
Vyanzo vya Theolojia ya Kimfumo
23 Juni 2025
Injili Inamaanisha Nini?
23 Juni 2025John Calvin kuhusu Umuhimu wa Kufanya Mageuzo ya Kanisa

Zaidi ya miaka 450 iliyopita, ombi lilimjia John Calvin kuandika kuhusu tabia na haja ya mageuzi katika Kanisa. Hali zilikuwa tofauti kabisa na zile zilizochochea maandiko mengine ya Calvin, na zinatuwezesha kuona vipengele vingine vya utetezi wake wa mageuzo. Mfalme Charles V alikuwa anaalika Bunge la Dola Takatifu la Kirumi kukutana katika mji wa Speyer mwaka 1544. Martin Bucer, mwanamageuzi mkuu wa Strassburg, alimwomba Calvin aandike tamko la mafundisho na umuhimu wa mageuzo. Matokeo yalikuwa ya kushangaza. Theodore Beza, rafiki na mrithi wa Calvin huko Geneva, aliiita “Umuhimu wa Kufanya Mageuzo ya Kanisa” kazi yenye nguvu zaidi ya wakati wake.
Calvin anapanga kazi hiyo katika sehemu tatu kubwa. Sehemu ya kwanza imejihusisha na maovu katika kanisa ambayo yalihitaji mageuzi. Ya pili inaeleza kwa undani tiba maalum kwa maovu hayo yaliyopitishwa na wanamageuzi. Ya tatu inaonyesha kwa nini mageuzo hayangeweza kucheleweshwa, bali jinsi hali ilivyohitaji “marekebisho ya haraka.”
Katika kila moja ya sehemu hizi tatu, Calvin anazingatia mada nne, ambazo anaziita roho na mwili wa kanisa. Roho ya kanisa ni ibada na wokovu. Mwili ni sakramenti na utawala wa kanisa. Sababu kuu ya mageuzo kwa Calvin inazingatia mada hizi. Maovu, tiba na umuhimu wa kuchukua hatua za haraka yote yanahusiana na ibada, wokovu, sakramenti na utawala wa kanisa.
Sababu kuu ya mageuzo kwa Calvin inazingatia mada hizi. Umuhimu wa mada hizi kwa Calvin unaangaziwa tunapokumbuka kwamba hakuwa anajibu mashambulizi katika maeneo haya manne, bali alizichagua mwenyewe kama vipengele muhimu zaidi vya mageuzo. Ibada sahihi ni jambo la kwanza analoshughulikia Calvin.
Ibada
Calvin anasisitiza umuhimu wa ibada kwa sababu wanadamu kwa urahisi huabudu kulingana na hekima yao wenyewe badala ya kwa hekima ya Mungu. Anasisitiza kwamba ibada lazima idhibitiwe na Neno la Mungu pekee: “Ninajua jinsi ilivyo vigumu kuishawishi dunia kwamba Mungu hapendezwi na aina zote za ibada ambazo hazijaidhinishwa na Neno Lake. Msimamo wa kinyume ambao unashikamana nao, ukiwa umeketi ndani ya mifupa na uroto wao, ni kwamba chochote wanachofanya kina idhini ya kutosha ndani yake, mradi tu kinaonyesha aina fulani ya ari ya utukufu wa Mungu. Lakini kwa kuwa Mungu haioni tu ikiwa haina matunda, bali pia anachukia waziwazi, chochote tufanyacho kwa ari ya ibada, ikiwa inapingana na amri Yake, tunafaidika na nini kwa kuwa kinyume nayo? Maneno ya Mungu ni wazi na dhahiri, ‘Kutii ni bora kuliko dhabihu.’ Imani hii ni mojawapo ya sababu ambazo mageuzo yalihitajika: “. . . kwa kuwa . . . Mungu katika vifungu vingi anakataza ibada yoyote mpya isiyoidhinishwa na Neno lake; kwa kuwa anatangaza kuwa anakasirishwa sana na dhana inayobuni ibada kama hiyo, na kuitishia na adhabu kali, ni wazi kwamba mageuzo ambayo tumeanzisha yalihitajika kwa umuhimu mkubwa.” Kwa kiwango cha Neno la Mungu, Calvin anahitimisha kuhusu Kanisa Katoliki la Kirumi kwamba “umbo zima la ibada ya kiungu inayotumika kwa ujumla siku hizi si chochote ila ufisadi mtupu.”
Kwa Calvin, ibada ya kanisa la enzi za kati ilikuwa “ibada mbaya ya sanamu.” Suala la ibada ya sanamu lilikuwa kwake zito kama suala la haki ya matendo katika kuhesabiwa haki. Yote mawili yalionyesha hekima ya kibinadamu ikichukua nafasi ya ufunuo wa kiungu. Yote mawili yalionyesha kujipendekeza kwa mwelekeo wa kibinadamu, badala ya kutaka kumpendeza na kumtii Mungu. Calvin anasisitiza kwamba hakuna umoja unaoweza kuwepo katika ibada na waabudu sanamu: “Lakini itasemwa kwamba, ingawa manabii na mitume walijitenga na makuhani waovu katika mafundisho, bado walikuza ushirika nao katika dhabihu na maombi. Ninakubali walifanya, mradi kwamba hawakulazimishwa kuabudu sanamu. Lakini ni yupi kati ya manabii tunayesoma kumhusu ambaye aliwahi kutoa dhabihu huko Betheli?”
Wanamageuzi, kama manabii wa zamani, walihitaji kushambulia ibada ya sanamu na “maonyesho ya nje” ya ibada ya wakati wao. Dawa dhidi ya saraksi ya kanisa katika siku za Calvin ilikuwa ni urahisi wa kiungu wa kuabudu — kama inavyoonekana katika mpangilio wa ibada katika kanisa la Geneva. Urahisi huo uliwatia moyo waabuduo kuabudu kwa akili na mwili. “Kwa muda ni wajibu wa waabuduo kwa kweli kuabudu kwa moyo na akili, watu daima wanatamani kubuni njia ya kumtumikia Mungu kwa namna tofauti kabisa, lengo lao likiwa ni kumfanyia ibada fulani za kimwili, na akili zao kutokuweko.”
Kuhesabiwa haki
Calvin sasa anageukia mada ya kuhesabiwa haki. Hapa anakubali kwamba kutokubaliana kumekuwa kwa ukali mkubwa zaidi: “Hakuna jambo ambalo linapingwa kwa nguvu zaidi, hakuna ambalo wapinzani wetu wanapinga kwa ukaidi zaidi, kuliko lile la kuhesabiwa haki, yaani, kama tunakupata kwa imani au kwa matendo.” “Usalama wa Kanisa” unategemea fundisho hili na kwa sababu ya makosa kuhusu fundisho hili kanisa limepata “jeraha la mauti” na “limefikishwa kwenye ukingo wa maangamizi.”
Calvin anasisitiza kwamba Kuhesabiwa Haki ni kwa imani pekee: “… tunadumisha, kwamba haijalishi matendo ya mtu yeyote ni ya aina gani, anachukuliwa kuwa mwenye haki mbele za Mungu, kwa msingi wa rehema ya bure; kwa sababu Mungu, bila kujali matendo, anamchukua bure katika Kristo, kwa kumhesabia haki ya Kristo kwake, kana kwamba ni yake mwenyewe.”
Mafundisho haya yana athari kubwa katika maisha na hali ya Mkristo: “. . . kwa kumshawishi mwanadamu juu ya umaskini wake na kutokuwa na uwezo, tunamfundisha kwa ufanisi zaidi unyenyekevu wa kweli, kumwongoza kuacha kujiamini, na kujikabidhi kikamilifu kwa Mungu; na kwa njia hiyo hiyo, tunamfundisha kwa ufanisi zaidi shukrani, kwa kumwongoza kuhusisha, kama inavyopaswa kweli, kila kitu kizuri alicho nacho kwa wema wa Mungu.”
Sakramenti
Mada ya tatu ya Calvin ni sakramenti ambazo anazichunguza kwa kina. Analalamika kwamba “. . . sherehe zilizopangwa na mwanadamu ziliwekwa katika daraja moja na mafumbo yaliyoanzishwa na Kristo” na kwamba Meza ya Bwana hasa ilikuwa imegeuzwa kuwa “maonyesho ya sarakasi.” Matumizi hayo mabaya ya sakramenti za Mungu hayawezi kuvumiliwa. Jambo la kwanza tunalolalamikia hapa ni kwamba, watu wanaburudishwa na sherehe za kuvutia, kukiwa hakuna neno linalosemwa kuhusu maana na ukweli wake. Kwa maana hakuna faida katika sakramenti isipokuwa kitu ambacho kinaashiriwa wazi kinaelezewa kwa mujibu wa Neno la Mungu.”
Calvin analalamika kwamba urahisi wa mafundisho na utekelezaji wa sakramenti yaliyokuwepo katika kanisa la awali umepotea. Hili linaonekana wazi zaidi katika Meza ya Bwana. Sadaka ya Ekaristi, ubadilishaji damu na ibada ya mkate na divai iliyowekwa wakfu si ya kibiblia na inaharibu maana halisi ya sakramenti. “Wakati sakramenti ilipopaswa kuwa njia ya kuinua akili za wacha Mungu kuelekea mbinguni, alama takatifu za Meza ya Bwana zilitumiwa vibaya kwa kusudi tofauti kabisa, na watu, wakiridhika na kuzitazama na kuzisujudia, hawakuwahi kumfikiria Kristo.” Kazi ya Kristo imeharibiwa, kama inavyoonekana katika wazo la dhabihu ya ekaristi, ambapo “. . . Kristo alitolewa dhabihu mara elfu moja kwa siku, kana kwamba hakufanya vya kutosha kwa kufa mara moja kwa ajili yetu.”
Maana ya kweli ya Karamu imeelezwa kwa ufupi na Calvin kwa urahisi: “. . . tunawahimiza nyote mje kwa imani . . . . tunahubiri kwamba mwili na damu ya Kristo vyote vinatolewa kwetu na Bwana katika Karamu; na kupokelewa na sisi. Wala hatufundishi hivyo kwamba mkate na divai ni ishara, bila kuongeza mara moja kwamba kuna ukweli ambao umeunganishwa nazo, na ambazo zinaziwakilisha.” Kristo kwa kweli anajitoa Mwenyewe na faida zote za wokovu kwa wale wanaoshiriki katika Meza ya Bwana kwa imani.
Muhtasari huu wa majadiliano ya Calvin kuhusu sakramenti unatupa tu ladha ya jinsi alivyoshughulikia mada hii muhimu. Azigatia umakini mkubwa ubatizo pamoja na kupinga msimamo wa Kirumi kwamba kuna sakramenti tano za ziada.
Utawala wa Kanisa
Hatimaye Calvin anageukia mada ya utawala wa kanisa. Anabainisha kuwa hii ni mada kubwa sana: “Kama ningepitia makosa ya utawala wa kanisa kwa undani, nisingevifanya kamwe.” Anazingatia umuhimu wa ofisi ya uchungaji. Heshima na wajibu wa kufundisha uko katika moyo wa ofisi hii: “. . . hakuna mtu aliye mchungaji wa kweli wa kanisa ambaye hatimizi jukumu la kufundisha.” Moja ya mafanikio makubwa ya Mageuzo ni urejeshaji wa mahubiri katika nafasi yake sahihi katika maisha ya watu wa Mungu. “. . . hakuna kanisa letu lolote linaloonekana bila mahubiri ya kawaida ya Neno.” Ofisi ya uchungaji lazima iunganishe utakatifu na mafundisho: “. . . wale wanaoongoza Kanisani wanapaswa kuwazidi wengine, na kung’aa kwa mfano wa maisha matakatifu zaidi. . . .”
Calvin analalamika kwamba badala ya kufundisha na kufuata utakatifu, uongozi katika kanisa la Kirumi unatekeleza “dhuluma ya kikatili zaidi” juu ya roho za watu wa Mungu, ukidai mamlaka na uwezo ambao hawakupewa na Mungu. Mageuzo yalileta uhuru wa ajabu kutoka katika mila zisizo za kibiblia ambazo zilikuwa zimelifunga kanisa. “Kama ilivyokuwa, kwa hivyo, ilikuwa ni wajibu wetu kuzikomboa dhamiri za waumini kutoka kwenye utumwa usiofaa ambamo walishikiliwa, kwa hivyo tumefundisha kwamba wako huru na hawajafungwa na sheria za kibinadamu, na kwamba uhuru huu, ambao ulinuniliwa kwa damu ya Kristo, hauwezi kuvunjwa.”
Kanisa la Kirumi lilitilia mkazo sana urithi wake wa kitume, hasa kwa ajili ya kuwekwa wakfu. Calvin anasisitiza kwamba mageuzo ya kuwekwa wakfu yanafuata mafundisho na utaratibu halisi wa Kristo, mitume na kanisa la kale. Anasema, “Kwa hiyo, hakuna mtu anayeweza kudai haki ya kuweka wakfu, ambaye haifadhi umoja wa kanisa kwa usafi wa mafundisho.”
Mageuzo
Calvin anahitimisha risala hii kwa tafakari juu ya mchakato wa mageuzo. Anauhusisha mwanzo na Luther ambaye kwa “mkono mpole” alitoa mwito wa mageuzo. Jawabu kutoka Roma lilikuwa juhudi “la kukandamiza ukweli kwa vurugu na ukatili.” Vita hivi havikumshangaza Calvin kwa kuwa ‘. . . hatima ya kawaida ya Injili, tangu mwanzo wake, imekuwa na daima itakuwa hadi mwisho, kuhubiriwa ulimwenguni katikati ya mashindano makali.”
Calvin anahalalisha shida hii katika maisha ya kanisa kwa sababu ya umuhimu wa masuala yanayobishaniwa. Hakuruhusu kupunguzwa kwa ukweli kwamba “kiini chote cha dini ya Kikristo” kiko hatarini. Kwa kuwa wanamageuzi walitenda kwa utiifu wa Biblia, anakataa pendekezo lolote kwamba wao ni waasi: “… jambo la muhimu la kuzingatia, kwanza kabisa, ni, kuwa makini na kutenganisha Kanisa na Kristo ambaye ni kichwa chake. Ninaposema Kristo, ninajumuisha mafundisho ya injili Yake, ambayo aliyatia muhuri kwa damu Yake. . . Kwa hiyo, na iwe ni jambo thabiti, kwamba umoja mtakatifu upo miongoni mwetu, tunapokubaliana katika mafundisho safi, tumeunganishwa katika Kristo pekee.” Si jina kanisa linaloleta umoja, bali ni uhalisi wa kanisa la kweli ambalo hukaa katika Neno la Mungu.
Kisha Calvin anageukia swali la utendaji la ni nani angeweza kuongoza vyema juhudi za mageuzo katika kanisa. Anakataa wazo kwamba papa anaweza kuongoza kanisa au mageuzo kwa lugha kali zaidi: “Ninakataa mamlaka hayo kuwa ya Kitume, ambapo hakuna kinachoonekana isipokuwa uasi wa kutisha—Ninakataa yeye kuwa mwakilishi wa Kristo, ambaye, kwa kupinga injili kwa nguvu, anaonyesha kwa matendo yake kwamba yeye ni Mpinga Kristo—Ninakataa yeye kuwa mrithi wa Petro, ambaye anafanya kila awezalo kubomoa kila jengo ambalo Petro alijenga na ninakataa yeye kuwa mkuu wa Kanisa, ambaye kwa udhalimu wake analirarua na kuligawanya Kanisa, baada ya kulitenganisha na Kristo, aliye Kiongozi wake wa kweli na wa pekee.” Anajua kwamba wengi wanataka baraza la ulimwengu ili kutatua matatizo ya kanisa, lakini anaogopa kwamba baraza kama hilo haliwezi kukutana na kwamba likikutana, litadhibitiwa na papa. Anapendekeza kwamba kanisa lifuate desturi ya kanisa la kale na kutatua masuala katika mabaraza mbalimbali ya ndani au ya majimbo. Kwa hali yoyote lazima shughuli hii hatimaye aachiwe Mungu ambaye atatoa baraka anazoona zinafaa kwa juhudi zote za mageuzo: “Kwa kweli, tunatamani, kama tunavyopaswa, kwamba huduma yetu iwe na manufaa kwa ulimwengu; lakini kuwa na matokeo haya ni jukumu la Mungu, si letu.”
Chapisho hili lilichapishwa awali na Dkt. W. Robert Godfrey hapa.
Makala haya yalichapishwa kwanza katika Blogu ya Huduma za Ligonier.