Martin Luther Alikufaje?
30 Juni 2025
Martin Luther Alikufaje?
30 Juni 2025

Kwa nini Mageuzo Yalikuwa ya Lazima?

Kanisa daima linahitaji mageuzo Hata katika Agano Jipya, tunamwona Yesu akimkemea Petro, na tunamwona Paulo akiwaonya Wakorintho. Kwa kuwa Wakristo daima ni wenye dhambi, kanisa litahitaji mageuzo kila wakati. Swali kwetu sisi, hata hivyo, ni lini haja ina kuwa lazima isiyoweza kuepukika?

Wanamageuzi wakuu wa karne ya kumi na sita walikata shauri kwamba mageuzo yalikuwa ya dharura na muhimu katika siku zao. Katika kutafuta mageuzo kwa kanisa, walikataa misimamo miwili mikali. Kwa upande mmoja, walikataa wale waliodai kwamba kanisa lilikuwa thabiti kimsingi na halikuhitaji mabadiliko ya msingi. Kwa upande mwingine, walikataa wale waliodhani kwamba wangeweza kuunda kanisa kamilifu katika kila hali. Kanisa lilihitaji mageuzo ya msingi, lakini pia lingehitaji kujirekebisha lenyewe kila wakati. Wanamageuzi walifikia maamuzi haya kutokana na uchunguzi wao wa Biblia.

Mnamo mwaka wa 1543, Mwanamageuzi wa Strasbourg, Martin Bucer, alimwomba John Calvin aandike utetezi wa Mageuzo kwa ajili ya kuwasilishwa kwa Mfalme Charles V katika baraza la viongozi wa milki ya Roma uliopangwa kufanyika Speyer mwaka 1544. Bucer alijua kwamba mfalme wa Kikatoliki wa Kirumi alikuwa amezungukwa na washauri ambao walikuwa wanakashifu juhudi za mageuzo kanisani, na aliamini kwamba Calvin alikuwa mhudumu mwenye uwezo zaidi wa kutetea madhumuni ya Waprotestanti.

Calvin aliinukia changamoto hiyo na akaandika moja ya kazi zake bora, “Umuhimu wa Kufanya mageuzo ya Kanisa.” Maandishi haya thabiti hayakumshawishi mfalme, lakini yamekuja kuchukuliwa na wengi kama mawasilisho bora ya sababu za Mageuzi yaliyowahi kuandikwa.

Calvin anaanza kwa kutambua kwamba kila mtu alikubaliana kuwa kanisa lilikuwa na “magonjwa mengi na makubwa.” Calvin anasema kwamba mambo yalikuwa mazito sana kiasi kwamba Wakristo hawangeweza kuvumilia “kuchelewa zaidi” kufanya mageuzo au kusubiri “suluhisho la polepole.” Anakataa madai kwamba Wanamageuzo walikuwa na hatia ya “ubunifu wa haraka na usio na heshima.” Badala yake, anasisitiza kwamba “Mungu alimwinua Luther na wengine” kuhifadhi “ukweli wa dini yetu.” Calvin aliona kwamba misingi ya Ukristo ilikuwa inatishiwa na kwamba ni ukweli wa kibiblia pekee ndio ungeweza kulihuisha kanisa.

Calvin anaangalia maeneo manne makubwa katika maisha ya kanisa ambayo yanahitaji mageuzo. Maeneo haya yanaunda kile anachokiita roho na mwili wa kanisa. Roho ya kanisa inaundwa na “ibada safi na halali ya Mungu” na “wokovu wa wanadamu.” Mwili wa kanisa unaundwa na “matumizi ya sakramenti” na “utawala wa kanisa.” Kwa Calvin, masuala haya yalikuwa katika kiini cha mijadala ya Mageuzo. Ni muhimu kwa uhai wa kanisa na yanaweza kueleweka kwa usahihi pekee kupitia mafundisho ya Maandiko.

Tunaweza kushangaa kwamba Calvin aliweka kumwabudu Mungu kama suala la kwanza la Mageuzo, lakini haya yalikuwa maudhui thabiti kwake. Hapo awali, alikuwa ameandika kwa Kadinali Sadoleto: “Hakuna kitu hatari zaidi kwa wokovu wetu kuliko ibada ya Mungu isiyo na mpangilio na iliyopotoka.” Ibada ni mahali tunapokutana na Mungu, na mkutano huo lazima ufanyike kwa viwango vya Mungu. Ibada yetu inaonyesha kama kweli tunakubali Neno la Mungu kuwa mamlaka yetu na kujisalimisha kwake. Ibada iliyobuniwa na mtu binafsi ni aina ya haki kwa matendo na pia ni maonyesho ya ibada ya sanamu.

Kisha, Calvin aligeukia kile ambacho mara nyingi tunafikiria kama suala kuu la Mageuzo, yaani, mafundisho ya kuhesabiwa haki:

Tunashikilia msimamo kwamba haijalishi matendo ya mtu ni ya aina gani, anahesabiwa kuwa mwenye haki mbele za Mungu kwa msingi wa rehema ya bure kabisa; kwa kuwa Mungu, bila kuzingatia matendo, humkubali kwa hiari ndani ya Kristo kwa kumhesabia haki ya Kristo kana kwamba ni yake mwenyewe. Hii tunaiita haki ya imani, yaani, pale mtu anapokuwa hana tena tumaini lolote katika matendo yake, na anatambua kwa hakika kwamba msingi pekee wa kukubalika kwake mbele za Mungu ni haki ambayo hana ndani yake mwenyewe, bali ameiazima kutoka kwa Kristo. Hoja ambayo kwayo ulimwengu daima hupotea, (kwa kuwa kosa hili limeendelea katika karibu kila enzi,) ni katika kufikiria kwamba mwanadamu, ingawa ana upungufu kwa kiasi fulani, bado kwa kiwango fulani anastahili kibali cha Mungu kwa matendo.

Mambo haya ya msingi yanayounda roho ya kanisa yanaungwa mkono na mwili wa kanisa: sakramenti na utawala wa kanisa. Sakramenti lazima zirudishwe kwa maana na matumizi safi na rahisi kama ilivyotolewa katika Biblia. Utawala wa kanisa lazima ukatae aina zote za udhalimu unaofunga dhamiri za Wakristo kinyume na Neno la Mungu.

Tunapoangalia kanisa katika siku zetu, tunaweza kuamua kwamba mageuzo yanahitajika—kwa kweli, ni muhimu—katika maeneo mengi ambayo Calvin alikuwa akiyashughulikia. Ni Neno na Roho wa Mungu pekee ndiye atakayefanya mageuzo katika kanisa. Lakini tunapaswa kuomba na kufanya kazi kwa uaminifu ili mageuzo kama hayo yaje katika wakati wetu.


Makala haya yalichapishwa kwanza katika Blogu ya Huduma za Ligonier.

W. Robert Godfrey
W. Robert Godfrey
Dkt. W. Robert Godfrey ni mwenyekiti wa bodi ya Ligonier pia ni rais mstaafu na profesa mstaafu wa historia ya kanisa katika Seminari ya Westminster California. Yeye ni mwandishi wa vitabu kadhaa, ikiwa ni pamoja na Kuokoa Mageuzo na Kujifunza Kupenda Zaburi.