
Ushauri wa Luther kwa Maisha ya Kikristo
15 Julai 2025
Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kuhusu Kuwa Mzazi
2 Septemba 2025Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kuhusu Kuwa Mzazi
Hivi karibuni nimekuwa babu mkubwa, nikiwakaribisha vitukuu wawili wa kike na kitukuu mmoja wa kiume katika familia yetu. Haya ni baadhi ya mawazo ya kibiblia kuhusu kulea watoto ambayo nina yarithisha kwa wajukuu zangu pamoja na wenza wao.
1. Malezi ni mwito muhimu ambao Mungu amekupa.
Zaburi 78 inanijia akilini:
Aliagiza amri kwa Yakobo na akaweka sheria katika Israeli, ambazo aliwaamuru baba zetu wawafundishe watoto wao, Ili kizazi kijacho kizijue, pamoja na watoto ambao watazaliwa, nao pia wapate kuwaeleza watoto wao. Ndipo wangeweka tumaini lao kwa Mungu, nao wasingesahau matendo yake, bali wangalizishika amri zake. (Zaburi 78:5–7)
Ni nini kinaweza kuwa cha muhimu zaidi kuliko kuwarithisha kizazi kijacho ukweli kuhusu Mungu? Je, kuna urithi gani muhimu zaidi kuliko kizazi baada ya kizazi kuweka tumaini lao kwa Mungu? Utakuwa na fursa nyingi zenye changamoto maishani mwako, lakini chache zitakuwa na athari kubwa kama kulea watoto “kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana” (Waefeso 6:4)
2. Kujifunza kuishi chini ya mamlaka ni msingi.
Katika Waefeso 6:1–3, Mungu anawahutubia watoto: “Enyi Watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema. “Waheshimu baba yako na mama yako (hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi), upate Baraka na uishi siku nyingi duniani” Mungu ameweka duara ambalo watoto wanapaswa kuishi ndani yake. Mpaka wa duara hilo ni kuwaheshimu na kuwatii wazazi. Mungu anaahidi baraka za ajabu mtoto anapoishi katika duara hilo; mambo yatakwenda vizuri, na watafurahia maisha marefu.
Hizi ni baraka ambazo kila mtoto na mzazi wanazitaka. Kuheshimu na kutii ni jambo la muhimu zaidi kuliko kufanya tu kile unachoambiwa. Ni ahadi ya imani kumtumaini na kumtii Mungu. Katika kuwafundisha watoto wako kuwa chini ya mamlaka, unaonyesha ukweli wa msingi kwamba kunyenyekea chini ya mamlaka ya Mungu ni njia ya baraka.
3. Moyo ndio chemchemi ya uzima.
Linda moyo wako, kuliko yote uyalindayo, maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. (Mithali 4:23)
Uzima hutiririka kutoka moyoni. Tatizo tulilonalo si tu njia ambazo tuna tenda dhambi, bali dhambi inayokaa chini ya dhambi. Ni kile kiburi, ubinafsi uliokithiri, kujipenda, wivu, na mienendo mbalimbali ya dhambi ya moyo ambayo huchochea tabia. Ni rahisi kwa wazazi kuangazia tabia na kukosa kuuona moyo.
Yesu anatukumbusha kwamba tabia kama vile kutamani, udanganyifu, wivu, kashfa, kiburi, na majivuno hutoka moyoni (tazama Marko 7:2–23). Sehemu kubwa ya kazi ya malezi ni kuwasaidia watoto kutambua mitazamo ya moyo iliyo msingi wa dhambi zao. Bila shaka, kuelewa mitazamo ya moyo iliyo chini ya dhambi zako zinazoendelea kukuzinga kwa upesi kutakusaidia kuuliza maswali mazuri ambayo yatawasaidia watoto wako kuielewa mioyo yao.
4. Weka injili kuwa ndio kiini.
kiini cha imani yetu si jinsi ya kuwa mwema vya kutosha ili kupata uzima wa milele. Kiini cha imani yetu ni kuhusu Yule ambaye alikuwa mwema vya kutosha. Yesu alifanyika mwili ili awe Mwokozi wetu. Aliishi maisha ambayo hatungeweza kuishi; Aliishi bila dhambi ili tuweze kuwa na haki. Alikufa kifo ambacho hatungeweza kufa; Aliyatoa maisha Yake juu ya msalaba ili atuokoe sisi kutoka kwenye hatia na hukumu ya dhambi zetu. Alifufuliwa ili tupate kuhesabiwa haki. Hata sasa Anatuombea akiwa mkono wa kuume wa Mungu Baba.
Tumaini hili la neema, msamaha, wokovu, na uwezeshwaji ni ukweli ambao watoto wetu (na sisi wenyewe) tunauhitaji daima. Unapowarekebisha na kuwafundisha, daima weka tumaini la injili mbele ya watoto wako. Tunaikana injili tunapowaambia watoto kwamba wanaweza kuwa wema kwa nguvu zao wenyewe. Jambo la kutia moyo kutoka Waebrania 2:17 ni kwamba Yesu ambaye, kama mwanadamu, aliteseka kwa kujaribiwa, anaweza kutusaidia katika majaribu yetu.
5. Mfano unaoonyesha una nguvu sana.
Kumbukumbu la Torati 6:5 inashikilia ukweli huu: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa nguvu zako zote.” Upendo wako kwa Mungu, furaha yako ndani Yake, na shukrani na kuridhika kwako kwa vyote ambavyo Mungu alivyo kwako katika Kristo ni ukweli muhimu kwako wewe kuonyesha mfano kwa watoto wako. Mistari inayofuata inaonyesha jinsi mfano huu ulivyo muhimu: “Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. wafundishe watoto wako kwa bidii” (Kumbukumbu 6:6–7).
Kila siku, unapoishi na watoto wako, unawasilisha mtazamo wa uhalisia. Unawaonyesha kwamba unaamini kuwa Mungu ni mwema na huwapa thawabu wale wanaomtafuta. Kwa kumpenda Mungu na wengine, unaonyesha ukweli kwamba sheria ya Mungu ni nzuri. Unapofanya ibada kuwa kipaumbele, unawaambia kwamba uzima unapatikana kwa Mungu. Unapokuwa mwema kwa watu ambao si wema, unaonyesha ukarimu na wema wa Mungu. Kila kitu unachofanya kinatoa simulizi ya ukweli kwa watoto wako.
Unyenyekevu wako kwa Mungu katika mambo yote, uaminifu wako kuhusu jinsi moyo wako unavyopenda kutangatanga, na tumaini lako katika neema ya injili, yote yanatoa simulizi kwa watoto wako. Kuwalea watoto kwa ajili ya Mungu ni moja wapo ya kazi kubwa zaidi utakayowahi kuifanya.
Makala haya yalichapishwa kwanza katika Blogu ya Huduma za Ligonier.


