
Tunamaanisha Nini Tunapozungumzia “Utakatifu wa Maisha ya mwanadamu”?
20 Juni 2025
Kusudi la Mungu Msalabani lilikuwa ni nini?
20 Juni 2025Yesu Kristo: Mwanakondoo wa Mungu

Wazo hili la Mwanakondoo wa Mungu ni mfululizo unaoendelea katika historia ya ukombozi. Linaweza kurudi nyuma hadi Mwanzo 22, wakati Mungu alipomwita Ibrahimu aende Mlima Moria na kumtoa mwanawe Isaka kama sadaka. Ibrahimu, kwa utiifu kwa Mungu, alikuwa tayari kufanya hivyo, lakini wakati wa mwisho kabisa, baada ya Ibrahimu kumfunga Isaka kwenye madhabahu na alikuwa akijiandaa kuchoma kisu moyo wake, Mungu alimzuia, akisema, “Usimdhuru kijana, wala usimtendee jambo lolote. Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwa sababu hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee” (mstari wa 12). Kisha kukawa na kelele nyuma ya Ibrahimu, naye akageuka na kumwona kondoo dume aliyenaswa kwenye kichaka kwa pembe zake. Mungu alitoa mwana-kondoo kama dhabihu mbadala kwa mwana wa Ibrahimu. Kwa kweli, haijasemwa kamwe katika Mwanzo 22 kwamba kondoo dume ambaye Ibrahimu alimkamata na kumtoa mahali pa Isaka alikuwa dhabihu ya upatanisho. Hata hivyo, ilikuwa ni dhabihu mbadala, na hiyo ndiyo dhana inayosimamia upatanisho wa Kristo. Yesu anatenda kwa niaba yetu, na Mungu anammiminia ghadhabu Yake kwa sababu ya dhambi zetu badala ya kutumiminia sisi. Halafu Mungu anamtoa Mwanakondoo wake mwenyewe na anakubali maisha yake mbadala.
Mungu anamimina ghadhabu yake kwa sababu ya dhambi zetu kwa Yesu badala yetu.
Vivyo hivyo, Mwanakondoo wa Mungu hakika ameonyeshwa awali katika Pasaka. Wakati Mungu alipojiandaa kuleta pigo lake la mwisho kwa Wamisri, kifo cha kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Wamisri, ikiwa ni pamoja na mwana wa kifalme wa Farao, aliwaagiza watu wake Israeli kuchinja wana-kondoo wasio na dosari na kupaka damu kwenye miimo ya milango yao. Mungu aliahidi kupita juu ya nyumba zote ambapo aliona damu ya wana-kondoo kwenye miimo ya milango (Kutoka 12:3–13). Kama vile damu ya wale wana-kondoo ilivyowafanya watu wa Israeli kuokolewa kutoka katika ghadhabu ya Mungu, Mwanakondoo wa Mungu aliwakomboa watu wake kutoka kwenye adhabu iliyostahili kwa dhambi zao.
Kwa kuzingatia taswira hii katika Mwanzo 22, Kutoka 12, na vifungu vingine katika Agano la Kale, ni upumbavu kusema kwamba jina “Mwanakondoo wa Mungu” ni uvumbuzi wa mtume Yohana. Maneno ya Yohana Mbatizaji yaliongozwa na ufahamu wake wa Agano la Kale, Maandiko Matakatifu ya Wayahudi wakati wa Kristo.
Licha ya matumizi mengi ya majina muhimu ya Yesu katika sura ya kwanza ya Yohana—”Mwanakondoo wa Mungu,” “Mwana wa Mungu,” “Masihi,” “Mwana wa Adamu,” na kadhalika—sidhani kwamba Yohana Mbatizaji, Andrea, Nathanaeli, au yeyote kati ya wanafunzi walikuwa na uelewa kamili wa maana ya majina haya. Yohana Mbatizaji, ambaye hapa alisema, “Tazama! Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu!” baadaye alitupwa gerezani na akatuma wajumbe kwa Yesu, akiuliza, Je, Wewe ndiye Yule Ajaye, au tumtazamie mwingine? (Luka 7:20). Swali hili linaonyesha kwamba Yohana hakuwa amefahamu kikamilifu utambulisho wa Yesu, licha ya ushuhuda wake wa kusisimua kuhusu utambulisho wa Yesu. Tatizo lilikuwa kwamba alikuwa na matarajio yake mwenyewe. Alitarajia kwamba Mwanakondoo wa Mungu angekuja na kuwafukuza Warumi, kama vile watu wengine wote walivyotarajia. Alipomwona Yesu akizunguka akihubiri tu, alichanganyikiwa.
Mwanakondoo wa Mungu aliwakomboa watu Wake kutoka kwenye adhabu waliyostahili kwa dhambi zao.
Yesu aliwaambia wajumbe wa Yohana, “Rudini mkamwambie Yohana yote mnayoyaona na kuyasikia: Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa habari njema” (Luka 7:22). Yesu aliashiria miujiza Yake ili kuthibitisha utambulisho Wake kwa Yohana aliyekuwa na shaka. Alirejelea pia unabii wa kimasihi katika Isaya 61:1–2a, ambao unasema:
“Roho wa Bwana Mwenyezi yu juu yangu
kwa sababu Bwana amenitia mafuta
Kuwahubiria maskini habari njema;
Amenituma kuwaganga waliovunjika moyo,
na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao,
kuwatangazia mateka uhuru wao;
kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”
Ilikuwa kana kwamba Yesu alikuwa akisema: “Yohana, kama ungekuwa umeisoma Biblia yako vizuri, usingeuliza kama Mimi ndiye Yule aliyepaswa kuja.” Huna haja ya kumtafuta mwingine. Ulikuwa sahihi mara ya kwanza. Mimi ni “Mwanakondoo wa Mungu”.
Petro pia alikuwa amechanganyikiwa, hata alipokuwa ametoa ungamo lake kuu huko Kaisaria Filipi. Katika kujibu swali la Yesu wanafunzi walidhani kwamba Yeye ni nani, Petro alisema, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai” (Mathayo 16:16). Yesu alithibitisha kwamba ungamo hilo lilikuwa sahihi na akamtangaza Petro kuwa “amebarikiwa” kwa kuelewa Yeye ni nani. Lakini mara baada ya hayo, Yesu alipowaambia wanafunzi Wake kwamba alikuwa anaelekea Yerusalemu kuteseka na kufa, Petro alimkemea na kusema, “Hili halitakutokea Wewe!” (16:22b). Dakika moja Petro alithibitisha kwamba Yesu alikuwa Masihi, lakini dakika iliyofuata alionyesha kwamba hakuelewa maana kamili ya Yesu kuwa Masihi.
Sisi, bila shaka, tunakabiliwa na mkanganyiko huo huo. Ni pale tu tunapoitazama picha nzima, tukizingatia msalaba, ufufuo, kupaa, na kumiminwa kwa Roho Siku ya Pentekoste, ndipo tunapoanza kuona kina na utajiri wa yote ambayo Mungu alikuwa akiwasilisha kupitia tangazo la mjumbe wake, aliyesema, “Tazama! Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu!”
Chapisho hili ni dondoo kutoka kwenye maoni ya R.C. Sproul kumhusu Yohana
Makala haya yalichapishwa kwanza katika Blogu ya Huduma za Ligonier.