
Kwa nini Mageuzo Yalikuwa ya Lazima?
1 Julai 2025
Imani na maungamo ya Kiprotestanti
8 Julai 2025Kwa nini Mageuzo Bado Yanamaana

Mnamo Oktoba 31, 2016, Papa Francis alitangaza kwamba baada ya miaka mia tano, Waprotestanti na Wakatoliki sasa “wana fursa ya kurekebisha wakati muhimu wa historia yetu kwa kusonga mbele zaidi ya mabishano na kutokubaliana ambako mara nyingi kumetuzuia sisi kuelewana.” Kutokana na hayo, inaonekana kana kwamba Mageuzo yalikuwa ugomvi usiofaa na usiohitajika juu ya mambo madogo, mlipuko wa kitoto ambao sote tunaweza kuusahau sasa kwa vile tumekuwa watu wazima.
Lakini mwambie hayo Martin Luther, ambaye alihisi ukombozi na furaha kubwa alipogundua kuhesabiwa haki kwa imani pekee kiasi kwamba aliandika, “Nilihisi kwamba nilizaliwa upya kabisa na nilikuwa nimeingia paradiso yenyewe kupitia milango iliyo wazi.” Mwambie hayo William Tyndale, ambaye aliiona kuwa ni “habari njema ya shangwe na furaha” kiasi kwamba zilimfanya “kuimba, kucheza, na kuruka kwa furaha.” Mwambie Thomas Bilney, ambaye aligundua ilimpa “faraja ya ajabu na utulivu, kiasi kwamba mifupa yangu iliyojeruhiwa iliruka kwa furaha.” Ni wazi kwamba, wale Wanamageuzo wa kwanza hawakufikiri walikuwa wanachochea ugomvi wa kitoto; kama walivyoona, walikuwa wamegundua habari njema za furaha kuu.
HABARI NJEMA MWAKA WA 1517
Mwanzoni mwa karne ya kumi na sita, Ulaya ilikuwa bila Biblia ambayo watu wangeweza kuisoma kwa takriban miaka elfu moja. Thomas Bilney hakuwahi kukutana na maneno “Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi” (1 Tim. 1:15). Badala ya Neno la Mungu, walibaki na ufahamu kwamba Mungu ni Mungu ambaye huwawezesha watu kupata wokovu wao wenyewe. Kama mmoja wa walimu wa siku hiyo alivyopenda kusema, “Mungu hatawakataza neema wale wanaofanya juhudi zao zote.” Hata hivyo, maneno yaliyokusudiwa kuwa ya kufurahisha yaliwaacha watu wote walioyachukulia kwa uzito na ladha chungu sana. Unawezaje kuwa na uhakika kwamba kweli umefanya juhudi zako zote? Je, ungejuaje kama umekuwa aina ya mtu mwenye haki anayestahili wokovu?
Martin Luther hakika alijaribu. “Nilikuwa mtawa mzuri,” aliandika, “na nilifuata taratibu zangu kwa dhati kiasi kwamba ningeweza kusema kwamba kama mtawa yeyote angeweza kufika mbinguni kupitia nidhamu ya kitawa, ningekuwa nimeingia.” Na bado, aligundua:
Dhamiri yangu haikunipa uhakika, lakini siku zote nilikuwa na shaka na kusema, “Hukulifanya hilo kwa usahihi. Hukuwa na majuto ya kutosha. Uliliacha hilo nje ya ungamo lako.” Kadiri nilivyojaribu kurekebisha dhamiri isiyo na uhakika, dhaifu na yenye matatizo ya mila za kibinadamu, ndivyo kila siku nilivyozidi kuipata ikiwa haina uhakika zaidi, dhaifu zaidi na yenye matatizo zaidi.
Kulingana na Ukatoliki wa Kirumi, Luther alikuwa sahihi kabisa kuwa na shaka kuhusu mbingu. Uhakika wa nafasi mbinguni ulionekana kama dhana potovu na ulikuwa mojawapo ya mashtaka yaliyotolewa dhidi ya Joan wa Arc katika kesi yake mwaka 1431. Hapo, majaji walitangaza,
Mwanamke huyu anatenda dhambi anaposema ana uhakika wa kupokelewa katika Paradiso kana kwamba tayari ni mshiriki wa … utukufu, kwa kuwa katika safari hii ya duniani hakuna hujaji anayejua kama anastahili utukufu au adhabu, ambayo hakimu mkuu pekee anaweza kusema.
Hukumu hiyo ilikuwa na maana kamili ndani ya mantiki ya mfumo huo: ikiwa tunaweza kuingia mbinguni tu kwa sababu tumekuwa (kwa neema ya Mungu) na tunastahili kibinafsi, basi bila shaka hakuna mtu anayeweza kuwa na uhakika. Kwa kufuata hoja hiyo, ninaweza kuwa na imani na mbingu kwa kiwango sawa na imani yangu ya kutokuwa na dhambi.
Hiyo ndiyo hasa sababu kijana Martin Luther alipiga kelele kwa hofu akiwa mwanafunzi alipokuwa karibu apigwe na radi katika dhoruba. Alikuwa na hofu ya kifo, kwani bila ufahamu wa wokovu wa Kristo wa kutosha na wenye neema —bila ufahamu wa kuhesabiwa haki kwa imani pekee—hakuwa na tumaini la mbinguni.
Na hiyo ndiyo sababu ugunduzi wake mpya katika Maandiko wa kuhesabiwa haki kwa imani pekee ulionekana kama kuingia paradiso kupitia mlango ulio wazi. Ilimaanisha kwamba, badala ya wasiwasi wake wote na hofu, sasa angeweza kuandika:
Wakati shetani anapotutupia dhambi zetu na kutangaza kwamba tunastahili kifo na jahanamu, tunapaswa kusema hivi: “Ninakubali kwamba nastahili kifo na jahanamu.” kwa hivyo? Je, inamaanisha kwamba nitahukumiwa laana ya milele? La hasha. Kwa maana namjua Mmoja ambaye aliteseka na kufanya upatanisho kwa niaba yangu. Jina lake ni Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Mahali alipo, ndipo nitakapokuwa pia.”
Na hiyo ndiyo sababu Mageuzo yalifanya watu wapende mahubiri na kusoma Biblia. Kwa kuwa, kuweza kusoma neno la Mungu na kuona ndani yake habari njema kwamba Mungu anaokoa wenye dhambi, si kwa msingi wa jinsi wanavyotubu vizuri bali tu kwa neema yake mwenyewe, ilikuwa kama mwangaza wa jua la Mediterania katika dunia tata yenye hatia ya kidini.
HABARI NJEMA MWAKA WA 2017
Hakuna wema au umuhimu wa maarifa ya Mageuzo ambayo yamefifia katika kipindi cha miaka mia tano iliyopita. Majibu ya maswali muhimu yale yale bado yanatofautisha kati ya kukata tamaa kwa binadamu na furaha. Nini kitatokea kwangu nitakapokufa? Nitajuaje? Je, kuhesabiwa haki ni zawadi ya mwenye haki (kama walivyodai Wanamageuzo), au ni mchakato wa kuwa mtakatifu zaidi (kama Roma inavyodai)? Je, naweza kumtegemea Kristo pekee kwa ujasiri kuhusu wokovu wangu, au wokovu wangu pia unategemea juhudi zangu na mafanikio katika kufikia utakatifu?
Kwa hakika kabisa, kinachowachanganya watu kufikiria kwamba Mageuzo ni sehemu ya historia ambayo tunaweza kuiwacha nyuma ni wazo kwamba ilikuwa tu ni jibu la tatizo fulani la siku hiyo. Lakini kadiri mtu anavyoangalia kwa karibu, ndivyo inavyokuwa wazi zaidi: Mageuzo hayakuwa hasa harakati hasi za kuhusu kuiondokea Roma na ufisadi wake; ilikuwa ni harakati chanya, ya kuikaribia injili. Na hiyo ndiyo hasa inayohifadhi uhalali wa Mageuzo hivi leo. Kama Mageuzo yangekuwa ni itikio tu kwa hali ya kihistoria miaka mia tano iliyopita, mtu angetarajia kuwa yangekwisha. Lakini kama mpango wa kusonga karibu zaidi na injili, hauwezi kumalizika.
Pingamizi nyengine ni kwamba utamaduni wa leo wa fikra chanya na kujithamini umeondoa haja yoyote inayoonekana ya mwenye dhambi kuhesabiwa haki. Si wengi leo wanaojikuta wakivaa mavazi ya ngozi na kuvumilia maombi ya usiku kucha katika baridi kali ili kupata kibali cha Mungu. Kwa jumla, basi, tatizo la Luther la kuteswa na hatia mbele ya Hakimu wa kimungu linatupiliwa mbali kama tatizo la karne ya kumi na sita, na suluhisho lake la kuhesabiwa haki kwa imani pekee linatupiliwa mbali kama lisilo la lazima kwetu hivi leo.
Lakini kwa kweli ni katika muktadha huu ambapo suluhisho la Luther linajitokeza kama habari yenye furaha na inayofaa. Kwa kuwa, baada ya kuachana na wazo kwamba daima huenda tukawa na hatia mbele za Mungu na kwa hivyo kuhitaji Kuhesabiwa haki yake, utamaduni wetu umeshindwa na tatizo la zamani la hatia kwa hila, bila kuwa na suluhisho. Leo, sote tunakabiliwa na ujumbe kwamba tutapendwa zaidi tukijifanya wa kuvutia zaidi. Inaweza kuwa haihusiani na Mungu, ila bado ni dini ya matendo, na ambayo imejikita kwa kina. Kwa hilo, Mageuzo yana habari njema inayong’aa zaidi. Luther anazungumza maneno yanayokata giza kama miale ya jua ya ajabu na isiyotarajiwa kabisa.
Upendo wa Mungu hautafuti, bali huumba, kile kinachompendeza…. Badala ya kutafuta mema yake yenyewe, upendo wa Mungu hutiririka na kutoa mema. Kwa hiyo wenye dhambi wanavutia kwa sababu wanapendwa; hawapendwi kwa sababu wanavutia.
KWA MARA NYINGINE, WAKATI UMEIVA
Miaka mia tano baadaye, Kanisa Katoliki la Kirumi bado halijafanyiwa mageuzo. Kwa lugha ya kiupendo ya kiekumeni inayotumiwa na Waprotestanti na Wakatoliki wengi wa Kirumi, Roma bado inakataa kuhesabiwa haki kwa imani pekee. Inajisikia inaweza kufanya hivyo kwa sababu Maandiko hayachukuliwi kama mamlaka ya juu kabisa ambayo mapapa, mabaraza, na mafundisho lazima wakubaliane nayo. Na kwa sababu Maandiko yamewekwa kando, ufahamu wa Biblia hautiliwi nguvu, na kwa hivyo maskini mamilioni ya Wakatoliki wa Kirumi bado wanazuiwa nuru ya Neno la Mungu.
Nje ya Ukristo wa Kikatoliki, mafundisho ya kuhesabiwa haki kwa imani pekee mara nyingi huepukwa kama lisilo na umuhimu, lisilo sahihi, au lenye kuchanganya. Baadhi ya mitazamo mipya kuhusu kile ambacho Mtume Paulo alimaanisha kwa kuhesabiwa haki, hasa wakati ambapo wamekuwa wakielekeza msisitizo mbali na haja yoyote ya wokovu wa kibinafsi, kwa vyovyote vile wamewachanganya watu, na kuacha makala ambayo Luther alisema hawezi kuyaachwa au kuathiriwa ikawa hivyo—imeachwa au kuathiriwa.
Sasa si wakati wa kuwa na haya kuhusu kuhesabiwa haki au mamlaka makuu ya Maandiko yanayotangaza kuhesabiwa haki. Kuhesabiwa haki kwa imani pekee si mabaki ya vitabu vya historia; inabaki leo kama ujumbe pekee wa ukombozi wa mwisho, ujumbe wenye nguvu ya kina zaidi ya kuwafanya wanadamu kufunguka na kustawi. Inatoa uhakikisho mbele ya Mungu wetu mtakatifu na kuwageuza wenye dhambi wanaojaribu kumhonga Mungu kuwa watakatifu wanaompenda na kumcha.
Na oh ni fursa gani tulizo nazo leo za kuieneza habari njema hii! Miaka mia tano iliyopita, uvumbuzi wa hivi karibuni wa mashine ya uchapishaji wa Gutenberg ulimaanisha kwamba nuru ya injili ingeweza kuenea kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa hapo awali. Biblia za Tyndale na vijitabu vya Luther vingeweza kusambazwa kwa maelfu. Leo, teknolojia ya kidijitali imetupa wakati mwingine wa Gutenberg, na ujumbe huo huo sasa unaweza kuenezwa kwa kasi ambayo Luther hangeweza kuifikiria.
Mahitaji na fursa ni makubwa kama yalivyokuwa miaka mia tano iliyopita—kwa kweli, ni makubwa zaidi. Basi na tuwe na ujasiri kutokana na uaminifu wa Wanamageuzi na tuiinue injili hiyo ya ajabu juu, kwa maana haijapoteza utukufu wake wala nguvu zake za kuondoa giza letu.
Chapisho hili lilichapishwa awali katika jarida la Tabletalk.