
Siku ya Mageuzo ni nini?
10 Julai 2025
Mambo Matano Unayopaswa Kujua Kuhusu Kuwa Mzazi
12 Agosti 2025Ushauri wa Luther kwa Maisha ya Kikristo

Je, enzi kuu ya Mungu, wokovu kwa neema, kuhesabiwa haki kwa imani, na maisha mapya katika umoja na Kristo yanamaanisha nini katika kuishi maisha ya Kikristo? Kwa Luther, yana maana nne:
Maana ya kwanza ni ufahamu kwamba muumini Mkristo ni simul iustus et peccato, mmoja amehesabiwa haki na bado ni mwenye dhambi. Kanuni hii, ambayo Luther huenda alichochewa na Yohana Tauler’s Theologia Germanica, ilikuwa kanuni yenye kuleta utulivu mkubwa: kwangu mimi, yote nionayo mimi ni mwenye dhambi; lakini ninapojiona ndani ya Kristo, naona mtu anayehesabiwa haki kwa haki Yake kamilifu. Mtu kama huyo basi anaweza kusimama mbele za Mungu akiwa mwenye haki kama Yesu Kristo—kwa sababu yeye ni mwenye haki tu katika haki ambayo ni ya Kristo. Hapa tumesimama salama.
Maana ya pili ni kugundua kwamba Mungu amekuwa Baba yetu katika Kristo. Tumekubaliwa. Moja ya masimulizi mazuri sana yanayopatikana katika Table Talk ya Luther, labda kwa umuhimu, yalirekodiwa na John Schlaginhaufen, ambaye alikuwa na sifa ya uzito wa moyo, lakini alipendwa sana.
Mungu lazima awe na urafiki zaidi kwangu na azungumze nami kwa njia ya kirafiki zaidi kuliko Katy wangu anavyozungumza na mtoto Martin. Aidha Katy au mimi hatungeweza kukusudia kung’oa jicho au kurarua kichwa cha mtoto wetu. Wala Mungu hangeweza. Mungu lazima awe na uvumilivu na sisi. Ametoa ushahidi wa hilo, na kwa hivyo alimtuma Mwanawe katika mwili wetu ili tumwangalie yeye kama mfano wa ubora.2
Tatu, Luther anasisitiza kwamba maisha katika Kristo ni lazima yawe maisha chini ya msalaba. Ikiwa tutaunganishwa na Kristo, maisha yetu yatafanana na Yake Njia ya kanisa la kweli na Mkristo wa kweli si kupitia theolojia ya utukufu (theologia gloriae) bali kupitia theolojia ya msalaba (theologia crucis). Hii inatuathiri kindani, tunapofia nafsi na kwa nje tunaposhiriki katika mateso ya kanisa. Theolojia ya utukufu ya enzi za kati ya kanisa la ulimwengu mzima lazima ishindwe na theolojia ya msalaba. Kwa tofauti zao zote katika kuelewa asili halisi ya sakramenti, Luther na Calvin ni wamoja hapa. Ikiwa tumeungana na Kristo katika kifo chake na ufufuo wake, na kuwekewa alama hivyo katika ubatizo wetu (kama Paulo anavyofundisha katika Rum. 6:1–14), basi maisha yote ya Kikristo yatakuwa ya kubeba msalaba.
Msalaba wa Kristo haumaanishi kipande cha ubao ambacho Kristo alibeba mabegani mwake, na ambacho baadaye aligongewa misumari, bali kwa ujumla unamaanisha mateso yote ya waaminifu, ambao mateso yao ni mateso ya Kristo, 2 Wakorintho 1:5 “Mateso ya Kristo yanazidi ndani yetu”; tena: “Sasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu, na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, ambao ni kanisa” n.k. (Wakolosai 1:24). Msalaba wa Kristo kwa hiyo kwa ujumla unamaanisha mateso yote ya Kanisa ambayo linayapitia kwa ajili ya Kristo.4
Muungano wa muumini na Kristo katika kifo chake na ufufuo wake, na jinsi unavyofanyakazi katika maisha ya kila siku, kwa Luther, ilikuwa kama lenzi za miwani ambazo Mkristo huzitumia kutazama kila tukio la maishani. Hii—theolojia ya msalaba—ndiyo inayoleta kila kitu katika mtazamo mkali zaidi na kutuwezesha kuelewa kupanda na kushuka kwa maisha ya Kikristo:
Ni faida kwetu kuyajua mambo haya, tusije tukamezwa na huzuni au kuanguka katika kutamauka tunapoona kwamba wapinzani wetu wanatutesa kikatili, wanatutenga na kutuangamiza. Lakini hebu tuwaze sisi wenyewe, kufuatia mfano wa Paulo kwamba lazima tujivunie msalaba tunaoubeba, si kwa ajili ya dhambi zetu, bali kwa ajili ya Kristo. Ikiwa tutazingatia tu ndani yetu yale mateso tunayovumilia, sio tu kwamba ni makali bali pia hayavumiliki; lakini tunapoweza kusema: “Mateso yako (Ee Kristo) yanazidi ndani yetu”; au, kama inavyosemwa katika Zaburi 44:22 “Hata hivyo kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa,” basi mateso haya siyo tu kwamba ni mepesi, bali pia ni matamu, kulingana na usemi huu: “Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi” (Mathayo 11:30).5
Nne, maisha ya Kikristo yanajulikana kwa uhakika na furaha. Hii ilikuwa mojawapo ya alama mahususi ya Mageuzo, na hueleweka hivyo. Ugunduzi upya wa Mageuzo kuhusu kuhesabiwa haki—kwamba, badala ya kufanya kazi hadi kufikia matumaini, maisha ya Kikristo kwa kweli huanza nayo—ulileta ukombozi wa kushangaza, na kufanya akili, nia na upendo kujawa na furaha. Ilimaanisha kwamba mtu sasa angeweza kuanza kuishi katika mwanga wa mustakabali uliotulia katika utukufu. Kwa hakika, mwanga huo uliangazia nyuma kwa maisha ya sasa, ukileta faraja kuu na kuachiliwa.
KUSIMAMA KWA KICHWA CHAKO
Kwa Luther, maisha ya Mkristo ni maisha yanayojikita katika Injili, yanayojengwa juu ya Injili, maisha yanayoitukuza Injili, ambayo yanayoonyesha neema huru na ukuu wa mamlaka ya Mungu, na kuiishi kwa shukrani kwa Mwokozi aliyekufa kwa ajili yetu, tukiwa tumeunganishwa naye katika kuubeba msalaba hadi mauti itakapomezwa katika ushindi, na imani ikawa kuona.
Pengine, mwaka 1522, walipokuwa wameketi wakimsikiliza Luther akihubiri Jumapili moja kanisani Borna, baadhi ya waumini wake walijiuliza ni nini kilichokuwa kiini cha injili hii iliyomfurahisha sana, na pia kumbadilisha, Ndugu Martin. Je, inaweza kuwa kwa ajili yao pia? Luther alikuwa amesoma akili zao. Alikuwa ameingia kwenye mimbari akiwa amejiandaa vizuri kujibu swali lao.
Lakini Injili ni nini? Ni hii, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe ulimwenguni ili kuwaokoa wenye dhambi, Yohana 3: 16, na kuiponda jehanamu, kushinda kifo, kuondoa dhambi na kutosheleza sheria. Lakini unapaswa kufanya nini? Hakuna ila kulikubali hili na kumtazama Mkombozi wako na kuamini kwa uthabiti kwamba amefanya haya yote kwa ajili ya mema yako na anakupa yote bure kama yako mwenyewe, ili katika hofu ya kifo, dhambi na jehanamu, unaweza kusema kwa kujiamini na kwa ujasiri ukimtegemea, na kusema: Ingawa sitimizi sheria, ingawa dhambi bado ipo na ninaogopa kifo na jehanamu, hata hivyo kutoka kwenye Injili ninajua kwamba Kristo amenikirimia matendo yake yote. Nina hakika hatadanganya, ahadi yake hakika ataitimiza. Na kama ishara ya hili nimepokea ubatizo.
Juu ya hili naiweka imani yangu. Kwa maana najua kwamba Bwana wangu Kristo ameshinda kifo, dhambi, jehanamu na shetani kwa manufaa yangu. Kwa maana alikuwa hana hatia, kama Petro anavyosema: “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake.” 1 Petro 2, 22. Kwa hiyo dhambi na mauti hayakuweza kumwangamiza, kuzimu hakukuweza kumshikilia, na amekuwa Bwana wao, na amewapa haya kwa wote wanaokubali na kuamini. Yote haya hayajatekelezwa kwa kazi zangu au wema wangu; bali kwa neema safi, wema na rehema.6
Luther aliwahi kusema, “Kama ningeweza kuamini kwamba Mungu hakuwa na hasira na mimi, Ningesimama juu ya kichwa changu kwa furaha.” 7 Labda siku hiyo hiyo baadhi ya wale waliomsikia akihubiri waliitikia na wakapata kuhisi “kujiamini” alikozungumzia. Nani ajuaye ila baadhi ya wasikilizaji wachanga baadaye nao pia waliwaandikia marafiki zao na kuwaambia kwamba walikwenda nyumbani na kusimama juu ya vichwa vyao kwa furaha?
Ujumbe wa Mhariri: Chapisho hili ni dondoo kutoka kwa The Legacy of Luther na lilichapishwa kwa mara ya kwanza tarehe 29 Oktoba, 2018.
- Nukuu inayojirudia katika Luther, kwa mfano, Luther: Lectures on Romans, 127, 208, 322.
- LW, 54:127.
- Kwa marejeleo mengi ya kanuni hii katika Luther, angalia Walther von Loewenich, Luther’s Theology of the Cross, tafsiri. Herbert J.A. Bouman (Minneapolis: Augsburg, 1976), 112–43.
- Luther, Tahariri ya Waraka wa Mt. Paulo kwa Wagalatia, 558.
- Ibid., 559.
- Mahubiri kamili ya Martin Luther, 1.2, 373.
- WA,176.6f, iliyotajwa na Oberman,Luther:Man between God and the Devil ,315
Makala haya yalichapishwa kwanza katika Blogu ya Huduma za Ligonier.