John Calvin kuhusu Umuhimu wa Kufanya Mageuzo ya Kanisa
23 Juni 2025
Kwa Nini Unafanya Kazi?
23 Juni 2025
John Calvin kuhusu Umuhimu wa Kufanya Mageuzo ya Kanisa
23 Juni 2025
Kwa Nini Unafanya Kazi?
23 Juni 2025

Injili Inamaanisha Nini?

Wakristo wengi, makanisa, na mashirika mara kwa mara hutumia neno injili kuelezea imani zao. Mijadala ya kitheolojia imejitokeza na inaendelea kutokea kuhusu maana ya injili na ni nani anaihubiri kwa uaminifu. Neno hili injili, linalojulikana linamaanisha nini? Njia bora ya kulijibu swali hilo ni kuigeukia Biblia.

Katika Agano Jipya la Kigiriki, nomino euangelion (“injili”) inatokea zaidi ya mara sabini. Kwa kuwa, kwa namna fulani, Agano Jipya lote linahusu injili, tungeweza kutarajia kwamba neno hilo lingetumika mara nyingi zaidi. Hata la kushangaza zaidi, matumizi yake yanatofautiana sana miongoni mwa waandishi wa vitabu vya Agano Jipya. Paulo analitumia neno hilo mara tatu zaidi ya waandishi wengine wote kwa pamoja. Matumizi mengine mengi yanapatikana katika Mathayo na Marko, na machache sana, kama yapo, katika Luka, Yohana, Petro, na Yakobo.

Neno injili kwa urahisi zaidi lina maana ya “habari njema.” Neno hilo si la kipekee kwa ujumbe wa Kikristo, lakini pia lilitumika katika dunia ya kipagani kumaanisha tangazo jema. Katika Agano Jipya, linarejelea habari njema za Yesu Mwokozi. Mara nyingi, hutumiwa kwa dhana kwamba msomaji anajua maana ya neno hilo.

Tunapochunguza kwa ukaribu zaidi njia ambazo injili inatumika katika Agano Jipya, mambo kadhaa yanajitokeza kwa nguvu. Kwanza, mara nyingi tunakutana na maneno “injili ya Mungu.” Maneno haya yansisitizia chanzo cha injili kama zawadi kutoka kwa Mungu. Injili ni ya asili ya kiungu, si ya kibinadamu. Pili, sifa ya injili imeelezewa kwa njia kadhaa: injili ni ya kweli (Wagalatia. 2:5, 14; Wakolosai. 1:5), yenye neema (Matendo 20:24), na yenye utukufu (2 Wakorintho. 4:4; 1 Timotheo 1:11). Tatu, tunaona maitikio mawili kwa injili. Itikio la msingi ni imani (Matendo 15:7; Waefeso 1:13). Lakini utiifu pia ni itikio (1 Petro 4:7; Warumi 1:5; 10:16; 16:26; 2 Thesalonike 1:8).

(Matumizi ya Paulo ya wazo la utiifu wa imani katika Warumi yana kipengele cha kejeli, anapowajibu wale waliomtuhumu kwa kuwa mpinga sheria (antinomianism), yaani, kuwa kinyume na sheria.) Jambo la nne, tunaona matokeo kadhaa ya injili. Injili, bila shaka, inaleta wokovu (Warumi 1:16; Waefeso 1:13). Pia inaleta ufalme (Mathayo 4:23; 9:35, 24:14). Inaamsha matumaini katika watu wa Mungu (Wakolosai 1:23). Injili pia ni motisha kwa utakaso (Marko 8:35; 10:29; 2 Wakorintho 9:13; Waefeso 6:15; Wafilipi 1:27).

Njia zote hizi ambazo neno injili linatumika zinaelekeza kwenye maudhui yake, lakini pia kuna vifungu katika Agano Jipya ambavyo vinaeleza wazi kuhusu maudhui yake. Katika kuchunguza maandishi haya, tunagundua kwamba wakati mwingine neno injili linarejelea kwa upana vipengele vyote vya wokovu na maisha mapya ambayo Yesu anawapa watu Wake, na wakati mwingine kwa matumizi finyu hurejelea kile ambacho Yesu anatufanyia nje yetu. Kwa maneno mengine, wakati mwingine neno injili linarejelea kwa upana kazi ya Yesu ya kutuhesabia haki na utakaso kwa ajili ya watu Wake na ndani yao, na wakati mwingine linarejelea kwa njia finyu kazi ya Yesu ya kutuhesabia haki. Njia nyingine ya kutofautisha hili ni kwamba wakati mwingine neno injili linarejelea kwa upana utimilifu wote wa Agano Jipya kwa kile kilichoahidiwa katika Agano la Kale, na wakati mwingine neno injili linatumika kwa njia finyu kwa matendo ya Yesu kinyume na matendo yetu ya Sheria.

Mfano wa maana pana ya neno injili unaweza kuonekana katika Marko 1:1, “Mwanzo wa injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.” Matumizi haya ya neno injili yanaonekana kurejelea kila kitu ambacho Marko anatueleza kuhusu mafundisho na kazi ya Yesu. Tunaona matumizi mengine mapana katika Ufunuo 14:6–7:

Kisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani, naye alikuwa na Injili ya milele ya kuwatangazia wale waishio duniani, kwa kila taifa, kabila, lugha na watu. Akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumpa utukufu, kwa maana saa ya hukumu yake imewadia. Mwabuduni yeye aliyeziumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.”

Hapa injili ni mwito wa kutubu na kumwabudu Mungu.

Mara nyingi, neno injili linatumika kwa njia finyu na kwa maudhui maalum. Tunaona hili katika 1 Wakorintho 15:1–4:

Basi ndugu zangu nataka niwakumbushe kuhusu Injili niliyowahubiria, mkaipokea na ambayo katika hiyo mmesimama, Kwa Injili hii mnaokolewa mkishikilia kwa uthabiti neno nililowahubiria ninyi—La sivyo, mmeamini katika ubatili. Kwa maana yale niliyopokea ndiyo niliyowapa ninyi kama yenye umuhimu wa kwanza: Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yasemavyo Maandiko.

Hapa, injili ni ujumbe wa kifo cha wokovu na ufufuo wa Yesu.

Katika sehemu nyingine, Paulo anaandika kuhusu “injili tukufu ya Mungu aliye na baraka ambayo nimekabidhiwa,” na anabainisha injili hiyo ni nini:

Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote. Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili katika mimi, niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Kristo Yesu apate kuonyesha uvumilivu wake usio na kikomo, ili niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini na wapate uzima wa milele. (1 Tim. 1:11, 15–16)

Hapa, injili ni kazi ya wokovu ya Kristo kwa wenye dhambi.

Paulo anaandika vile vile katika 2 Timotheo:

Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu,ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele,Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Kristo Yesu, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kwa njia ya Injili…. Kumbuka Yesu Kristo, aliyefufuka kutoka kwa wafu, uzao wa Daudi, kama ilivyohubiriwa katika injili yangu. (2 Tim. 1:8–10; 2:8)

Matumizi haya finyu ya neno injili yalikuwa ya kawaida sana katika maandiko ya Wanamageuzi wa karne ya kumi na sita. Tunaweza kuona hili katika wazo la John Calvin:

Neno la imani limewekwa kwa njia ya tamathali ya semi (metonymy) [kutumia jina la wazo moja kumaanisha wazo lingine linalohusiana nalo] kumaanisha neno la ahadi, yaani Injili yenyewe, kwa sababu lina uhusiano na imani. Tofauti kati ya sheria na Injili inapaswa kueleweka, na kutokana na tofauti hii tunatambua kwamba, kama vile sheria inavyohitaji kazi, Injili inahitaji tu kwamba watu walete imani ili kuipokea neema ya Mungu.

Pia ni wazi katika Zakaria Ursinus. Karibu na mwanzoni mwa tahariri yake juu ya Katekisimu ya Heidelberg, Ursinus anayagawanya mafundisho yote katika sheria na injili:

Mafundisho ya kanisa yanajumuisha sehemu mbili: Sheria, na Injili; ambamo tumeelewa ujumla na kiini cha Maandiko Matakatifu. Sheria inaitwa Dekalojia, na injili ni mafundisho kuhusu Kristo mpatanishi, na msamaha wa bure wa dhambi, kupitia imani.

Tafakari kama hizo juu ya injili zimeendelea kuwa za kawaida katika theolojia ya Mageuzi, kama tunavyoona kutoka katika nukuu hii ndefu ya kuvutia kutoka kwa mwanatheolojia mkuu wa Kiholanzi Herman Bavinck:

Lakini neno la Mungu, kama sheria na injili, ni ufunuo wa mapenzi ya Mungu, kutangaza agano la matendo na agano la neema. . . . Ingawa kwa maana pana maneno “sheria” na “injili” yanaweza kwa hakika kutumika kuashiria agano la zamani na jipya la neema, katika maana yao halisi yanaelezea waziwazi ufunuo wa mara mbili tofauti wa mapenzi ya kimungu [Bavinck hapa anataja ushahidi wa maandiko mengi ya Agano Jipya]. . . . Katika maandiko haya sheria na injili zinatofautishwa kama madai na zawadi, kama amri na ahadi, kama dhambi na neema, kama ugonjwa na uponyaji, kama kifo na uzima . . . . Sheria inatokana na utakatifu wa Mungu, injili inatokana na neema ya Mungu; sheria inajulikana kutoka kwenye mazingira, injili inajulikana tu kutoka katika ufunuo maalum; sheria inadai haki kamilifu, lakini injili inakupa haki kamili; sheria inawaongoza watu kwenye uzima wa milele kwa matendo, na injili inazalisha matendo mema kutoka katika utajiri wa uzima wa milele uliotolewa kwa imani; sheria kwa sasa inawahukumu watu, na injili inawaondolea hatia; sheria inajieleza kwa watu wote, na injili kwa wale tu wanaoishi ndani ya usikivu wake.

Jinsi gani ilivyo wazi, tofauti, ya kibiblia, na ya thamani uwasilishaji huu wa injili.

Kanisa linahitaji kuihubiri injili katika maana zake zote pana na finyu. Neno la Kigiriki la injili limeipa dunia inayozungumza Kiingereza neno uinjilisti. Uinjilisti wa kweli, kulingana na Agizo Kuu alilotoa Yesu katika Mathayo 28:18–20, ni suala la kufanya wanafunzi: kwanza, kwa maana finyu ni kuwaita wanaume na wanawake kumwamini Yesu na, pili, kwa maana pana ni kuwafundisha kushika mambo yote ambayo Yesu amewafundisha watu Wake. Kwa ajili ya injili, hebu sote tuendeleze uinjilisti wa kweli.


Makala haya yalichapishwa kwanza katika Blogu ya Huduma za Ligonier.

W. Robert Godfrey
W. Robert Godfrey
Dkt. W. Robert Godfrey ni mwenyekiti wa bodi ya Ligonier pia ni rais mstaafu na profesa mstaafu wa historia ya kanisa katika Seminari ya Westminster California. Yeye ni mwandishi wa vitabu kadhaa, ikiwa ni pamoja na Kuokoa Mageuzo na Kujifunza Kupenda Zaburi.