
Kazi ya Mchungaji ni Nini?
3 November 2026Nadharia Tisini na Tano zilikuwa nini?
Mnamo tarehe 31 Oktoba 1517, Martin Luther, wakati huo akiwa na umri wa kati ya miaka ya thelathini, alikwenda katika Kanisa la Kasri huko Wittenberg na akabandika Nadharia zake Tisini na Tano kwenye mlango wa kanisa. Hapo mwanzo, Nadharia hizo zilibuniwa kama hoja za mjadala wa hadharani; ziliandikwa kwa Kilatini—lugha ya wanazuoni, wala si ya mitaani. Luther hakujua kujua kwamba yale yangevuma kote Ulaya na kuwa kichocheo cha mapinduzi ya kiroho.
Wengi wa wale walioziona nyaraka zilizobandikwa kwenye mlango wa Kanisa la Kasri—ambao unaonekana ulitumika kama ubao wa matangazo ya umma—wasingeweza kusoma Kilatini. Lakini si muda mrefu nadharia hizo zilitafsiriwa kwa Kijerumani, kisha zikaenea Ulaya yote kama moto wa nyika—naam, kama “matendo ya Mungu.”
Nadharia Tisini na Tano zilikuwa nini?
Zilikuwa nadharia zilizolenga moja kwa moja upotovu mahususi uliokuwapo ndani ya kanisa katika siku za Luther; mengi yake yalihusiana na masuala ya msamaha, toharani, na mamlaka ya papa. Ya kwanza miongoni mwao ilikuwa ya kushangaza sana:
Kwa kusema “Tumbun,” Bwana na Mwalimu wetu Yesu Kristo, alipendelea kwamba maisha yote ya waaminio yawe ya toba. (Dominus et magister noster Iesus Christus dicendo “Poenitentiam agite etc.” omnem vitam fidelium poenitentiam esse voluit.)
Luther alikuwa ametambua kwamba tafsiri ya Vulgate ya “Tubuni” (poenitentiam agite) ilikuwa rahisi kutafsiriwa vibaya kuwa “fanyeni kitubio (au toba).” Na pia alikuwa ameielewa kanuni ambayo John Calvin angekuja kuufafanua baadaye kwa uwazi mkubwa: toba au kutubu si tendo la muda mfupi tu; ni kugeuza maisha yote—kuikana dhambi kunakofanywa kwa kazi ya neema ya Roho Mtakatifu. Kwa hivyo haiwezi kuwa tendo moja linalokamilika mara moja; ni mtindo wa maisha unaodumu hadi kufika utukufu.
Luther aliishi maisha yaliyojaa na ya kuthubutu ambayo ni wasifu mrefu tu unaoweza kuyasimulia ipasavyo. Alikuwa mtu wa ajabu mwenye nguvu nyingi alizopewa na Mungu. Hotuba yake ilikuwa ya moja kwa moja na wazi, na mara nyingi pia ilikuwa ya lugha ya kidunia. Alikuwa mwalimu wa theolojia, mhubiri wa injili, na mwandishi wa baadhi ya vitabu muhimu zaidi katika kipindi cha Mageuzo. Mojawapo ya maandishi yake ya mwanzo yaliyojulikana sana ni On the Babylonian Captivity of the Church, na katika On the Freedom of a Christian alieleza jinsi waamini ndani ya Yesu Kristo wanavyowekwa huru ili wampende Mungu na kuwahudumia jirani zao. Hivyo aliandika sentensi iliyosukwa kwa uzuri inayokamata upinzani wa maisha yanayoweka injili kuwa kiini: “Mtu Mkristo ni bwana aliye huru kuliko wote, na hayuko chini ya yeyote; na mtu Mkristo ni mtumishi mwenye wajibu kuliko wote, na amejitiisha kwa kila mtu.”
Kwa mahubiri yake, maandishi, na hasa kwa ushawishi wake katika kufafanua wokovu kwa neema kupitia imani katika Kristo, Luther alitumiwa na Mungu kuligeuza kanisa la Kikristo. Viongozi wa Mageuzi nchini Uingereza na Uskochi waliathiriwa na maandishi yake, ambayo mara nyingi yalipenyezwa mabaharia wafanyabiashara. Hasa huko Uskochi, wafia-dini wa St. Andrews, Patrick Hamilton na George Wishart (ambaye mlinzi wake alikuwa John Knox), walikuwa wafuasi wa mafundisho ya Luther. Vivyo hivyo nchini Uingereza, shujaa William Tyndale aliacha urithi si tu katika tafsiri yake ya Biblia ya Kiingereza bali pia katika katika mkusanyiko mzima wa maandiko yaliyoakisi kazi ya Mwanamageuzi huyo wa Kijerumani.
Lakini Luther alifundisha nini? Mambo aliyoyapa mkazo yanafupishwa vyema katika zile sola zinazojulikana za Mageuzi: (1) sola Scriptura: tunamjua Mungu kupitia Maandiko pekee, si kwa mapokeo ya kanisa; (2) sola gratia: tunapokea msamaha kwa neema ya Mungu pekee, si kwa sababu tunastahili; (3) sola fide: tunahesabiwa haki kwa imani pekee, si kwa imani pamoja na kitu kingine; (4) sola Christus: utajiri wote wa Mungu hutolewa kwetu katika Kristo pekee; (5) Soli Deo gloria: lengo la maisha yote ni utukufu wa Mungu pekee.
Kanuni hizi zilitilia mkazo tu msisitizo ambao Martin Luther aliupata katika Maandiko Matakatifu. Lakini katika muktadha wake, kilicho muhimu zaidi kuhusu kanuni hizo si tu yale waliyoyasisitiza bali pia yale yaliyoachwa. Sio Martin Luther wala Wanamatengenezi wengine wa ngazi ya juu walilidharau kanisa. Lakini waliliona kanisa kuwa shahidi na kielelezo chenye nguvu cha wokovu kwa neema—si mtoaji wa wokovu huo. Kwa namna fulani, basi, kanisa halikushindwa tu kuifundisha injili kwa usahihi; lilikuwa limechukua kwa nguvu nafasi ya Roho Mtakatifu katika wokovu. Kule kurejeshwa kwa huduma ya Roho katika utekelezaji wa ukombozi ndiko kulikoleta hisia ya ukaribu wa moja kwa moja wa neema ya Mungu, pamoja na furaha na faraja ya msamaha na maisha mapya ndani ya Kristo. Ni kwa Kristo peke yake, wala si kwa upatanishi wa kanisa, ndiko tunakopaswa kukimbilia ili tupate neema na wokovu.
Hatujajadili hapa Wanamatengenezi wengine wakuu—Huldrych Zwingli na Heinrich Bullinger, John Calvin na John Knox, na wengine wengi. Lakini hata mtazamo huu mfupi kumhusu Luther na ushawishi wake unaonyesha kwamba karne ya kumi na sita ilikuwa kipindi cha kihistoria chenye uzito mkubwa katika historia ya Kanisa la Kikristo. Hakikuwa bila makosa yake, wala mapungufu yake. Lakini Wakristo wa siku hizo walijaa nguvu na msukumo wa ugunduzi huu mkuu—kwamba mzigo wa dhambi zao ulikuwa umechukuliwa na Yesu Kristo, nao, hatimaye, wangewekwa huru. Hizo zilikuwa siku, kama Knox alivyoeleza, ambazo “Mungu aliwapa Roho Wake Mtakatifu watu wa kawaida kwa wingi sana.”
Hilo ndilo ambalo bado tunalihitaji!
Makala haya yalichapishwa awali kwenye Blogu ya Ligonier Ministries.


