za kufanya uharibifu halisi wa uhai unaoweza kuwa?

Uharibifu halisi wa uhai unaoweza kuwa si sawa na uwezekano wa uharibifu wa maisha halisi. Hivi si visa vinavyofanana, lakini vinakaribiana vya kutosha kutufanya tusite na kuzingatia kwa makini matokeo yanayoweza kutokea kabla ya kuharibu uhai unaoweza kuwa. Kama kipengele hiki cha sheria hatimaye hakikuelezea kwa kikamilifu suala la utoaji mimba ndani ya marufuku pana na tata dhidi ya uuaji, basi kipengele cha pili bila shaka hufanya hivyo.”

Marufuku hasi ya sheria humaanisha mitazamo na vitendo chanya. Kwa mfano, sheria ya kibiblia dhidi ya uzinzi pia inahitaji usafi na utakatifu. Vivyo hivyo, sheria inapowekwa katika mfumo chanya, kinyume chake hasi kinakatazwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Kwa mfano, ikiwa Mungu anatuamuru kuwa wasimamizi wazuri wa pesa zetu, ni wazi hatupaswi kuwa watumiaji wa ovyo. Amri chanya ya kufanya kazi kwa bidii ina maana ya marufuku ya kutozembea kazini.

Marufuku hasi dhidi ya mauaji halisi na yanayoweza kutokea yanahusisha kimya kimya agizo chanya la kufanya kazi kwa ajili ya ulinzi na ustawi wa maisha. Kupinga mauaji ni kuendeleza maisha. Lolote jingine ambalo utoaji mimba hufanya, hauendelezi maisha ya mtoto ambaye hajazaliwa. Ingawa baadhi ya watu wanatoa hoja kwamba utoaji mimba unakuza ubora wa maisha ya wale ambao hawataki watoto, hauendelezi maisha ya mhusika anayezungumziwa, mtoto ambaye anakua na hajazaliwa.

Biblia inaunga mkono kwa dhati thamani kubwa sana ya maisha yote ya binadamu. Maskini, waliodhulumiwa, wajane, yatima, na walemavu—wote wanathaminiwa sana katika Biblia. Hivyo, mjadala wowote kuhusu suala la utoaji mimba hatimaye lazima ushughulike na mada hii kuu ya Maandiko. Wakati uharibifu au utupaji wa hata maisha ya binadamu yanayoweza kuwa unafanywa kwa urahisi na kwa bei nafuu, kivuli kinatia giza mandhari yote ya utakatifu wa maisha na utu wa binadamu.


Dondoo hii imetoholewa kutoka katika Abortion: A Rational Look at an Emotional Issuea na R.C. Sproul.

Makala haya yalichapishwa kwanza katika Blogu ya Huduma za Ligonier.

R.C. Sproul
R.C. Sproul
Dkt. R.C. Sproul alikuwa mwanzilishi wa Ligonier Ministries, mchungaji wa kwanza wa mahubiri na mafundisho katika Saint Andrew’s Chapel huko Sanford, Fla., rais wa kwanza wa Reformation Bible College, na mhariri mtendaji wa gazeti la Tabletalk. Kipindi chake cha redio, Renewing Your Mind, bado kinapeperushwa kila siku katika mamia ya stesheni za redio ulimwenguni na kinaweza kusikilizwa mtandaoni pia. Alikuwa mwandishi wa vitabu zaidi ya mia moja, vikiwemo The Holiness of God, na Everyone’s a Theologian. Alijulikana ulimwenguni kote kwa utetezi wake mahiri wa Kutokukosea kwa Maandiko na uhitaji wa watu wa Mungu kusimama na ukweli wa Neno lake.